Unafiki usipodhibitiwa utaumiza taifa

Thursday April 08 2021
MAONIPIC
By Daniel Mjema

Kwa miaka mitano na ushee, tumeshuhudia kuibuka kwa kundi ambalo nasema ni la watu wanafiki, ambao husifia hata pale pasipostahili kusifia huku wakigeuza ukosoaji kuwa usaliti na kupongeza hata pasipostahili kukabatizwa ni uzalendo.

Leo hii Rais wetu, Samia Suluhu Hassan anapojaribu kurejesha upendo, umoja wa kitaifa na mshikamano na kuukabili wizi na ubadhirifu, kundi lilelile lililowabatiza waliokosoa mambo hayo yakitokea kuwa ni wasaliti, limebadili gia angani.

Tabia za aina hii hazina tafsiri nzuri zaidi ya kwamba kundi la aina hii ni la watu wanafiki ambao wako tayari kumwaminisha mfalme kuwa hili ni shati wakati ni gauni, na ukilitizama kwa undani ni kundi lililotanguliza maslahi binafsi mbele.

Mfano mzuri ni wakati wa kupitisha sheria ile ya madini ya mwaka 2010, wapo wabunge hasa wa upinzani waliikosoa sana kwa maslahi mapana ya nchi, lakini wapo wabunge wa CCM waliowananga na kuiunga mkono kwa mbwembwe.

Lakini mwaka 2015 alipoingia madarakani Rais wa tano, hayati John Magufuli na kuikosoa vikali sheria ileile, ni kundi lilelile la wabunge wa CCM waliopiga makofi kuipitisha 2010 ndio hao hao waligeuka na kumpongeza Rais.

Naomba nikushauri Rais wangu, kama kweli unataka kuliongoza taifa hili kwa haki na kuacha kumbukumbu inayoishi (legacy), kaa mbali na kundi hili la watu wanafiki na wengine hata sasa ninapokushauri, pengine wapo waliokuzunguka.

Advertisement

Tulipopaza sauti kusema misingi ya umoja wetu wa kitaifa inatikiswa, ni kundi hilo hilo lilinyanyuka na kubatiza watu kuwa ni wasaliti na tuliposema Watanzania kuna mbegu za ubaguzi wa kiitikadi zinapandikizwa, ni kundi hilohilo lilipinga.

Tuliposema misingi ya utawala bora inayoheshimu utawala wa sheria inatikiswa, ni kundi hilo hilo lilibatiza watu majina kuwa wanatumika na mabeberu, lakini ulipotoa tu hotuba yako ya kwanza, kundi hilohilo likageuka na kukuunga mkono.

Ndiyo maana nimetangulia kusema unafiki na kujipendekeza ndiko kutaliangamiza taifa letu na nikusihi sana Rais wangu, usipokuwa makini litakufanya kama yule mfalme aliyekuwa uchi lakini mawaziri waliomzunguka wakasema hakuwa uchi.

Kisa hiki ni mashuhuri sana, pale mfalme alipotaka ashonewe vazi ambalo angewakoga wananchi wake, fundi aliyeshinda zabuni ya kulitengeneza akamwambia wale wasio na dhambi tu ndio watakaoweza kuliona vazi hilo.

Mbiu ikapigwa kuwa kesho yake mfalme angepita barabarani kutambulisha vazi lake jipya, siku ya siku akajitokeza akipita uchi ila yeye akaamini amevaa nguo, hadi mtoto mdogo alipopaza sauti kuwa hee mbona mfalme yuko uchi.

Kwa hiyo ndani ya wasaidizi wako watakaokuwa wanakuzunguka, wapo ambao watakuwa tayari kukuambia hili ni shati badala ya gauni, kama watakusoma na kuona ni mtu unayependa sifa na pongezi hata pale mambo yanapokwenda mrama.

Ni mambo matano tu yatakayokufanya uliongoze taifa hili kwa haki, ufanisi na kuacha legacy nayo ni kutenda haki kwa watu wote, kuwaweka kando wanafiki, teua wasaidizi wanaojali maslahi ya taifa badala ya matumbo yao na familia zao.

Hakikisha unajenga taasisi imara (strong institutions) na hii itawezekana tukiwa na katiba mpya, kuwa na Bunge imara na huru linaloisimamia serikali na kisha ruhusu uhuru wa vyombo vya habari na asasi za kiraia zitekeleze majukumu yao.

Mbali na hivyo, ruhusu shughuli za vyama vya siasa kufanyika kwa mujibu wa katiba yetu na sheria za nchi na vichukulie vyama vya upinzani kama jicho lako la pili kama itakavyokuwa vyombo vya habari na asasi zisizo za kiraia nchini.

Wala usione nongwa Rais kuanza na jitahidi sana kusimamia utawala wa sheria utamalaki katika nchi yetu, kwani ikiwa hivyo, Tanzania na watu wake ni rahisi sana kuwaongoza kwa sababu tayari Mwalimu Nyerere alishatuwekea misingi. Tangazo la UN la mwaka 1948 kuhusu haki za binadamu linatahadharisha kwamba watu wanaweza kulazimika kuasi ili kupinga dhuluma na ukandamizali ambayo hutokea pale tu utawala wa sheria unapokosekana au kupuuzwa.

Rais wa Marekani (1801-1809), Thomas Jefferson aliwahi kusema na hapa namnukuu “when injustice becomes law, resistance becomes duty”, akimaanisha udhalimu unapokuwa sheria basi kupinga nako kunageuka wajibu.

Rais Samia ameanza vizuri sana, hasa katika dhamira yake ya haki haki haki na kuliunganisha taifa na kusimamia utawala wa sheria, tunaamini dhamira yake hii haitabadilika ili aweze kuwaachia Watanzania kumbukumbu inayoishi.

Advertisement