Ulega ataka wananchi washirikishwe mipango ya maendeleo

Muktasari:

  • Naibu Waziri Ulega amewataka watumishi wa umma wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara kuwashirikisha wananchi katika mipango ya maendeleo.

Kiteto. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amewataka watumishi wa Serikali wilayani hapa kuhakikisha wanatatua migogoro kabla haijafika ngazi za juu.

Naibu Waziri Ulega ameyasema hayo leo Februari 18, 2023 mjini Kibaya wakati akizungumza na watumishi wa Serikali katika ziara yake ya siku moja wilayani Kiteto iliyolenga kukagua maendeleo ya mifugo.

 "Changamoto zinazojitokeza ikiwemo migogoro ya wakulima na wafugaji ni kutokana na baadhi ya viongozi wa Serikali kutoshirikisha wananchi katika kupanga na kutekeleza maendeleo yao,” amesema.

Amewataka watumishi hao kuwashirikisha wananchi katika kupanga mipango yao ya maendeleo ili kuepusha migogoro hiyo.

Akieleza migogoro ya ardhi inayowakabili wananchi wilayani Kiteto, Mkuu wa wilaya hiyo, Mbaraka Batenga amesema, tatizo sio ardhi bali ni watu kushindwa kuheshimu mipango yao walioamua wenyewe.

"Niliwahi kusema mara nyingi tu kuwa, Kiteto tulipaswa kupimwa akili zetu kujua kama tunazo, kwani pamoja na kuwa na eneo ni kubwa, lakini watu wanashindwa kulitumia kwa misingi ya ubinafsi na uchoyo,” amesema.