Utata vifo vya vijana watatu

Khatib Kabwele

Muktasari:

  • Utata umeghubika vifo vya vijana watatu wanaotuhumiwa kwa uhalifu, ambao ndugu wa marehemu wanadai walichukuliwa na polisi wilayani Temeke na miili yao ikakutwa baadaye hospitalini.


Dar es Salaam. Utata umeghubika vifo vya vijana watatu wanaotuhumiwa kwa uhalifu, ambao ndugu wa marehemu wanadai walichukuliwa na polisi wilayani Temeke na miili yao ikakutwa baadaye hospitalini.

Vifo hivyo vimetokea wakati polisi mkoani Mara wakilalamikiwa pia kuua watu watatu wilayani Serengeti waliodaiwa kuwa wahalifu, katika mazingira yanayofanana.

Katika matukio hayo mawili, familia za marehemu zimelalamika kuwa waliouawa hawakukutwa kwenye maeneo ya uhalifu, bali walichukuliwa nyumbani.

Tukio hilo limetokea zikiwa zimepita wiki mbili tangu Jeshi la Polisi Kanda Maalumu litangaze kuua watu sita, waliotajwa kuwa walikuwa wanakwenda kutekeleza tukio la kihalifu.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke Richard Ngole alipoulizwa kuhusu madai hayo alisema, suala hilo atafutwe Kamanda wa Polisi Kanda Maalum.

Kamanda wa Kanda Maalum Jumanne Muliro alipotafutwa hakutaka kuzungumzia vifa hivyo, bali alisema wananchi kwenye mtaa huo wamekuwa wakilalamikia baadhi ya vijana kujihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo uporaji na kufikia hatua ya kutaka kuchoma moto nyumba za wazazi wa vijana hao.

“Hiyo taarifa naendelea kuifuatilia nitaitolea taarifa, baadaye huo mtaa unaouzungumziwa wananchi wamekuwa wakiandamana kutaka kuchoma nyumba za wazazi wao, hatuwezi kuacha fujo ziendelee,” alisema Muliro.

Muliro aliongeza kuwa jeshi hilo limekuwa linalalamikiwa na wananchi kwa kuwaachia wahalifu ambao hurudi katika maeneo yao kuendelea na uhalifu.

“Maeneo mengi wananchi wamechoka hadi kufikia wakati wanataka kuwachoma moto, lakini sisi tunafanya kazi kubwa kuhakikisha wananchi na mali zao wanakuwa salama.”

Akizungumza juzi kwenye mjadala uliofanyika kwa njia ya mtandao, Kamanda Muliro amesema jeshi hilo hulazimika kutumia nguvu iwapo mazingira yanachochea hilo kutokea.

“Kila mtu ana haki ya kuishi ila inapotokea mmoja anataka kusababisha mwenzake awe kwenye mazingira ya hatari ya kutokuishi, pale ile nguvu inayotumika inahesabiwa kama nguvu ya kadri,” alisema.


Malalamiko ya ndugu

Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya ndugu wa marehemu wamesema ndugu zao walichukuliwa na watu waliojitambulisha ni askari polisi wakidai kuwapeleka kuwahoji lakini baadaye miili yao ilikutwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti wakiwa wameshafariki.

Mkazi wa mtaa wa Nyambwela, Tandika, Amina Ally alisema mwanaye Amir Hassan, (25) ambaye alikuwa akiishi naye alichukuliwa na polisi nyumbani kwao Septemba 17, saa 10 alfajiri.

Alisema baada ya kufika waligonga mlango, lakini alikataa kuwafungulia kwa kuwa ilikuwa usiku.

“Baada ya kuwaeleza hivyo walitishia kuvunja mlango, nikawaambia wasubiri nivae, walisukuma mlango na kufanikiwa kuingia ndani, wakavunja milango ya vyumba vitatu, kimoja kilikuwa na watoto wa kike na kingine alikuwa mwanangu Amiri.

“Walimkuta ndani amelala wakamwamsha kwa vibao na kumwambia ni mwizi na kwamba hata runinga waliyoikuta ndani ni ya wizi, wakaichukua na kuondoka nayo,” alisema Amina.

Alisema hata alipojaribu kujitetea na kuonyesha risiti ya duka alikoinunua Tandika Mei 29, mwaka huu, polisi hawakusikia wakaondoka naye.

Kulipokucha alisema walianza kufuatilia katika vituo vya polisi bila mafanikio hadi siku ikaisha, baadaye walikutana na mmoja wa vijana ambaye pia alikuwa amekamatwa, walipomuuliza aliwajibu kuwa wakimkosa waende vituo vingine vya polisi au hospitali.

“Tulizunguka vituo mbalimbali vya polisi na kwenye hospitali za rufaa za mikoa bila mafanikio, mwishoni tulienda Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuikuta maiti ya Amiri ikiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.”

Amina alisema walipouliza waliambiwa maiti hiyo na nyingine zilipelekwa pale na askari kutoka Kituo cha Maturubai, Mbagala.

“Walitwambia kama tunahitaji mwili wake twende kituoni (Maturubahi) ili waje kutukabidhi.

“Tuliporudi kituo cha Maturubai, tulielezwa gari halina mafuta, labda tutoe Sh20,000,” alisema na kufafanua kuwa walipozitoa wakakaenda kukabidhiwa mwili.

Mmoja wa majirani aliyejitambulisha kwa jina la Bakari Mussa alisema kijana huyo alikuwa akiishi mtaani bila matatizo ingawa alikuwa ni mtu anayependa kujichanganya na wenzake.

“Amiri hata kama alikuwa anavuta au kuuza bangi, lakini hakuwa panyarodi ndio maana polisi walimkuta nyumbani, alikuwa akitoka, baadaye anarejea nyumbani bila tatizo,” alisema.

Jirani mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema, “Amiri amekulia hapa tunamfahamu pamoja na marafiki zake alikuwa hana tabia hizo, kwanza yeye ndio alikuwa akiwasaidia ndugu zake kwa kuwa baba yake alishafariki.”

Katika tukio lingine lilitokea katika mtaa huohuo wa Nyambwela, imedaiwa Septemba 17 majira ya saa 12 asubuhi, polisi pia walimchukua Khatibu Kabwele ambaye pia baadaye mwili wake ulikutwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) .

Mjomba wa marehemu ambaye pia ni mwenyekiti wa Wazazi - CCM, mtaa wa Nyambwela, Sued Shoo alisema, askari hao walipofika waliulizia jina la Bahati, mwanamke aliyekuwa anaishi na Kabwele.

Alisema baada ya kumuelekeza, waliingia ndani na kutoka na Kabwele wakaondoka naye wakisema wana mazungumzo na atarudi baadaye.

“Siku iliyofuata tulianza kufuatilia vituo mbalimbali vya polisi bila mafanikio, ndipo tuliposhauriana kwenda hospitali mbalimbali, ikiwemo zile zilizoainishwa na mkuu wa mkoa,” alisema.

Shoo alisema Septemba 22 walienda MNH na kuukuta mwili wa kijana wao ukiwa na matundu matatu ya risasi, moja ubavuni na lingine shingoni na walipouliza waliambiwa ulipelekwa pale na polosi wa kituo cha Maturubali Septemba 19.

Kijana mwingine anayedaiwa kuuwa ni Khalfan Jongo (21), ambaye pia inadaiwa alifuatwa na askari nyumbani kwao Sandali, Tandika Septemba 16.

Dada wa marehemu, Sada Jongo alisema baada ya askari kumchukua wao waliamini watamkuta kituo cha polisi Maturubai, lakini walianza kufuatilia kwa siku kadhaa bila mafanikio.

“Kusema kweli ndugu yetu huyu alikuwa si mwizi, ila kama unavyojua vijana wetu hawa, ni watu wa kujichanganya mara starehe wakati mwingine sigara kubwa (bangi),” alisema Sada aliyedai ni dada wa marehemu.


ACT yatoa mapendekezo

Kufuatia matukio hayo, Chama cha ACT Wazalendo kimependekeza mambo manne kwa Serikali ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi askari wanaotuhumiwa kwa mauaji hayo.

Mapendekezo mengine ni Bunge kuunda Tume ya kuchunguza mauaji yote ya raia yanayotekelezwa na Polisi ili kujiridhisha na hatua zilizofanywa na jeshi hilo.

Pia, chama hicho kimependekeza Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kuwajibika kwa kushindwa kuchukua hatua tangu matukio hayo.

Akizungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam jana, msemaji wa kisekta wa Mambo ya Ndani, Mbarala Maharagande alisema “kutokana na tuhuma za mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi taswira yake imeendelea kuchafuka.

Alisema badala ya kuleta matumaini jeshi hilo limeongeza hofu na mashaka,” alisema.

Kwa mujibu wa Maharagande, Septemba 27 walitoa tamko kuitaka Serikali kuchukua hatua za kiuchunguzi na kiuwajibikaji, hata hivyo haikuchukua hatua yoyote.


Kauli ya Makalla

Septemba 15, alipokuwa akizugumza na wananchi wa Kata ya Zingiziwa jijini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alionya kuhusu vitendo vya uhalifu akisema:

“Kuanzia leo naomba mzazi au mlezi ambaye hatamuona kijana wake afike vituo vya polisi na hospitali kubwa za wilaya ikiwemo Amana Mwananyamala, Muhimbili wodi ya Mwaisela na Temeke,” alisema Makalla.