VIDEO: NEC yatangaza uchaguzi mdogo ubunge na madiwani

NEC yatangaza ratiba ya uchaguzi jimbo la Konde

Muktasari:

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza ratiba ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba na kata sita  za Tanzania Bara.

Dodoma. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza ratiba ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba na kata sita  za Tanzania Bara.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dodoma leo Alhamisi, 3 Juni, 2021, na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC  Dk Willson Mahera,  imesema uchaguzi huo umeapangwa kufanyika tarehe  Julai 18,2021.

 “Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, ameitaarifu tume uwepo wa nafasi wazi ya kiti cha ubunge katika jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba,” imesema taarifa hiyo.

Kiti cha ubunge wa jimbo la Konde, kiko wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Khatib Said Haji aliyefariki hivi karibuni katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Aidha, Tume imepokea barua kutoka kwa waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,  akiitaarifu juu ya kuwapo kwa nafasi za wazi za madiwani katika kata sita  za Tanzania Bara.

“Kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 37(1)(b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Kifungu cha 13 (2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, sura ya 292, Tume imeandaa chaguzi ndogo ili kujaza nafasi ya mbunge iliyo wazi katika jimbo la Konde na nafasi za udiwani kwenye kata sita (06) za Tanzania Bara,” iliongeza kusema taarifa hiyo.

Kata zitakazohusika katika uchaguzi huo ni  Mbagala Kuu jimbo la Mbagala Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Diringish iliyopo jimbo la Kiteto, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara,  Mitesa iliyopo jimbo la Lulindi, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Kata nyingine ni  Gare, jimbo la Lushoto Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Mchemo iliyopo  Newala Vijijini, Wilaya ya Newala mkoani Mtwara na kata ya Chona iliyopo jimbo la Ushetu, Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga.

 Maandalizi kwa ajili ya uchaguzi huo yameshafanyika na kazi ya utoaji fomu za uchaguzi kwa wagombea inaanza Juni 21 hadi 27,2021, huku uteuzi wa wagombea watakao =wania nafasi hizo ukifanyika Juni 27 mwaka huu.

Aidha Dk Mahera amesema kampeni za uchaguzi katika jimbo la Konde na kata hizo utaanza Juni 28, 2021 na zitafikia ukomo wake Julai 17 mwaka huu na uchaguzi kufanyika 18 Julai, 2021.