Utani wa Simba na Yanga bungeni

Utani wa Simba na Yanga bungeni

Muktasari:

Ushindi wa goli 4-1 ilioupata Simba dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC) umefikishwa bungeni na mbunge wa Kinondoni (CCM), Abbas Tarimba akitaka moto wa timu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam kuigwa.

Dodoma. Ushindi wa goli 4-1 ilioupata Simba dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC) umefikishwa bungeni na mbunge wa Kinondoni (CCM), Abbas Tarimba akitaka moto wa timu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam kuigwa.

Tarimba ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 8, 2021 baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kulieleza Bunge kuwa walikuwa vizuri katika sikukuu ya Pasaka kutokana na ushindi wa Simba.

Mabao ya Simba katika mchezo huo uliopigwa katika uwanja  wa Benjamin Mkapa yalifungwa na Clatus Chama aliyefunga mawili na kutoa pasi moja ya bao, Luis Miquissone na Larry Bwalya.

Leo bungeni Ndugai alitoa kauli hiyo akimtania Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kwamba anatakiwa kusikiliza kwa makini.

"Niwaombe na wenzetu wa Yanga kuwa na moyo wa uzalendo kama sisi na ushindi ule unaisaidia nchi yetu na kuipa heshima zaidi," amesema Tarimba.

Kauli ya Tarimba ilipigiwa makofi na wabunge waliofurahishwa na ushindi wa Simba.

Hata hivyo, Mwigulu wakati akisoma mpango wa Serikali alijibu mapigo, akibainisha kuwa yeye aliteuliwa  kuiongoza wizara hiyo kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia alimteua Dk Philip Mpango kuwa makamu wa rais, ana imani na wana Yanga.