VIDEO: Anayedaiwa kumzushia kifo Dk Mwakyembe akamatwa

Anayedaiwa kumzushia kifo Dk Mwakyembe akamatwa

Muktasari:

Mbali na mtu huyo, Jeshi la Polisi limemkamata mtu mwingine anayedaiwa kutumia jina la Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Dk Hassan Abbas kutapeli watu.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, linawashikilia watuhumiwa wawili kwa makosa ya kimtandao kufuatia msako unaoendelea.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Septemba 26, 2022 na Kamanda wa Kanda Maalum, Jumanne Muliro imeeleza kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa, kwa kushirikiana na Kikosi Kazi Maalum cha Kupambana naMakosa ya Mtandao.

Amemtaja mtuhumiwa Tazarn Mwambengo (27), mkazi wa Ukonga anayetuhumiwa kusambaza taarifa za uongo kuhusu kifo cha Dk Harrison Mwakyembe kupitia chaneli ya televisheni ya mtandaoni, jambo ambalo si la kweli.

Muliro amesema katika chanel hiyo mtuhumiwa aliandika “Breaking News huzuni yatanda mazishi ya Mwakyembe” ambapo taarifa hizo ziliibua taharuki kubwa kwa wananchi hasa kwa Dk Mwakyembe mwenyewe na familia yake.

“Watuhumiwa hawa wamekutwa wakiwa na vifaa mbalimbali wanavyotumia kufanya uhalifu ikiwemo kompyuta mpakato 1, simu 3, mike ya kutangazia 1, modem 1, na kadi za mitandao mbalimbali 9 zenye usajili wa majina tofauti,” imesema taarifa hiyo.

Mtuhumiwa wengine ni pamoja na Innocent Chengula (23), mkazi wa Kigogo Luanga ambaye amekamatwa kwa tuhuma za kujinasabisha kuwa yeye ni Dk Hassan Abbas Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo.

 “Mtuhumiwa huyu amekuwa akijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia mtandao na kutumia laini za simu zenye usajili usio na majina yake.

“Mtuhumiwa huyu amekuwa akiweka picha na majina ya Dk Hassan Abbas katika maelezo ya ukurasa wake kwenye mitandaoni ya kijamii (Profile) na kutuma jumbe kwa watu akiwaomba wamtumie fedha kwenye namba tofauti za simu,” amesema Muliro.

Kamanda Muliro amesema miongoni mwa jumbe alizotuma zinazosomeka “kaka naomba niazime Sh3 milioni Alhamis nitakurudishia.” Mwingine umesomeka, “kaka nina mtoto wangu naomba umpatie kazi hapo kwako yeye amesomea bachelor of commerce in accounting”.

Aidha, Jeshi hilo limetoa rai kwa Watanzania kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii, pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari na sheria zinazohusika kuepuka kuchapisha taarifa zitakazo zua taharuki kwa umma.