Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utafiti na ubunifu UDSM waongoza mapinduzi ya ujasiriamali kwa wahitimu

Wadau mbalimbali wakisikiliza wasilisho la Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Nelson Boniface, katika maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu, June 9, 2026.

Muktasari:

  • Uwekezaji wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika utafiti na ubunifu unaendelea kuzaa matunda, huku asilimia 19 ya biashara mpya nchini zikianzishwa na wahitimu wake.

Dar es Salaam. Katikati ya mjadala wa changamoto ya ajira kwa vijana nchini, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimebadili njia ya kuwezesha wahitimu wake.

Badala ya kuwaandaa kutegemea ajira rasmi, sasa wahitimu wa UDSM wanatengeneza ajira zao kupitia tafiti na ubunifu unaotolewa na chuo hicho kwa wanafunzi wake.

Takwimu zilizowasilishwa katika Maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya chuo hicho, leo Jumanne, June 9, 2026, zinaonesha asilimia 19 ya biashara zinazoanzishwa nchini hadi mwaka 2025 zimeanzishwa na wahitimu wa UDSM.

Hali hii inaashiria uwekezaji katika utafiti, ubunifu na ujasiriamali ni hatua muhimu katika kubadilisha mwelekeo wa wahitimu katika soko la ajira mara wanapohitimu masomo yao.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Utafiti, Profesa Nelson Boniface amesema maadhimisho ya utafiti na ubunifu yamekuwa chachu ya kuwaibua watafiti na wabunifu pamoja na kuyapa mwonekano matokeo ya kazi zao.

“Hii imejidhihirisha kwa ukuaji wa ubunifu kupitia machapisho yao, ambapo kwa UDSM tuna ukuaji wa asilimia 11, kiwango cha juu zaidi duniani,” amesema Profesa Boniface.

Kwa miaka mingi, vyuo vikuu vilitazamwa zaidi kama maeneo ya kuzalisha watafuta ajira.

Hata hivyo, mwenendo unaoonekana UDSM unaashiria mabadiliko ya kimkakati ambapo elimu, utafiti na ubunifu vinaanza kutumika kuwaandaa wanafunzi kuwa wabunifu wa suluhisho la changamoto ya ajira nchini.

Profesa Boniface amesema ushahidi wa mabadiliko hayo unaonekana kwa wahitimu wengi wanaotumia maarifa waliyojifunza chuoni hapo kuanzisha biashara katika sekta mbalimbali.

Amemtaja mhitimu wa mwaka 2021, Deus Mwami, ambaye ameonesha mafanikio kupitia ubunifu wake katika usanifu na mapambo, kiasi cha kupewa jukumu la kupamba ukumbi uliotumika katika maadhimisho hayo.


Mafanikio yavutia taasisi za fedha.

Kwa mujibu wa Profesa Boniface, CRDB Foundation katika huduma zake kwa vijana, ilibaini kuwa sehemu kubwa ya wafanyabiashara wadogo waliokuwa wakifanya vizuri walikuwa wahitimu wa UDSM, hali iliyochangia kuanzishwa kwa huduma maalumu ya mikopo nafuu kwa wahitimu wa chuo hicho.

“Zaidi ya wahitimu 800 wameomba mikopo hiyo kwa ajili ya kuendeleza biashara zao,” amesema.

Katika kuimarisha zaidi mazingira ya uzalishaji wa maarifa na kuchochea ubunifu huo, UDSM pia imeanzisha mfumo maalumu wa kuhifadhi kazi za kitafiti unaowezesha tafiti kufikiwa na kutumiwa na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Mfumo huo umezinduliwa rasmi na Waziri wa Madini wakati wa maadhimisho hayo, ukitajwa kama hatua muhimu itakayochochea tafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia nchini.


UDSM, Barrick Mining wasaini makubaliano

Maadhimisho hayo pia yameshuhudia kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya UDSM na kampuni ya Barrick Mining, yakilenga kuendeleza tafiti na ubunifu katika teknolojia za uchenjuaji wa madini na kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Meneja wa Taifa wa Barrick Gold Minerals, Dk Merikiole Ngido, amesema kampuni hiyo inaamini ushirikiano huo utafungua fursa mpya za ubunifu na kusaidia kuendeleza teknolojia za madini zitakazochangia maendeleo ya sekta hiyo.

Rehema James wa Udsm amefafanua makubaliank hayo kuwa ni mkataba wa Ushirikiano unaolenga kuchochea tafiti za kitaaluma na ubunifu katika sekta ya madini ili kuimarisha huduma za uchenjuaji wa madini nchini.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wahandisi Tanzania, Mhandisi Assah Mwaipopo, amesema Tanzania inapaswa kuwekeza zaidi katika tafiti na teknolojia ili kunufaika kikamilifu na rasilimali zake za madini na fursa za ushirikiano wa kimataifa.

Amesema, ukosefu wa ubunifu na teknolojia umeendelea kuyafanya mataifa yanayoendelea kushindwa kunufaika na fursa nyingi za rasilimali zake, akikipongeza Udsm kwa kuamua kuwekeza katika tafiti na ubunifu ambao matunda yake yameanza kuonekana.

"Tanzania inatakiwa kuwekeza vyakutosha katika tafiti za masuala ya nishati na madini ili kuwezesha uchakataji wa madini," amesema.