Utouh: Hapa kuna ufisadi

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Daniel Sillo (katikati) akizindua ripoti nne za wajibikaji zilizoandaliwa na taasisi ya Wajibu jijini Dodoma jana. Wengine katika picha ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wajibu, CAG mstaafu Ludovick Utouh ( kushoto), Ofisa Ufuatiliaji wa Wajibu, Teckla Mleleu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya wajibu, Yona Killagane. Na Mpigapicha wetu

Muktasari:

  • Wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizunguka katika maeneo mbalimbali nchini na kuanza kuwachukulia hatua baadhi ya watendaji waliotajwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2020/21, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Wajibu, Ludovic Utouh amesema zabuni ya upanuzi wa kina cha Bandari ya Tanga na uteketezaji wa noti chakavu uliofanywa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni ufisadi unaopaswa kushughulikiwa haraka.


Dodoma. Wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizunguka katika maeneo mbalimbali nchini na kuanza kuwachukulia hatua baadhi ya watendaji waliotajwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2020/21, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Wajibu, Ludovic Utouh amesema zabuni ya upanuzi wa kina cha Bandari ya Tanga na uteketezaji wa noti chakavu uliofanywa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ni ufisadi unaopaswa kushughulikiwa haraka.

Licha ya harufu ya rushwa kwenye maeneo hayo mawili, uchambuzi wa ripoti ya CAG uliofanywa na Wajibu umebaini kutoingizwa kwa Sh1.2 trilioni kwenye mfuko wa Hazina, jambo alilosema linahitaji umakini wa Serikali katika kusimamia fedha za umma.

Utouh alitoa kauli hiyo jana, kwenye uzinduzi wa ripoti nne za uwajibikaji zilizozinduliwa na taasisi ya Wajibu mbele ya Kamati za Kudumu za Bunge, asasi za kiraia, watendaji pamoja na waandishi wa habari jijini hapa.

“Zabuni ya Bandari ya Tanga na uteketezaji wa fedha BoT ni ufisadi wa hali ya juu unaopaswa kushughulikiwa na Serikali kwa kuwachukulia hatua wahusika wote walioshiriki. Hivi ni vitu vinavyoumiza uchumi ambavyo mwisho wa siku vinawaumiza wananchi,” alisema Utouh.


Ripoti ya CAG iharakishwe

Wadau walioshiriki uzinduzi wa ripoti nne za Wajibu ulioongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Daniel Sillo wamependekeza kupunguzwa kwa muda wa uandaaji wa ripoti ya CAG ili kulipa Bunge na wadau wengine kuichambua kwa wakati.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Japhet Hasunga alisema kwa utaratibu uliopo sasa, ripoti hiyo hujadiliwa zaidi ya mwaka mmoja tangu udhaifu uliobainishwa na CAG uonyeshwe hivyo kutokuwa na nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko.

“Hesabu za fedha zinafungwa Juni na taarifa inatakiwa kutolewa mpaka Septemba 30. Baada ya hapo CAG anapewa ili aandae ripoti yake kwa miezi sita na kuiwasilisha Machi 31. Bunge huanza kuijadili Agosti. Kwa maendeleo ya teknolojia yaliyopo, hesabu zinaweza kufungwa ndani ya mwezi mmoja. CAG naye akipunguziwa muda wa kukamilisha ripoti yake wadau watapata muda wa kutosha kujadili mapendekezo yaliyotolewa,” alishauri Hasunga.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wajibu, Yona Killagane alisema ni jambo linalowezekana kupunguza muda wa kufunga hesabu za Serikali na CAG kuandaa ripoti, ingawa utaratibu huo umewekwa kwenye Katiba na sheria ya hesabu za Serikali.

“Wakati Katiba inatungwa mwaka 1977 hakukuwa na teknolojia iliyopo sasa. Tusichelewe kwa kuogopa kufanya mabadiliko yatakayokuwa na tija,” alisema Killagane akitaka Katiba na sheria zirekebishwe kuruhusu mabadiliko hayo.

Kwenye ukaguzi wake, CAG Charles Kichere amebaini harufu ya rushwa katika upanuzi wa kina cha Bandari ya Tanga ambako mzabuni aliyeshinda alilipwa zaidi ya Sh104 bilioni, lakini naye akamtafuta mkandarasi wa kuitekeleza kazi hiyo kwa Sh40 bilioni, hivyo kujipatia Sh64 bilioni bila kufanya kazi yoyote.

Ripoti hiyo iliyotokana na ukaguzi maalumu uliofanywa kwa kipindi cha kuanzia Januari 2017 mpaka Desemba 2019 inabainisha kuwa BoT ilipata hasara ya Sh3.99 bilioni kutokana na ubadilishaji wa noti chakavu zisizostahili kuendelea kutumika.

Kati ya Januari na Septemba 2019, CAG amesema alibaini BoT ilipokea noti 417,006 za Sh10,000 zenye thamani ya Sh4.17 bilioni zikidaiwa kuwa chakavu ili zibadilishwe.

Pia, uchunguzi wake ulionyesha noti 1,427 zenye thamani ya Sh14.27 milioni zilikuwa safi zinazofaa kuendelea kutumika na noti 16,187 zenye thamani ya Sh161.87 milioni zilikidhi vigezo vya kubadilishwa wakati noti 399,392 zenye thamani ya Sh3.99 bilioni hazikuwa na vigezo ila zilipewa noti mpya kwa njia ya udanganyifu uliofanywa na maofisa wawili na watunza fedha wanne wa BoT.

“Niligundua wahusika walikata vipande vya noti 399,392 za Sh10,000 na kuvibandika kwenye karatasi nyeupe kisha kudai noti mpya. Vipande hivyo 399,392 vilikatwa kutoka kwenye noti 199,696 zilizokuwa safi,” amesema CAG kwenye ripoti yake.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Emmanuel Tutuba alipoulizwa kuhusu kupunguza muda wa kukabidhi ripoti ya ukaguzi, alisema siku 90 za kukabidhi ni kwa ajili ya kukamilisha majukumu ya ukaguzi na kwamba, hata muda ukipunguzwa hana uhakika kama watakamilisha.

Kuhusu madai ya ufisadi kwenye mradi wa Bandari ya Tanga, alisema kila taasisi ya umma ina ofisa masuhuli ambaye anawajibika kama kuna uzembe ama hasara kwenye eneo lake.

“Mimi ni mlipaji mkuu wa Serikali, nikishalipa, kuna maofisa walnaowajibika kusimamia matumizi ya fedha za umma, kunapotokea uzembe au rushwa inayosababisha hasara kwa Serikali basi kuna ofisa masuhuli anayewajibika. Kama CAG ameona kuna rushwa basi kuna Takukuru na taasisi nyingine zinazoshughulika na masuala hayo, siyo mimi tena,” alisema.

Kuhusu mapato ya Sh1.2 trilioni kutoingizwa Hazina, alisema: “Kwa sasa siwezi kujibu kwa sababu sina hiyo taarifa, utaratibu ni kuwa kila fedha lazima iingie kwenye mfumo wa Serikali. Sasa hapo sijui, inawezekana amekosea.”