Utafiti waonesha asilimia 20 ya mbega wanaopatikana duniani wapo Burigi Chato

Muktasari:
Uwepo wa wanyama hao kunaifanya hifadhi hiyo kuwa ya kipekee kati ya hifadhi 21 zilizopo nchini.
Geita. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (Tawiri) pamoja na watafiti wa masuala ya Nyani kutoka nchini Uganda umebaini asilimia 20 ya mbega mwenye rangi ya kijivu na nyekundu wanaopatikana duniani wapo Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato.
Uwepo wa wanyama hao kunaifanya hifadhi hiyo kuwa ya kipekee kati ya hifadhi 21 zilizopo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni walipotembelea hifadhi hiyo ikiwa ni maandalizi ya tamasha la Chato Utalii Festival linalotarajiwa kufanyika Novemba 26 hadi Desema 3, 2023; Mhifadhi Mwandamizi kutoka Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato, Ombeni Hingi amesema mbega hao wameadimika maeneo mbalimbali duniani.
Amedai kuwepo kwa asilimia 20 katika hifadhi hiyo kumeifanya kuwa ya kipekee nchini na kwamba ipo haja ya tafiti nyingine kufanyika ili kubaini nini sababu zilizopeleka wanyama hao kutoweka katika maeneo mengine nchini.
“Ni wakati sasa ufanyike utafiti mwingine ili usaidie kujua idadi ya waliopo sasa maana kwenye utafiti wa awali walibaini eneo moja lakini makundi yameongezeka sasa yapo maeneo matatu ndani ya hifadhi watafiti watoe pia ushauri wa namna gani waendelee kuzaliana lakini wabaini sababu za kwanini waliondoka katika maeneo mengine,”amesema Hingi
Akizungumzia Hifadhi ya Burigi Chato ambayo ni ya nne kwa ukubwa nchini, yenye kilomita za mraba 4,707 iliyoanza mwaka 2019 baada ya kupandishwa hadhi kwa mapori ya akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi, Hingi amesema mbali na uwepo wa mnyama huyo hifadhi hiyo ina maziwa matano yanayo ongeza upekee wake ikilinganishwa na hifadhi nyingine ndani ya Tanzania.
“Hifadhi hii ina upekee wa kuwa na maziwa matano Burigi, Ngoma, Kasinga, Nyamalebe na Ziwa Victoria. Maziwa haya manne hayatambuliki kwakuwa hayajawekwa kwenye ramani ya nchi lakini ni makubwa mfano Burigi lina ukubwa wa hekta 7,000 na maziwa haya yameifanya hifadhi kuwa ya kipekee na kutoa mahitaji muhimu kwa wanyama na kuwa na malisho yanayopatikana wakati wote”amesema Hingi
Mbali na maziwa, hifadhi hiyo ina wanyama wakubwa wanne ambao ni Tembo, Simba, Chui na Nyati huku Serikali ikiwa mbioni kupeleka Faru mweupe na kuifanya kuwa na ‘bigi 5’ ambao ni kivutio kwa watalii.
Hingi amesema idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka ambapo kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2022/23 walikuwa na watalii 295 na kwa robo ya mwaka 2023/24 wameongezeka na kufikia watalii 493.
Kuhusu uwekezaji amesema wapo wawekezaji kutoka nje ya nchi walioonyesha nia ya kujenga ‘Lodge’ kwenye maji na kwamba uwekezaji huo utaongeza idadi ya watalii watakaotembelea hifadhi na kuifanya kuwa miongoni mwa hifadhi zenye ushindani katika kukusanya mapato kwa wingi nchini.
Mhifadhi huyo amewataka wafanyabiashara na wadau wa utalii kuwekeza kwenye hifadhi hiyo kwa kujenga nyumba za kulala wageni, huduma za chakula na kusafirisha wageni.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale amesema uwepo wa wanyama kwa makundi makundi kunadhihirisha uhifadhi mzuri uliopo kwenye hifadhi hiyo ambayo ni ya muda mfupi lakini ikiwa na hazina ya wanyama wengi.
Amesema hifadhi hiyo inawanyama ambao awali walikua hatarini kutoweka kutokana na uwindaji haramu uliofanya wanyama kuogopa watu lakini kutokana na kuendelezwa na kuhifadhiwa kumefanya wanyama waongezeke mara dufu.
“Hifadhi hii ni kivutuo kwa Tanzania na Dunia...rasilimali hii ni kwa manufaa ya nchi tunapozungumza ndani ya hifadhi kuna maziwa matano watu wanashangaa haya manne hawajayasikia lakini yapo ni wakati sasa maziwa haya yawekwe kwenye ramani yatambulike yafanyiwe tafiti maalum ili kuendelea kuhamasisha utalii wa ndani na nje ya nchi”amesema Katwale
Sekta ya utalii nchini huchangia asilimia 17 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni huku kwa mwaka sekta hiyo huiingizia Serikali mapato ya Sh400 bilioni.
Kwa mujibu wa ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza idadi ya watalii kutoka nje ya nchi imeongezeka kutoka watalii 900,182 kwa kipindi cha Januari hadi Agosti 2022 na kufikia watalii 1,131,286 kwa kipindi kama hicho mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 25.7 huku lengo la Serikali ni kufikia watalii million tano kutoka ndani na nje ya nchi ifikapo 2025.