VIDEO: Rais Samia na Kenyatta wakubaliana mambo matano

LIVE: Rais Samia awasili nchini Kenya

Muktasari:

  • Tanzania na Kenya zimekubaliana mambo matano kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa nchi hzi mbili.


Dar es Salaam. Tanzania na Kenya zimekubaliana mambo matano kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa nchi hzi mbili.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo Jumanne Mei 4, 2021  jijini Nairobi nchini Kenya baada ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwasili nchini humo kwa ziara ya siku mbili, kupokewa na mwenyeji wake Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Mambo hayo ni kuimarisha tume ya ushirikiano wa nchi hizo na kuwataka mawaziri wa pande mbili kukutana mara kwa mara kujadili ushirikiano huo.

Mengine ni kuimarisha sekta ya mawasiliano, mkataba wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam kwenda Mombasa, kuimarisha usalama na mkataba wa kuimarisha utamaduni na masuala ya kijamii.  

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kumkaribisha Rais Samia, Kenyatta amesema Wakenya wanaichukulia Tanzania kama ndugu.

“Tumekubaliana kwamba tutaimarisha ile joint commission cooperation (tume ya ushirikiano) ya nchi hizi mbili na mawaziri wetu wameambiwa wawe wanakutana mara kwa mara kuhakikisha kwamba wanazingatia uhusiano wetu na kutatua shida ndogo ndogo zinazosumbua wananchi wetu.”

“Wanapofanya biashara wakati wawekezaji wanakuja ama kutoka Tanzania au Kenya, tuhakikishe kwamba tumeimarisha masuala ya kibiashara, kiuchumi na kitamaduni ambayo yatatusaidia kujenga Taifa letu la Kenya na Tanzania kwa manufaa yetu sote,” amesema Rais Kenyatta.

Kuhusu mawasiliano amesema wamekubaliana kuiamrisha usafiri wa ndege, safari za reli na usafiri wa maji na barabara.

“Pia tumesema tutaweka kipaumbele cha kuharakisha barabara kutoka Malindi, Lungaluunga mpaka tufike Bagamoyo. Pia tutaanzisha safari za Ziwa Victoria wakati wananchi na mizigo inayopita kutoka Jinja, Kisumu, Mwanza Bukoba, ili kurahisisha biashara za wananchi wetu,” amesema.

Kuhusu usalama amesema wamekubaliana kuimarisha mapambano dhidi ya ugaidi, “tumeweka mikataba ya mambo ya kujenga bomba la gesi kutoka Dar es Salaam mpaka Mombasa ambayo itarahisisha bei ya stuima katika nchi yetu na itahakikisha viwanda vyetu vinapata stuima na energy itakayokuwa inalinda mazingira kwa Kenya.”

“Pia tumeweka kidole mkataba wa kuimarisha uhusiano katika mambo ya utamaduni, ushirikiano wa kijamii na mengineyo kuhusu utalii.”

Kwa upande wake Rais Samia amesema Kenya ni mdau mkubwa wa biashara na uwekezaji.

“Kwa mfano, wakati wa mazungumzo yetu nimemwarifu Kenyatta kuwa Kenya inashika nafasi ya tano kwa uwekezaji nchini kiulimwengu, lakini ka nchi za Afrika Mashariki inashika nafasi ya kwanza.”

“Imewekeza miradi 513 yenye thamani ya Dola 1.7 bilioni ambayo imetoa ajira 51,000 za Watanzania. Zipo kampuni 30 za Tanzania zimewekeza mtaji ndani ya Kenya wenye thamani ya Ksh19,330 milioni na kutoa ajira kwa watu 2,640 hivi. Nikatoa ahadi kwamba Watanzania tutakuja ili kukuza ukubwa wa biashara,” amesema Rais Samia.

Amesema kwa miaka mitano iliyopita wastani wa biashara kati ya Tanzania na Kenya ni Sh1 trilioni au Dola 450 aliosema unahitaji kuongezwa.

“Kwa lengo la kukuza biashara na uwekezaji, tumekubaliana kuendelea kufanyia kazi changamoto hususani vikwazo visivyo vya kodi hivyo sasa viondoke na tumekubaliana kuwa tume yetu ya ushirikiano iwe inakaa na kutoa suluhuu ya vikwazo vinavyotokea,” amesema.

Kuhusu mapambano dhidi ya maambukizi ya corona, Rais Samia amesema wamekubaliana kuwa mawaziri wa afya wa nchi hizo wakutane  kuangalia na kurahisisha mfumo kukabiliana na ugonjwa huo.

Akizungumzia suala la ushirikiano, Rais Samia amesema wamekubaliana kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa pamoja na kuhamasisha nchi wanachama kulipa michango yao. 

“Mwisho wa mwaka huu Desemba Tanzania inatimiza miaka 60, kwa hiyo tumetuma mwaliko Kwa Rais Kenyatta awe mgeni rasmi,” amesema Rais Samia.