VIDEO: Dk Kijaji ataja sababu kupanda sabuni za kufulia

Dk Kijaji ataja sababu kupanda sabuni za kufulia

Muktasari:

Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda nchini Tanzania, Dk Ashatu Kijaji amesema bei ya sabuni za kufulia za mche zimeongezeka kutokana na kupanda kwa bei ya malighafi zinazoazoagizwa kutoka nchi za Indonesia na Malaysia.

Dodoma. Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda nchini Tanzania, Dk Ashatu Kijaji amesema bei ya sabuni za kufulia za mche zimeongezeka kutokana na kupanda kwa bei ya malighafi zinazoazoagizwa kutoka nchi za Indonesia na Malaysia.

 Dk Kijaji ameyasema hayo leo Jumatatu Agosti 15, 2022 wakati akitangaza tathmini ya mwenendo wa bei ya bidhaa muhimu nchini.

“Bei zimepanda kutoka wastani wa Dola za Marekani 500 hadi 600 kwa tani hadi Dola za Marekani 1,800 kwa tani hasa baada ya Indonesia kuweka zuio la kusafirisha nje malighafi hizo,”amesema.

Amesema kutokana na ongezeko hilo la bei ya malighafi,bei ya mche wa sabuni ni kati ya 3,000 hadi 4,500.

Amesema sabuni ya kufulia ya unga inauzwa kwa kati ya Sh1, 000 hadi Sh4,500 kwa kilo huku Omo ikipatikana kwa kati ya Sh8,000 na Sh8,200.

Bidhaa nyingine zilizoongezeka bei katika kipindi cha Julai na Agosti mwaka huu ni mchele, viazi mviringo, maharage na sukari vimepanda bei.

Dk Kijaji amesema katika bidhaa za ulezi, ngano, uwele mahindi na unga wa mahindi pamoja na vifaa vya ujenzi hakuna mabadiliko ya bei katika kipindi hicho cha miezi miwili.

Hata hivyo, Dk Kijaji amesema vyakula viko vya kutosha nchini na hivyo wakulima waendelee kuuza huku wakizingatia akiba yao.

“Napenda kusisitiza kauli ya Waziri wa Kilimo (Hussein Bashe) hatutafunga mipaka kwa wananchi wetu kuuza mazao nje ya nchi, kwasababu bado tuna chakula cha kutosha ndani kinachohitajika ni wakulima wetu kufikia bei ya mazao nzuri, huku wajihakikishia kuwa wanabakiza chakula cha kutosha ndani,”amesema.

Dk Kijaji amesema wakati huo Serikali ikiendelea kufuatilialia kuhakikisha kuna chakula cha kutosha sokoni na kuwaondoa hofu wananchi kuwa chakula kipo cha kutosha nchini.