VIDEO: Mkutano wa CUF utata mtupu, polisi wauzuia, waruhusu

Muktasari:

Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Profesa Ibrahim Lipumba leo kinafanya mkutano mkuu jijini Dar es Salaam ambapo licha ya polisi kuuzuia lakini unaendelea

Dar es Salaam. Licha ya Polisi mkoa wa Ilala kutoa taarifa ya kuzuia mkutano mkuu wa CUF upande mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, jeshi hilo limeshindwa kuzuia mkutano huo.

Polisi walifika na magari manne likiwamo lenye maji ya kuwasha katika eneo la mkutano Buguruni jijini Dar es Salaam lakini walishindwa kusitisha mkutano huo kufuatia simu iliyopigwa na Profesa Lipumba ambayo hata hivyo alikataa kusema alimpigia nani.

Baada simu hiyo iliyopigwa mbele ya RPC wa Ilala, Zubery Chembera, magari ya polisi yaliondoka eneo la mkutano.

Profesa Lipumba alitoka nje ya ukumbi na kuzungumza na RPC Chembera, baada ya kuahirisha mkutano huo mchana na kupangwa kuendelea tena saa 9:00 alasiri.

Alipoulizwa kuhusu simu aliyokuwa akipiga Profesa Lipumba amesema: "Niliongea na jamaa ninaowafahamu. Mimi ni mtu mzito siwezi kukwambia nimeongea na nani. Wewe unapopiga simu nakuuliza yakhe uliongea na nani?"

Amesema mkutano huo ni halali kwa kuwa una kibali cha msajili wa vyama vya siasa.

"Wenzetu wanachama upande wa Maalim (Seif Sharif Hamad) walipeleka taarifa potofu polisi, sasa ndiyo walikuja kuuliza nini kimetokea,” amesema.

Kuhusu madai ya kuwapo zuio la Mahakama, amesema waliozuiwa majina yapo lakini baraza kuu lina mamlaka ya kuitisha mkutano.

Naibu msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza amesema amehudhuriamkutano huo kwa sababu ni halali kikatiba.

"Mimi nahudhuria mkutano huu kumwakilisha msajili wa vyama vya siasa. Kwa mujibu wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa yaliyofanyika Januari mwaka huu, tunawajibika kuhudhuria mikutano hii hata tusipoalikwa," amesema.

Kuhusu zuio la Mahakama amesema, "Sisi tumehudhuria huu mkutano hatujaona zuio la Mahakama wala halijaletwa ofisini kwetu. Tunachojua viongozi wa CUF wako hapa na wanatambuliwa na ofisi ya msajili na hatujaona hilo zuio linalodaiwa kuwapo."

 

Jinsi Polisi walivyoondoka

Awali, saa 4:00 asubuhi, kamanda wa polisi wa Ilala (RPC), Zubery Chembera alifika katika hotel ya Lekam unakofanyika mkutano huo na kuwataarifu viongozi wa chama hicho kuwapo kwa hukumu ya Mahakama inayozuia mkutano huo, lakini walikataa kusitisha mkutano.

Baada ya saa 2 kupitia wakati mkutano huo ukiendelea, askari waliokuwa katika magari manne likiwAmo la maji ya kuwasha wakiongozwa na OCD wa Buguruni, Adam Maro walifika eneo hilo na kuamuru mkutano huo uvunjwe, hali iliyoleta malumbano makali.

OCD Maro aliwaambia viongozi kuwa anataka kuonana na Profesa Lipumba lakini walikataa.

Viongozi hao wakiongozwa na Mkurugenzi wa uhusiano wa CUF, Abdul Kambaya walisema wako tayari kufia hapo kuliko kusitisha mkutano huo.

Baada ya muda mrefu wa malumbano, OCD Maro alilazimisha kuingia kwenye mkutano lakini walinzi na makada wa CUF walimzuia kwa nguvu.

Baada ya kuondolewa mlangoni, ndipo Profesa Lipumba alitoka kuzungumza na RPC na baadaye kupiga simu iliyozima malumbano na hatimaye polisi kuondoka na magari yao.