Ulimwengu wa Kiislam wampoteza mwanazuoni

Sheikh Yusuf Qaradawi

Muktasari:

Ni sheikh Yusuf Qaradawi mzaliwa wa Misri aliyekuwa akiishi nchini Qatar

Dar es Salaam. Ulimwengi wa Kiislam, umempoteza mmoja wa wasomi aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika dini ya Kiislam.

Ni sheikh  Yusuf Qaradawi aliyefariki leo Jumatatu Septemba 26, 2022 akiwa na umri wa miaka 96. Aliwahi kuwa mwenyekiti wa umoja wa kimataifa wa wanazuoni wa Kiislamu

Taarifa za kifo chake zilitangazwa kupitia ukurasa wa mtandao wa twitter wa Umoja wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu (IUMS), pamoja na ile ya mwanawe, Abdul Rahman Yusuf al-Qaradawi.

Al-Qaradawi alizaliwa mwaka wa 1926 nchini. Wakti nchi hiyo ikiwa bado chini ya ukoloni wa Uingereza, alichanganya elimu ya dini na harakati za kupinga ukoloni wakati wa ujana wake.

Harakati zake dhidi ya uvamizi wa Uingereza na baadaye, ushirika wake na Muslim Brotherhood ulisababisha kukamatwa kwake mara kadhaa  miaka ya 1950s.

Atakumbukwa kwa maandiko yake mbalimbali yaliyotoa elimu juu ya dini ya kiislamu ambayo yamekuwa marejeo maarufu  kwa Waislamu duniani kote.

Moja ya andiko lake, "Halali na Haramu katika Uislamu", limetafsiriwa katika karibu lugha nyingi, na inachukuliwa kuwa moja ya rejea kuu  kwa Waislamu ulimwenguni

Mwaka 2009, serikali ya Malaysia ilimkabidhi tuzo ya "Tokoh Maal Hijrah", ambayo inawatambua mchango wa kazi au huduma zilizofanywa na watu mbalimbali sambamba na mwaka mpya wa Kiislam.

Mwenyekiti wa Halmashauri kuu ya Baraza la Waislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka amesema Waislamu wamepoteza mtu ambaye alikuwa ni hazina muhimu katika masuala ya elimu ya dini ya Kiislamu.

“Katika maisha yake alikuwa ni mtu ambaye alitumia muda wake kutangaza na kufundisha dini pia ameandika maandiko mbalimbali ambayo ni hazina kwa Waislamu, kikiwamo kitabu cha Halali na Haramu katika Uislamu,”amesema.