Ukweli kuhusu shilingi ya Tanzania kuimarika

Ukweli kuhusu shilingi ya Tanzania kuimarika

Muktasari:

  •  Shilingi ya Tanzania imeongezeka thamani dhidi ya dola ya Marekani kwa wiki mbili zilizopita kutokana na kuimarika kwa sekta ya utalii, uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na fedha za wabia wa maendeleo.


Dar es Salaam. Shilingi ya Tanzania imeongezeka thamani dhidi ya dola ya Marekani kwa wiki mbili zilizopita kutokana na kuimarika kwa sekta ya utalii, uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na fedha za wabia wa maendeleo.

Wiki mbili zilizopita, taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zilionyesha dola moja ilinunuliwa na kuuzwa kati ya Sh2,288 na Sh2,310 lakini imeendelea kuimarika na kufika kati ya Sh2,284.9 na Sh2,307.75.

Hata kwenye benki za biashara nako hali inaimarika kwani awali ubadilishaji wa dola moja huuzwa na kununuliwa kwa kati ya Sh2,313 na Sh2,337.5 lakini jana ilionyesha kuwa kati ya Sh2,290 na 2,320.

Kuimarika kwa Shilingi dhidi ya dola ambapo ununuzi wa kimataifa unafanyika, inamaanisha bidhaa za ndani zinazoingizwa kutoka nje ya nchi yakiwemo mafuta na bidhaa za petroli, mafuta ya kula, nguo na nyinginezo haziathiriwi na sarafu ya nchini.

BoT imetabiri kuendelea kuimarika kwa shilingi kwa miezi ijayo ikisema kuimarika huko kulianza Julai.

Mkurugenzi wa utafiti wa uchumi wa BoT, Dk Suleiman Missango alisema kuimarika huko kunamaanisha waagizaji na waingizaji wa bidhaa watanufaika zaidi kipindi hiki.

Alisema tangu Julai kumekuwa na ongezeko la fedha za kigeni kutoka Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF). Septemba 7, IMF iliidhinisha mkopo wa dharura wa dola 567 milioni kwa sekta ya afya ili kuinua uchumi ulioathiriwa na Uviko-19.

Kati ya fedha hizo, dola 189 milioni zilitolewa kwa mfumo wa mikopo ya haraka, huku dola 378 milioni zikitolewa kwa nchi wanachama zenye mahitaji muhimu ya malipo.

Fedha hizo zililenga kulipia malipo ya muhimu kwa ajili kupambana na Uviko-19, ikisema ugonjwa huo ulisababisha kuanguka kwa sekta ya utalii na hivyo kukawa na mahitaji ya haraka ya fedha.

Kwa mujibu wa Dk Missango, kumekuwa pia na ongezeko la upelekaji wa bidhaa nje ya nchi kwa miezi michache iliyopita wakati utalii nao ukiimarika wakati ambao dunia inapata unafuu wa janga la Uviko-19.

Taarifa ya BoT ya miezi ya hivi karibuni (MER) inaonyesha kuwa Tanzania iliingiza dola 2.941 bilioni kutokana na biashara ya dhahabu kwa mwaka ulioishia Agosti 2021, likiwa ni ongezeko la dola 2.735 bilioni kwa kipindi cha mwaka mmoja.