VIDEO: Biashara ya uume wa ng’ombe yamtajirisha kijana Vingunguti

What you need to know:

  • Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni! Msemo huu unajidhihirisha baada ya kauli ya Onesmo Mbasha, ambaye ni mmoja wa vijana wanaouza bidhaa mbalimbali zitokanazo na wanyama zikiwamo sehemu za uzazi za ng’ombe dume zinazojumuisha uume na korodani.

Dar es Salaam. Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni! Msemo huu unajidhihirisha baada ya kauli ya Onesmo Mbasha, ambaye ni mmoja wa vijana wanaouza bidhaa mbalimbali zitokanazo na wanyama zikiwamo sehemu za uzazi za ng’ombe dume zinazojumuisha uume na korodani.

Zipo taarifa kuwa viungo hivyo vya ng’ombe ni maalumu kwa ajili ya kutengenezea nyuzi zinazotumika kuwashonea watu waliopata ajali na chakula kinachotumika zaidi nchini China.

Daktari wa mifugo kutoka The Old Farm House, Wilfred Hongoli anasema uume wa ng’ombe unaweza kutumika kutengenezea nyuzi za kushonea binadamu au mnyama pale anapopata majeraha au kufanyiwa upasuaji.

“Nyuzi zinazotengenezwa na bidhaa hiyo huwa na tabia ya kubaki mwilini hata baada ya jeraha kupona, tofauti na nyingine ambazo lazima zitolewe baada ya jeraha kupona,” alisema.

Hata hivyo, Onesmo anasema kabla ya kuanza biashara hiyo alikuwa na biashara ya nguo alizokuwa akizitoa Mombasa nchini Kenya na kuziuza katika Soko la Kariakoo.

Mbasha anasema alianza biashara ya uume na korodani za ng’ombe miaka sita iliyopita baada ya daktari wa mifugo katika machinjio hayo, Dk Mgeta (ambaye jina la kwanza halikupatikana mara moja), kumueleza fursa ya kibiashara iliyopo ya viungo hivyo vya ng’ombe.

“Alinipa mchongo huu kwa kuwa nilikuwa nachinja ng’ombe wengi na kwa mara ya kwanza niliuza kwa Wachina na kupata Sh35 milioni,” alisema.

Anasema uume mmoja anauunua machinjioni kwa Sh1,000 na hukausha kisha huuza kwa kilo hapa nchini na nje ya nchi.

Anasema kwa hapa nchini huwauzia Wachina wanaofanya biashara za hoteli na migahawa ambao huvitumia kwa ajili ya kitoweo.

Hata hivyo, anasema suala la bei kwa hapa nchini huwa ni maelewano kati yake na mnunuzi ambao huvinunua viungo hivyo kabla hajavikausha.


Matumizi

Onesmo anasema licha ya kutokwenda nchini China kuona viwanda vinavyotumia bidhaa anazowauzia, lakini wateja wake humuambia kuwa hutumia viungo hivyo kwa chakula na kutengeneza nyuzi. “Zikikaushwa huuzwa nje ya nchi ambapo hutumika kutengeneza nyuzi zinazotumiwa na madaktari kushona watu wanaofanyiwa upasuaji,” anasema kijana huyo.

Lakini pia, amesema bidhaa hiyo huuzwa kwa gharama kubwa kwa kuwa ni kitoweo katika hoteli zinazouza vyakula vya Kichina ndani na nje ya Tanzania,” anasema.

Onesmo anasema biashara hiyo pia huifanya hapa nchini kwa watu wanaojishughulisha na tiba asili.

Anasema wataalamu hao wa tiba asili humuambia wanazitumia kutengenezea dawa zinazoaminika kuongeza nguvu za kiume.

“Ukiachilia mbali kuwauzia watu wa tiba asili, uume wa ng’ombe hutumika kutengenezea supu ambayo pia huaminika kuwa husaidia kuongeza nguvu za kiume,” anasema.

Anasema baadhi ya wanaume hununua bidhaa hiyo wakiihusisha na imani za kishirikina kwa ajili ya kupata dawa za kutatulia mambo mbalimbali.

Kuhusu korodani, Mbasha anasema bidhaa hiyo hununuliwa kwa kiasi kikubwa na Wachina huzisafirisha nje ya nchi.

“Wachina hununua kwa wingi bidhaa hii kiasi kwamba kuna kipindi inakuwa ni adimu na haipatikani sokoni,” anasema.

Mbali na kuuza nje ya nchi, korodani pia huuzwa nchini, watu huchoma na kula wakiamini zinasaidia kuongeza nguvu za kiume na dawa ya watu wanaosumbuliwa na magoti.

“Ashua za ng’ombe huziuza 3 kwa Sh1,000 na za mbuzi hupatikana 4 kwa Sh1,000,” anasema.

Kijana huyo anasema kutokana na biashara hiyo, ameingia mkataba na wanunuzi wakubwa wa kati ambao humpa fedha nyingi zinazomsaidia kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo, kuhudumia familia na kufanya uwekezaji.

“Hivi sasa ninamiliki nyumba kadhaa ndani ya jiji la Dar es Salaam, mabucha, magari na pia imeniwezesha kuwasomesha watoto wangu katika shule za kulipia.

“Nimetoa ajira kwa vijana wa Tanzania takribani 100 ambao wanaendesha maisha yao kupitia kazi hiyo,” anasema.

Anasema biashara hiyo imemwwezesha apate umaarufu ndani na nje ya nchi na hivyo kukuza zaidi biashara yake.

“Hii inatokana na kuwa mimi ni mmoja wa watu wanaonunua bidhaa hiyo katika machinjio mbalimbali nchini kwa kiwango kikubwa na kuuza nje ya nchi na kuniwezesha kupata mikataba minono,” anasema.

Suala la ajira

Mbasha anatoa wito kwa vijana wanaohangaika kutafuta ajira wasichague kazi au fursa inayojitokeza mbele yao, pia wajitoe na kujituma zaidi kwa kile wanachokifanya.

“Nawashauri vijana, hasa waliomaliza elimu zao wakiwa wanasubiri ajira wawe wabunifu na kuanzisha biashara ambazo hazihitaji mtaji mkubwa, kuna zinazohitaji mtaji wa Sh5,000,” anasema.

Fursa za biashara

Akizungumza namna wafanyabiashara hao wanavyotumia fursa ya vitu vya mifugo baada ya kuchinjwa, kiongozi wa wafanyabiashara wa machinjio ya Vingunguti, Joel Meshack anasema zipo taarifa kuwa uume na korodani za ng’ombe zinachukuliwa na Wachina kwa ajili ya kutengenezea nyuzi za kushonea binadamu kipindi cha upasuaji.

“Kwenye ng’ombe viungo vingi vina faida, lakini Waafrika hatuna utaalamu wa kutosha, hivyo kazi yetu ni kuzalisha malighafi zinazotokana na ng’ombe lakini matumizi wanayajua wahusika,” anasisitiza.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.