VIDEO-Chongolo asikitishwa wananchi kukosa dawa Kilimanjaro

Chongolo asikitishwa wananchi kukosa dawa Kilimanjaro

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameonyeshwa kusikitishwa na kitendo cha wananchi kukosa huduma ya dawa katika Zahanati zilizopo Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro kwa sababu ya deni wanalodaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) la Sh104 milioni.

Mwanga. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameonyeshwa kusikitishwa na kitendo cha wananchi kukosa huduma ya dawa katika Zahanati zilizopo Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro kwa sababu ya deni wanalodaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) la Sh104 milioni.

 Leo Jumamosi Agusti 6, 2022, Chongolo akiwa Kijiji cha Vuchama, Diwani wa Mwaniko, Baraka Maradona, alimweleza changamoto zinazowakabili wananchi, ikiwemo kukosekana kwa dawa katika zahanati zao.

Diwani huyo aliomba deni hilo lifutwe na dawa zipelekwe ili kusaidia wananchi wanapohitaji matibabu.

"Tuna zahanati zetu kwenye wilaya hii ya Mwanga, hizi Zahanati zilikuwa na madeni Sh104 milioni, madeni haya hayakulipwa MSD, wananchi wakienda zahanati hawapati huduma, ikikupendeza deni hilo lifutwe ili wananchi waendelee kupata huduma," amesema Maradona.

Akijibu malalamiko hayo, Chongolo alisema anakwenda kukaa na wataalamu ili kupata taarifa ya deni ambalo linadaiwa ili kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.

"Ndugu zangu mmesema kwenye zahanati kuna changamoto ya deni la dawa, mimi najua pamoja na kwamba mtakuwa mnajua mna deni la dawa lakini kuna fedha hutolewa kwa ajili ya dawa kwenda kila zahanati na fedha hizo hutolewa na Serikali kwenda MSD kwa ajili ya kuleta dawa huku chini," amesema

"Ninakwenda kukaa na wataalamu, waniambie zahanati zote zilizopo hapa zinadaiwa shilingi ngapi, tumeahidi kuhudumia na kulinda afya za wananchi na dawa ni sehemu muhimu katika huduma za afya," amesema

Chongolo amesema, “hatuwezi kuwa tunapiga hadithi kwenye afya za watu, hapa mwananchi mmoja akipotea kwa nchi ni hasara kubwa, hatuwezi kuruhusu mwananchi mmoja apotee eti kwa sababu amekosa dawa ya kumtibu na ugonjwa unatibika."

"Kwa kweli nimesikitishwa kusikia dawa haziji eti kwa sababu kuna deni, hiyo haikubaliki na hiyo siyo sawa, ni lazima tujue kama kuna changamoto tutafute njia ya kuitatua lakini tusitishe huduma kwa wananchi," amesisitiza

Amesema hapa diwani, mwananchi ana bima kubwa anaenda hospitali anakuta hakuna dawa eti kwa sababu kuna deni, hilo halikubaliki, lazima tuende tukaketi ili kupata ufumbuzi na wsnanchi waondokane na changamoto hii".

Aidha alisema wanatambua MSD kulikuwa na changamoto ambazo zimeendelea kutatuliwa na Wizara inajipanga kuboresha mifumo lakini wao kama chama wanachohitaji ni dawa kupatikana kwa wananchi na huduma kuboreshwa.

"Tunataka dawa huku chini na hiyo ndiyo kazi ambayo nimetumwa na mwenyekiti , kuja kujiridhisha na huduma wanazopewa wananchi, na pale kwenye changamoto lazima tuseme ukweli, hatuwezi kuwa chama tunachoisimamia serikali halafu tunapiga makofi hata mahali ambako hakuna tija."

"Tutakuwa wa ajabu maana kesho tutakuja kuulizwa tulipewa dhamana mbona hakuna dawa, mbona hakuna kituo cha afya, mbona hakuna barabara, mbona hamkufanya hiki au kile, hatuko tayari kuulizwa maswali, niwahakikishie tunakwenda kubanana huko, kujua changamato ya hayo madeni kwenye zahanati na tujue yako kwa kiwango gani".

"Tujue sababu za hayo madeni na tutafute suluhisho kwa kuhakikisha madeni yanafutwa ili tuanze upya kuwa na uhakika wa dawa kwenye zahanati zetu," amesema