Utata waibuka baada ya lifti kuporomoka Dar

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akizungumza na Msimamizi wa jengo la Millenium Tower, Martin Mhina (kushoto) alipofika katika jengo hilo kuangalia madhara yaliyojitokeza baada ya lifti ya jengo hilo kuanguka na kujeruhi watu 7 waliokuwa wakifanya mkutano katika jengo hilo, jijini hapa jana. Picha na Ericky Boniphace

Dar es Salaam. Utata wa taarifa umeibuka juu ya lifti iliyokuwa na watu saba katika jengo la Millenium Tower, Kijitonyama jijini Dar es Salaam baada ya kudondoka kutoka ghorofa ya 14 na kuwajeruhi waliokuwamo.

Utata huo unatokana na taarifa za matumizi ya lifti ya jengo hilo linalomilikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kutofautiana kati ya uongozi na wapangaji.

Wakati wamiliki wa jengo wakisema lifti hiyo ilikuwa kwenye matengenezo na waliweka utepe wa kuwazuia watu wasiingie, wapangaji walisema utepe huo ulitolewa tangu Jumatatu (Mei 22, 2023) na lifti hiyo kuanza kutumika kwa majaribio.

Mkanganyiko huo ulibuka baada ya lifti hiyo kudondoka jana saa 3:50 asubuhi ikiwa na watu saba waliokuwa wanahudhuria mkutano wa masuala ya afya ambao walikuwa hapo katika mkutano wa siku tatu.

Majeruhi walipelekwa Hospitali ya Kairuki iliyopo jirani na jengo hilo na Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Onesmo Kaganda alisema waliwapokea majeruhi saa nne asubuhi na kati yao wapo waliovunjika viungo vya mwili, huku wengine wakipatwa msongo wa mawazo.

"Unajua kutoka ghorofa ya 14 hadi chini sio jambo dogo, mtu lazima apate msongo wa mawazo, lakini tumewaweka sawa na sasa wanaendelea vizuri huku wakiendelea kupata matibabu,” alisema.

Dk Kaganda alisema jambo la kushukuru katika tukio hilo hakuna hata mmoja aliyepoteza maisha.

Utata ulianza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alipofika kwenye jengo hilo la ghorofa 25, Msimamizi wa jengo hilo, Martin Mhina alisema kulikuwa na utepe mwekundu kuonesha matengenezo yalikuwa yakiendelea.

Chalamila aliyeanzia hospitali ya Kairuki walipopelekwa majeruhi alionekana kutokubaliana na maelezo ya kuwa lifti ilikuwa kwenye matengenezo lakini ilibeba watu.

Kiongozi huyo alilitaka Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi kufanya uchunguzi wa kina zaidi kuhusu hilo.

Pia, aliwataka wamiliki wa majengo marefu kuwa na utaratibu wa kukarabati mara kwa mara lifti zao ili zisilete madhara kwa binadamu na kueleza kuwa hivi karibuni atatoa tamko kuhusiana na majengo yenye lifti.

Mrakibu wa Polisi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kinondoni, Peter Mtui alisema waliodondoka walitoka ghorofa ya 14 na walikuwa saba wote ni wanaume na waliokolewa kisha kupelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi.

Mwananchi liliweka kambi katika jengo hilo kuanzia asubuhi hadi saa moja usiku katika eneo hilo, lilishuhudia watu mbalimbali wakihojiwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

Mahojiano hayo yalikuwa yakifanyika katika chumba kinachotumika kama ofisi ya wamiliki wa jengo.


Matengenezo

Akizungumza na Mwananchi, Mhina alisema katika lifti sita zilizokuwa zikifanya kazi katika jengo hilo mbili tu ndio zilikuwa nzima na zimekuwa katika hali hiyo tangu mwaka jana.

Alisema matengenezo yake yalianza mwanzoni mwa mwezi huu na kati ya hizo, tatu ziliamuliwa na uongozi wa juu zikarabatiwe na mbili zinunuliwe mpya.

"Katika kipindi chote ambacho lifti hiyo ilikuwa kwenye matengenezo tuliweka utepe mwekundu ambao mtu alikuwa akiifungua lifti anaiona na pia tuliwapa taarifa wapangaji wetu wote 49 waliopo humu kuhusu ubovu wa lifti hiyo.

"Lakini hawa wenzetu waliopata ajali leo (jana) ni wageni, hivyo naona hawakulijua hilo wao wakaitumia," alisema Mhina.

Tulipomuuliza sababu ya kuchelewa kutengenezwa kwa lifti hiyo muda wote huo ni nini, alijibu imetokana na taratibu za manunuzi kwa kuwa hiyo ni taasisi ya Serikali, hivyo lazima kila eneo wataalamu wajiridhishe.