Urembo wa miwani unavyoandaa walemavu wa macho watarajiwa

Urembo wa miwani unavyoandaa walemavu wa macho watarajiwa

Muktasari:

  • Mgonjwa mmoja kati ya watatu wa macho, ameathiriwa na uvaaji wa miwani za lenzi kama urembo.

  

Dar es Salaam. Mgonjwa mmoja kati ya watatu wa macho, ameathiriwa na uvaaji wa miwani za lenzi kama urembo.

Kwa mujibu wa Programu ya Taifa ya Uangalizi wa Macho chini ya Wizara ya Afya, idadi ya wagonjwa wa macho katika kundi la upeo mdogo wa macho unaorekebishika kwa miwani, imeongezeka kutoka asilimia 32.69 ya milioni 1.3 mwaka 2019 hadi asilimia 35.11 ya milioni 1.2 mwaka 2020. Hawa ni wale waliofika vituo vya afya.

Hii inamaanisha, kila baada ya saa moja kulikuwa na wastani wa wagonjwa 136 waliothibitishwa katika vituo vya afya kwa ajili ya matibabu kwa mwaka jana, ikilinganishwa na wastani wa wagonjwa 148 kila baada ya saa waliofika katika huduma za afya kwa mwaka 2019.


Uvaaji miwani

Pamoja na tishio hilo la takwimu, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwapo kwa wimbi kubwa la uvaaji wa miwani hizo kwa vijana hususani mabinti, kwa lengo la kuongeza mvuto.

Hellena Peter, mkazi wa Tabata Kimanga jijini Dar es Salaam kwa sasa ni miongoni mwa waathirika wa macho aliyethibitishwa na watalaamu wa afya. Alivaa miwani hizo kuanzia mwaka 2020 hadi mwishoni mwa jana. Watalaamu wa afya walimwambia tatizo lake limesababishwa na uvaaji wa miwani.

“Nilinunua miwani yangu kwa machinga nikiwa mkoani Mbeya kimasomo, nilinunua kama urembo tu. Baada ya miezi minane nikaanza kusikia macho yakivuta, mishipa ya kichwa inaumia. Nikaamua kwenda hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya Desemba (2020) kupima,” anasema Hellena.

“Majibu yangu ninayo (ambayo gazeti hili linathibitisha), kwa sasa ninajutia. Sitaki tena kusikia habari za miwani. Nimetumia gharama ya Sh150, 000 vipimo, matibabu na miwani kwa urembo ulionigharimu. Nashaauri tuepuke uvaaji wa miwani za lenzi bila kupima macho.”

Mwingine ni Kelvin Salehe aliyetumia miwani ya kuzuia mwanga wa jua kwa muda wa mwaka mmoja, kabla ya kupatwa na changamoto ya uoni hafifu.

“Sikuwa na changamoto yoyote ya macho, nilitumia miwani hiyo kwa kufuata mikumbo ya marafiki ila baada ya muda nikawa na uoni hafifu ikanilazimu kuvaa miwani maisha yangu yote,” alisema.

Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Gaudensia Simwanza, anatoa tahadhari kuhakikisha kila anayenunua miwani awe amepata ushauri kwa wataalamu.

Simwanza anasistiza miwani za macho hutolewa na wataalamu maalum wa macho wenye kampuni zilizosajiliwa na mamlaka hiyo kuagiza na kuuza miwani hizo.

“Mamlaka tumejipanga kutoa huduma bora salama na fanisi na huwa tunapita kwenye vituo kukagua utoaji wa huduma hizo,’’ alisema.


Tatizo, tahadhari

Clement Mugisha, daktari bingwa wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Hospitali ya Aga Khan, alisema uvaaji wa miwani bila vipimo unaweza kuathiri mishipa ya fahamu inayopeleka taarifa katika ubongo wa nyuma ambao hutafsiri picha inayoonekana.

“Kesi zipo nyingi, ni hatari sana mtu kujivalia tu miwani bila vipimo, madhara yake yanaweza kujitengeneza na kuonekana baada ya kipindi cha muda fulani,” alisema Dk Mugisha.


Programu ya Taifa ya Uangalizi wa Macho

Meneja wa program hiyo, Dk Bernadetha Shilio anasema athari za muda mfupi baada ya kuanza kutumia miwani bila kufanyiwa vipimo ni pamoja na kuathiri asione kwa kiwango kinachotakiwa kwani nguvu ya miwani haiendani na hali ya macho yake.

“Anaweza kuwa ana tatizo lingine la macho lisilohitaji miwani na akachelewa kutambulika na kupata tiba sahihi kwa wakati huo, mfano, mtoto wa jicho, kisukari kwenye macho na shinikizo la jicho ambayo dalili zake zinaweza kuwa sawa na dalili za mtu mwenye uhitaji wa miwani,” alifafanua.

Dk Bernadetha alisema mwanachi anapaswa kufanyiwa kwanza vipimo ili kufahamu afya yake ya macho ikiwemo uwezo wa kuona, kiwango cha presha ya jicho, afya ya kioo cha ndani cha jicho na afya ya pazia la jicho ili kuhakikisha mgonjwa hana tatizo lingine la macho.

Hatua hiyo pia itasaidia kuwa na vipimo sahihi vya lensi iwapo atahitajika kupata tiba ya miwani, ni muhimu mgonjwa kufanyiwa vipimo kituo cha tiba na baada ya kupata miwani, bado anahitajika kupima macho kila mwaka,”alisema.

“Lengo ni kuhakikisha ile hali ya afya ya mwanzo bado ni hiyo au imebadilika, na pia uwezo wake wa kuona kwa kutumia miwani aliyopewa awali utahakikiwa iwapo hakuna mabadiliko.”

Martine Peter wa Kigamboni ni mwathirika wa macho alisema kuna kundi la wagonjwa wa macho lakini hununua miwani kwa machinga kwa kigezo cha gharama nafuu, wakijua miwani yoyote ya lensi itawasaidia lakini wengi wao hununua kama urembo bila kujua uwezo wa lenzi utaathiri macho yao.

Martin anatumia miwani ya lenzi na nyingine kwa ajili ya kuzuia mwanga wa jua na vumbi wakati akiendesha bodabodabo yake. “Nilipima kwa daktari lakini hii ya mwanga wa jua nilinunua tu.”


Biashara mtaani

Machinga wa miwani katika masoko ya Kariakoo, Manzese na Ubungo jijini Dar es Salaam walithibitisha kujihusisha na uuzaji pia wa miwani zenye lensi bila ya kuwa na utaalamu, wakati TMDA ikisisitiza miwani hizo zinatakiwa kuuzwa katika vituo vyenye watalaamu pekee.

Ismail Abdalah, machinga mwenye uzoefu wa miaka 10 ya kuuza miwani katika Jiji la Dar es Salaam, alithibitisha kuuza miwani zenye lensi za namba kwa wateja wake na imekuwa hivyo kwa miaka mingi lakini wachache huenda na vyeti vya watalaamu ili kupata miwani hizo.

“Mteja ananunua miwani akishaona imekaa vizuri usoni, hawezi kujua palepale kama ina lenzi yenye namba au haina na kwa upande wangu siwezi kuacha kuuza kwa sababu huwezi kujua anavaa yeye au anaipeleka wapi,” alisema Abdalah anayenunua miwani hizo madukani kwa bei ya jumla.

Shukrani Makene pia ni machinga aliyedai ni changamoto kuacha pesa kwa mteja asiye na cheti cha afya .

“Wateja saba kati ya kumi ni mabinti kila siku, ninauza miwani kati ya Sh2000 hadi Sh6,000, ninauza miwani za urembo zaidi kuliko za mwanga wa jua na fremu kwa wanaotaka kuweka lenzi.”