Upelelezi kesi ya raia wa Ufaransa, mawakili wawili wakamilika

Watu saba wafikishwa kortini wakidaiwa kujipatia Sh 428milioni mali ya Tanesco

Muktasari:

Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili raia wa Ufaransa, Bernad Bougault na mawakili wawili wanaokabiliwa na shtaka la kughushi nyaraka umedai upelelezi umekamilika.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili raia wa Ufaransa, Bernad Bougault na mawakili wawili wanaokabiliwa na shtaka la kughushi nyaraka umedai upelelezi umekamilika.

Mbali na Bougault, washtakiwa wengine ni Respicious Mukandala na Simphorian Kitare ambao wanaokabiliwa na shtaka hilo.

Wakili wa Serikali, Tuli Helela aliieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na ameomba kesi hiyo ipangwe tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mwandamizi, Francis Mhina aliahirisha hadi Juni 21, 2022 kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Februari 18, 2020 katika mtaa wa Samora washitakiwa hao kwa pamoja walighushi nyaraka zilizoonyesha kuwa Kapteni Phillipe Gerniers amemchagua Boulgault kuwa mwakilishi wake kisheria na wakala wake.

Katika hati hiyo ilionyesha Gerniers amempa Boulgault mamlaka ya kufungua mashtaka kwa ajili ya mali zake zilizoko katika Hoteli ya Bagamoyo Beach au alipwe kiasi cha dola za Marekani 80,000 kwa niaba yake huku wakijua nyaraka hizo sio za kweli.