Uspika unavyogeuzwa kuwa kazi rahisi

Muktasari:

  • Katika mihimili mitatu ya dola, Bunge hutambulika kama “supreme organ”, yaani mhimili mkuu. Ni kwa sababu Bunge linaisimamia na kuishauri Serikali cha kufanya. Bunge linatunga sheria ambazo zinatafsiriwa na Mahakama.

Katika mihimili mitatu ya dola, Bunge hutambulika kama “supreme organ”, yaani mhimili mkuu. Ni kwa sababu Bunge linaisimamia na kuishauri Serikali cha kufanya. Bunge linatunga sheria ambazo zinatafsiriwa na Mahakama.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 84 (8), inaelekeza kuwa hakuna shughuli yoyote itakayotekelezwa bungeni kama kiti cha Spika wa Bunge kitakuwa wazi, isipokuwa uchaguzi wa Spika.

Tafsiri; kama kiti cha Spika wa Bunge kipo wazi maana yake hakuna Bunge. Hivyo, mtu ambaye anabeba dhima ya kiti cha Spika, anapaswa kufanana na hadhi ya ukuu wa mhimili huo ambao Magharibi huuita “August House” – “Nyumba Adhimu”.

Ni kutokana na uzito wa kiti cha Spika wa Bunge, ndio maana miaka ya nyuma watu waliogopa kukimbilia uspika. Ajabu ya sasa, makumi ya watu wamekimbilia fomu za Chama cha Mapinduzi (CCM), wakiomba kuteuliwa kugombea uspika.

Utitiri wa wanachama wa CCM waliojitokeza kuutaka uspika ni kipimo dhahiri kwamba watu wengi, pengine, wanaona kazi hiyo imekuwa nyepesi, kwa hiyo kila mtu anaiweza. Yaani watu hawajaona maajabu yoyote ya kumfanya aogope.

Jinsi watu wengi wanavyoutaka uspika kupitia CCM, ni kipimo kuwa nchi inazihama zile nyakati za wananchi kutafakari na kupima mtu ambaye anaweza kuwaongoza, kisha wao ndio wanajitoa kwenda kumshawishi ili akubali kugombea. Sasa hivi, kama hujitokezi hakuna wa kukufuata.

Upo mtazamo mwingine kwamba pengine Spika wa Bunge aliyepita, Job Ndugai alishindwa kufanya kazi yake sawasawa, kwa hiyo watu wengi wameona wajitokeze kwa wingi ili kwenda kusahihisha makosa. Hii pia inaweza kuwa nadharia mojawapo.

Yupo mtu anaweza kuona kuwa uspika imekuwa kazi yenye ulaji ulionona. Mamlaka makubwa. Unaweza kumkalisha kimya yeyote au kumketisha chini umtakaye. Hapohapo, wanaona Spika wa Bunge aliyepita hakufanya maajabu yoyote. Kwa hiyo, inashawishi kila mtu kuwania hiyo kazi.

Kama Spika wa Bunge aliyepita angeonyesha utumishi wa kipekee, pengine kuna watu wangeogopa kugombea kiti chake. Lazima watu wangekuwa wanajitathmini kwanza uwezo wao. Na kungekuwa na woga wa kuzikimbilia fomu za kuwania ubunge.

Kuna mtu kajitokeza kutia nia, huku kichwani akiwaza “sasa fulani ameonesha nini ambacho sikiwezi?” Si ajabu katika kundi kubwa la wanaotaka uspika, idadi ya waliotangaza kugombea baada ya kujiuliza swali hilo, ikawa ni kubwa.

Hapa ni changamoto kwa Job Ndugai, anapaswa kujiuliza; kwa nini watu wengi wamekimbilia uspika kwa idadi kubwa kuwahi kutokea baada ya yeye kujiuzulu?

Je, ameufanya uspika kuwa kazi pendwa yenye kukimbiliwa na wengi au ameshusha hadhi kiasi kwamba inaonekana ni kazi ya yeyote.

Soma zaidi: Spika Ndugai ajiuzulu

Ukweli usiofichika ni kuwa kama Ndugai angetengeneza hadhi ya juu katika kiti cha Spika wa Bunge, bila shaka kungekuwa na woga kwa watu wengine kukimbilia.

Mbona watu hawakuukimbilia uspika kwa wingi baada ya Chifu Adam Mkwawa, Chifu Erasto Mang’enya, Pius Msekwa, Samuel Sitta au Anne Makinda? Kwa nini baada yake?

Kama Donald Trump alivyofanya kazi ya urais wa Marekani ionekane inaweza kufanywa na yeyote mpaka mwanamuziki wa hip hop mwenye vioja vingi, Kanye West akatangaza nia ya kuwania urais kwenye Uchaguzi wa Rais Marekani Novemba 2020, ndivyo na mtu aliyejipatia umaarufu mitandaoni kwa kuzungumzia maisha ya kimapenzi ya watu wengine, Mwijaku, naye ameona anaweza kufanya kazi ya Ndugai bungeni?

Kuna jingine; mfumo wa uteuzi serikalini umekuwa ukiwaelekea makada wa CCM wenye kuonekana. Wakuu wa wilaya, maofisa tawala wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, waliopo sasa, wengi wao ni makada wa CCM walioonekana baada ya kugombea nafasi mbalimbali katika hatua za awali. Hasa ubunge.

Katika hali hiyo, wana CCM 71 waliochukua fomu ya kuutaka uspika na 70 kufanikiwa kurejesha, wanaweza kuwa wamejitokeza kwa wingi wakiamini kuwa hata kama hawatashinda, basi watajiweka kwenye mazingira mazuri ya kupata uteuzi wa nafasi nyingine za uongozi. Ni sawa na ule msemo wa “lenga mwezi, ukikosa unaweza kuangukia nyota”. Wanalenga uspika. Kama watapigwa mweleka, hawatakosa kabisa. Zipo nafasi nyingine za uteuzi.

Siku hizi CCM wana msemo wa “kujipitisha ili uonekane na ujulikane”. Hivyo, jukwaa la kutia nia kuna watu wanalitumia kujipitisha, angalau watambulike kama nao wana dhamira ya kushiriki uongozi wa nchi. Basi, na kwa kujipitisha kwao waonekane na wateuliwe.

Kwa vyovyote vile, wingi wa wanaoutaka uspika, hasa CCM, ni tafsiri ya hali ya siasa za nchi kwa sasa. Jinsi watu wasivyoogopa kukimbilia uspika, ni dhahiri siku hizi kazi ya uwakilishi na usimamizi wa Serikali, inachukuliwa kama fursa ya kimaisha. Ubunge umekuwa njiapanda ya kufanikisha mipango mingine ya kimaisha. Kwa maana hiyo, huhitaji kuwa mtu maalumu sana kuongoza wabunge na mhimili wa Bunge.

Nchi inapaswa kurudi kwenye nyakati za misingi. Kipindi ambacho, ukiitwa mbunge, hadhi yako haitafutwi, bali inajionesha. Siku hizi kuna wabunge wanaonesha vitendo au kutamka maneno ya kihuni, hata wahuni wanaweza kuogopa kutamka. Tena wanatamka chini ya kinga ya kutoshitakiwa. Na Spika wa Bunge anacheka. Nani angeogopa uspika leo?

Si ajabu, wapo watu wenye heshima zao, wanaogopa kujiingiza kwenye kinyang’anyiro cha uspika kwa sababu wanahisi hadhi zao zinaweza kushuka kutokana na hulka za baadhi ya wabunge na vitendo vyao bungeni. Ukiwa kiongozi wa wabunge wasiojiheshimu, wewe utaheshimika vipi? Ni hivi; utitiri wa wanaoutaka uspika ni kipimo kikubwa mno cha hadhi ya Bunge kuporomoka.

Hili si la kukwepa; Ndugai alijiuzulu uspika baada ya kutofautiana kauli na Rais Samia Suluhu Hassan. Na Spika wa Bunge ndiye mkuu wa Bunge, ambao ni mhimili wenye wajibu wa kuisimamia Serikali. Kwa maana suala la mgongano kati ya Serikali na Bunge halikwepeki kama kila mhimili utafanya kazi yake vizuri.

Kuna swali; hawa watu wengi waliojitokeza kugombea uspika, wao wanakimbilia kuwa watiifu kwa Rais Samia au wanajiona wana msuli wa kushindana na Rais hata kama kutatokea mgongano baina yao?

Inapotokea mgombea uspika anaanza kumsifia Rais (mkuu wa mhimili wa Serikali), unadhani akichaguliwa kuongoza kiti hicho ataweza kubadilika na kuidhibiti Serikali?