Uzembe wa madereva watajwa ajali iliyoua 20, kujeruhi 15

Muktasari:

  • Ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia leo Jumanne, imesababisha vifo vya watu 20 na 15 wakijeruhiwa, wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga.

Kahama. Wakati majeruhi watatu kati ya 15 wa ajali iliyotokea Kahama Mkoa wa Shinyanga na kusababisha vifo vya watu 20 wakitarajiwa kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga au Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza, uzembe wa madereva umetajwa kuwa chanzo cha ajali hiyo.

Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Dk Deogratius Nyaga amesema uamuzi wa kuwapa rufaa majeruhi watatu unatokana na hali zao kuhitaji huduma za kibingwa zisizopatikana katika hospitali hiyo ya wilaya.

“Tumepokea maiti ya watu 20 na majeruhi 15 ambao watatu kati yao hali zao siyo nzuri; tunawapa huduma na matibabu ya awali ikiwemo vipimo kufahamu ukubwa wa matatizo yao ili kuyadhibiti kabla ya kuwahamishia Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga au Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza,” amesema Dk Nyaga

Akizungumzia ajali hiyo iliyotokea eneo la Mwakata Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama ikihusisha magari matatu, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga (RPC), Leonard Nyandahu ametaja uzembe wa maderava wote watu kuwa chanzo cha ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia leo Jumanne Agosti 9, 2022.

“Madereva wote walifanya uzembe wa kutochukua tahadhari; dereva wa trekta iliyokuwa imeegeshwa pembezoni mwa barabara hakuweka alama za kiashiria chochote kuonyesha kuna gari imeegeshwa, hali iliyosababisha gari ndogo aina ya IST kuligonga kwa nyuma na kusababisha majeruhi,” amesema Kaimu Kamanda Nyandahu

Akifafanua, Kaimu kamanda huyo amesema baada ya ajali ya kwanza iliyohusisha IST na trekta, magari mengine mawili aina ya Toyota Hiace iliyokuwa inatoka mjini Kahama kwenda eneo la Tinde iligongana uso kwa uso na Lori aina ya Fuso wakati dereva wa Hiece alipojaribu kukwepa IST na trekta zilizohusika kwenye ajali ya kwanza.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa hata madereva wa Toyota Hiece na Fuso nao hawakuchukua tahadhari wakati wanapita eneo la ajali ya awali ndio maana waligongana uso kwa uso,” amesema Kaimu Kamanda Nyandahu

Kigogo huyo wa Polisi mkoani Shinyanga amewataka madereva wote kuendesha kwa kuwajibika, tahadhari na utii wa sheria na kuangalia alama za usalama barabarani kuepusha ajili zisinazozuilika kuokoa maisha ya watu wasio na hatia.

Mabula Chande, mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo ameunga mkono kauli ya Jeshi la Polisi kuwa uzembe wa madereva ndio chanzo cha ajali.

“Pamoja na kukosa umakini, madereva wa Hiece na lori pia walikuwa wakiendesha kwa mwendo kasi ndio maana walishindwa kufunga breki walipofika kwenye eneo la ajali ya IST na treka. Wangekuwa kwenye mwendo wa kawaida wangefunga breki na kusimama,” amesema Chande

Kauli kama hiyo pia imetolewa na John Maduhu akisema; “Kwa idadi ya vifo na majeruhi katika ajali hii, hasa ile iliyohusisha Toyota Hiece na lori ni dhahiri magari yote mawili yalikuwa kwenye mwendo kasi na hivyo madereva kushindwa kufunga breki,”

Maduhu amewaomba madereva wanapopita eneo lilikotokea ajali kuchukua tahadhari siyo tu ya ajali zinazohusisha magari, bali pia mikokoteni inayokokotwa kwa punda, hasa nyakati za usiku kwa sababu nyingi hazina alama wala viakisi mwanga.