VIDEO: Mnyukano wa wabunge CCM

Mnyukano wa wabunge CCM

Muktasari:

  • Ni Bunge ambalo halina Kambi Rasmi ya upinzani, lakini limeanza kuwa moto kutokana na minyukano ya wabunge wa CCM.

Dodoma. Ni Bunge ambalo halina Kambi Rasmi ya upinzani, lakini limeanza kuwa moto kutokana na minyukano ya wabunge wa CCM.

Juzi na jana kwenye mjadala wa hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, wabunge wa CCM walianza kurushiana maneno kutokana na maoni yao ya ama kusifu au kukosoa mambo yaliyofanyika wakati wa Serikali ya awamu ya tano.

Katika mjadala huo na ule wa mpango wa Serikali wamejitokeza wanaotumia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo imebainisha madudu mengi yaliyofanyika katika mwaka 2019/2020, huku wengine wakiibeza.

Aina ya michango inayowainua wengine kujadili ni wa Mrisho Gambo, mbunge wa Arusha Mjini (CCM), aliyeeleza kushangaa ahadi ya kuzalisha ajira milioni nane, akisema tangu nchi ipate uhuru ajira kwa watumishi wa umma hazijawahi kuzidi 600,000 na akahoji hizo milioni nane zitapatikana vipi.

“Sasa unajiuliza kama tangu uhuru unaajiri watu 600,000, unafikiriaje ajira milioni nane? Lazima tuweke msukumo mkubwa katika private sector (sekta binafsi). Lazima tukafanyie kazi changamoto zote zilizoelezwa,” alisema.

Baadhi ya wabunge ambao wameonekana kushambulia wenzao ni Joseph Musukuma na Livingstone Lusinde, huku January Makamba (Bumbuli (CCM) na Kilumbe Ng’enda (CCM Kigoma Mjini) wakionekana kutuliza hali ya hewa.

Hali hiyo imemfanya Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dk Benson Bagonza naye kutoa neno akisema “Bunge linaomboleza vibaya”.

Livingstone Lusinde

Hali ya kushambuliana ilianza juzi baada ya Mbunge wa Mvumi (CCM) Livingstone Lusinde kuwashukia wabunge wenzake na viongozi wengine aliosema “wanaopinga mambo mazuri yaliyofanywa na Hayati Magufuli.”

"Mhe. Spika nataka nipige mabomu ya ndani, lakini nipige ya masafa marefu"

Akichangia Bajeti ya Waziri Mkuu, Lusinde alisema haiwezekani kuwa na amani na utulivu wakati kuna watu wanamsema vibaya Magufuli na haiwezekani kuwa na viongozi nchini ambao wanajaribu kupinga mambo mazuri yaliyofanywa na kiongozi huyo.

“Hatuwezi kuwavumilia hawa wanaomsema vibaya Magufuli, watamsema vibaya Rais Samia, hii ni tabia jamani, Magufuli amefanya kazi nzuri sana nchi hii. Lazima tukubaliane, unajua kuna wengine wanafikiri Rais Samia alikuwa benchi akaingia kucheza mpira, hapana. Samia alikuwa akicheza pamoja na Magufuli,” alisema.

Joseph Musukuma

Mbunge mwingine aliyeonyesha kukerwa na hali hiyo ni Joseph Musukuma (CCM, Geita Vijijini), ambaye moja kwa moja alimshambulia mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo kutokana na mchango wake uliokosoa Sekta ya Madini na Nishati.

Musukuma alisema Muhongo alipokuwa waziri wa Nishati na Madini hakusaidia sekta ya madini kukua kama ilivyo sasa, huku akitamba yeye ni mhitimu wa darasa la saba, mbali na kushambulia uprofesa wa Muhongo na wasomi aliosema waliwekwa kwenye mgodi wa Tanzanite wa Mererani, kwamba hawawezi kazi na wanaibiwa tu.

Tazama 'Mbunge Musukuma' alivyomshukia 'Prof. Muhongo' bungeni leo

Musukuma alishauri wapelekwe wahitimu wa darasa la saba kutoka kijijini kwake wanaoweza kujua madini kwa kutumia tochi badala ya vifaa vya kisasa.

Alisema michango inayotolewa na wabunge wengi wasomi haina tija na baadhi inalenga kupotosha.

Musukuma alimtaja moja kwa moja Profesa Muhongo kwamba alipokuwa waziri alishindwa kutumia elimu yake kulisaidia Taifa, badala yake alipeleka hasara serikalini kwa kukataa kushauriwa, lakini sasa amekuwa mstari wa mbele kukosoa.

“Nilimwambia hadharani kuwa hawa watu wanatuibia lakini yeye akachukua kipaza sauti akatangaza hadharani kwamba Geita Vijijini mmechagua mbunge wa ajabu, tatizo hana elimu ya kupambanua mambo,” alisema Musukuma.

Mapema, Profesa Muhongo akichangia mpango wa maendeleo, alisema uchumi wa gesi pekee ndio utaifikisha Tanzania kwenye uchumi thabiti na imara badala ya kuzungumzia mafanikio ya umeme wa maji ambao alisema itachukua muda mrefu kuanza kutoa faida, hoja iliyowagusa baadhi ya wabunge wa CCM na kumuona kama msaliti.

“Kinachotakiwa ni kujikita katika matumizi ya umeme mchanganyiko badala ya kutegemea mabwawa ya maji ambayo wakati wowote yanakwenda kukauka, halafu unasema utaleta fedha, huko ni kujidanganya kwani umeme wa maji huchukua muda mrefu kuanza kutoa faida, huku wenzetu wamepita,” alisema Profesa Muhongo.

Kuhusu madini alisema dunia ya sasa imegeukia madini mengine ambayo yapo ya kutosha Tanzania, hivyo wasielekeze kwenye dhahabu na Tanzanite ambayo hayatengenezi vitu vya kisasa.

Hata hivyo, wakati wa kujibu hoja za wabunge, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema duniani kote umeme wa maji ndiyo mkombozi namba moja kwa uchumi kwa kuwa unatumia gharama ndogo kuuzalisha.

Dk Kalemani alisema kuna watu wanapotosha ukweli na kuwafanya watu wawaamini wakati wanachozungumza hakina ukweli ndani yake.

Mbunge Shabiby

Mwingine aliyewanyuka wenzake ni mbunge wa Gairo (CCM) Ahmed Shabiby, aliyewatuhumu baadhi ya wabunge kula rushwa huku akionya kwamba wakimkera atawataja.

Shabiby alikuwa anazungumzia Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta na Maji (Ewura) kuwa imekuwa inachukua kati ya Sh16 hadi Sh17 kwenye lita moja ya mafuta kwa ajili ya kuweka vinasaba kwenye bidhaa hiyo.

Mbunge asema kuna baadhi ya wabunge walikuwa wanakula rushwa nje nje tena mkinikera nitawataja

Alisema vinasaba hivyo vimeleta mzozo ambao ulifanya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuvunja kamati ya Nishati na Madini wakati wa Bunge la kumi na moja.

“Walikuja hapa kwako wakataka wakusomeshe, lakini wewe ukawafukuza. Baadhi ya wabunge hapa walikuwa wanakula rushwa njenje, tena mkinikera nitataja, lakini basi leo wacha ninyamaze kwa sababu ya kutetea huu wizi,” alisema.

Kauli ya Shabiby ilimfanya Gambo aombe kutoa taarifa, na alipopewa nafasi alimtaka mbunge huyo awataje wabunge waliokula rushwa kwa sababu ni tuhuma nzito, ili wengine wasiohusika wabaki na heshima zao.

Mbunge Makamba

Baada ya mivutano ya hapa na pale, ndipo ikaja zamu ya Makamba (Bumbuli) akatumia muda wake kusawazisha hali ya hewa.

Alisema kauli za utengano, kutiliana shaka, kutuhumiana na kuhujumiana hazijengi na zinawachanganya Watanzania.

Alisema kazi aliyoifanya Rais Magufuli anaweza kuichukulia kama fundi alishona nguo nzuri ikitokea mtu akaona kuna uzi umejitokeza isionekane kuwa ni dhambi.

Makamba atema cheche bungeni | Mambo makubwa aliyofanya Magufuli hayatafutika || Watu wasibezwe

“Akatokea mtu akasema kwenye hii nguo kifungo kimelegea hebu tukiweke vizuri isionekane kuwa huyu mtu ni msaliti. Na mtu huyo anapokaza kifungo, kukata uzi na nguo ikapendeza bado sifa ni ya mshonaji,” alisema.

Ushauri huo wa Januari ulimwinua tena Musukuma jana jioni alipopewa nafasi ya kutoa taarifa wakati Deo Sanga (CCM Njombe Kaskazini) anachangia, akasisitiza kuwa wanaona nongwa kwa wakosoaji wote waliokosoa, walikula viapo na viapo vinaendelea hata ukitolewa kwenye madaraka.

“Tutaendelea kuwapiga hadi watambue umuhimu wa kiapo walichokiapa,” alisema Musukuma.

Aliposimama Kilumbe Ng’enda aliwataka wabunge kuishi kwa kuheshimiana na kuvumiliana kwa kutorushiana maneno.

Alisema Taifa lilipopata msiba wa Magufuli lilihuzunika, watu hawakuamini na walijiuliza nini hatima ya Taifa baada ya kuondoka kwake.

“Sisi makada tuliobobea vinenoneno vingine tulivyoviona vinapita tulivitarajia. Ninachokiomba sisi wenye mapenzi mema wenye kujua kazi ya Rais Magufuli tutumie busara sana katika kusema jambo lolote lile,” alisema.