Uzoefu turufu ya uspika

Aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai

Muktasari:

  • Wakati CCM ikiendelea na mchakato wa kusaka mgombea wa nafasi ya Spika wa Bunge, vigogo sita kati ya 70 walioomba nafasi hiyo ndio wanaoonekana kuwa na mchuano mkali.


Dodoma. Wakati CCM ikiendelea na mchakato wa kusaka mgombea wa nafasi ya Spika wa Bunge, vigogo sita kati ya 70 walioomba nafasi hiyo ndio wanaoonekana kuwa na mchuano mkali.

Vita hiyo inaonekana pia itakuwa kati ya wabunge na walio nje ya Bunge, lakini walipata kuhudumu kwenye nyadhifa mbalimbali serikalini na bungeni.

Uwepo wa vigogo hao unakifanya chama hicho ambacho leo na kesho kitakuwa na kikao cha Kamati Kuu chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan kukuna kichwa cha kupitisha jina moja hadi matatu.

Hatua itakayofuata jina moja au matatu yatapelekwa kwa wabunge wa chama hicho kuwapigia kura ambao watapiga kura kupitisha jina moja litakalokwenda bungeni kupigiwa kura.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, vigogo hao sita ni Naibu Spika, Dk Tulia Akson, aliyekuwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, aliyekuwa mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele, mbunge wa Ilala Azan ‘Zungu’ na Mhandisi Stela Manyanya.

Uzoefu katika kuongoza mhimili huo kwa nyakati tofauti inatajwa sifa mojawapo itakayombeba mmoja kati ya vigogo hao kukalia kiti cha Spika.

Licha ya jukumu kubwa la kusimamia uendeshaji wa Bunge kwa kufuata Katiba, lakini CCM watampa nafasi mgombea ambaye watataka asimamie masilahi ya chama hicho hasa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa kuwa pia atakuwa mjumbe wa Kamati Kuu.


Chenge

Andrew Chenge huyu alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia mwaka 1993 hadi mwaka 2005 baada ya hapo aliwania ubunge na aliporejea bungeni alishika nyadhifa mbalimbali ikiwemo uenyekiti wa Bunge, Kamati ya Bajeti na Sheria ndogo.

Chenge ni miongoni mwa makada wa CCM waliopewa jukumu la kuboresha rasimu ya Katiba wakati wa Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014 ambayo iliwasilishwa kwenye bunge hilo na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Licha ya uzoefu wake katika kuendesha Bunge akiwa Mwenyekiti wa Bunge unatajwa unaweza kumbeba kwenye kinyang’anyiro hicho, tuhuma za ufisadi zilizomuandama zinaweza kutia doa safari yake.


Dk Tulia Akson

Huyu ni Naibu Spika aliyepata nafasi hiyo mwaka 2015 baada ya Rais John Magufuli kumteua kuwa mbunge na baadaye aliwania nafasi ya uspika, lakini baadaye aliwania Unaibu Spika akimpisha kwenye nafasi ya Uspika Ndugai.

Uzoefu wa miaka sita kwenye uongozi wa Bunge na katika sheria zinamfanya apewe nafasi ya kupenya, ingawa baadhi ya wadau wanaona amewania nafasi hiyo kutia chachu kinyanganyiro hicho.

Kama atapata fursa hiyo, Bunge litalazimika kufanya uchaguzi mwingine kuziba nafasi ya Naibu Spika.


Manyanya

Mwanasiasa huyu tangu aingie bungeni mwaka 2010 ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini na kwenye chama hicho anatajwa kufanya siasa zisizo za kashkash, jambo linalotajwa linaweza kumsaidia kupata nafasi hiyo.


Zungu

Mwaka 2005 aliingia bungeni na kupata nafasi mbalimbali bungeni na serikalini ikiwemo kuwa Mwenyekiti wa Bunge, Waziri na Mwenyekiti wa Kamati mbalimbali.


Kashililah

Aliyekuwa Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililah naye anapewa nafasi kubwa kwenye kinyang’anyiro hicho kutokana na uzoefu wake kwenye Bunge akifanya kazi na maspika watatu (Samuel Sitta, Anne Makinda na Job Ndugai).

Katika kipindi chake Bunge lilifanya mabadiliko mbalimbali ya kimfumo yaliyoboresha masilahi ya wabunge na kuufanya muhimili huo ufuatiliwe zaidi na wananchi.

Anatajwa kuwa ni mtu anayeweza kuhimili mikimiki ya kisiasa na hana makundi hasa wakati huu ambao chama kinaelekea kufanya uchaguzi wa ndani.


Masele

Stephen Masele, alikuwa mbunge wa Shinyanga Mjini kati ya mwaka 2010 na 2020, alichaguliwa na Bunge kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika (PAP) lenye makao makuu yake Afrika Kusini.

Mei 10, 2018, alichaguliwa na wabunge wa PAP kuwa Makamu wa Rais, nafasi iliyomwezesha kuongoza vikao vya Bunge hilo hadi mwishoni mwa mwaka 2020 baada ya kutoteuliwa kugombea ubunge katika jimbo lake.


Maoni ya wadau

Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bakari Mohamed alisema pamoja na vigezo vingine, anayetafutwa ni mtu atakayekuwa mtiifu wa Serikali.

“Mtu hasa wanayemtaka, ni yule anayependelewa na Serikali kwa wakati huu. Yule ambaye Serikali wanahisi wanaweza kufanya naye kazi, nadhani ndiye mtu ambaye jina lake litafika mbali zaidi.

“Sioni kuna vita kubwa kiasi cha kusema wabunge watatofautiana na Serikali, kama tunavyojua wabunge wetu huwa hawana misimamo, bali wanakwenda kutokana na utashi wa Serikali,” alisema Profesa Bakari.

Alitaja pia kigezo cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 akisema watatafuta mtu atakayejenga kundi litakalolinda masilahi ya utawala uliopo madarakani.

“Unapomchagua mtu anayeweza kuunganisha watu kwa ajili ya uchaguzi, ni miongoni mwa mambo watakayoangalia.

Alitoa mfano wa Chenge akisema ni mwanasiasa anayeweza kuunganisha watu wa eneo husika kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

“Kwa hiyo wanaweza kusema tukimchagua huyu tutarahisisha harakati za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025,” alisema.

Kwa upande wake, Profesa wa Sayansi ya Siasa, Bernadetta Killian alisema watakachozingatia ni mtu atakayejali masilahi ya chama.

“Tuwaache wao wafanye mchujo, lakini spika watakamchukua ni yule atakayesimamia masilahi ya chama chao. Wananchi tungependa kupata spika atakayesimamia masilahi ya nchi,” alisema.