VIDEO: Safari ya siku 25,742 za Lowassa kuhitimishwa leo

Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa na Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume nyumba kwa hayati Edward Lowassa . Picha na Said Khamisi

Muktasari:

  • Mchana wa leo Jumamosi, Februari 17, 2024 ndio itakuwa mara ya mwisho kuuona mwili au jeneza la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika sura ya dunia.

Monduli. Mchana wa leo Jumamosi, Februari 17, 2024 ndio itakuwa mara ya mwisho kuuona mwili au jeneza la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika sura ya dunia.

Lowassa atakuwa anahitimisha safari ya siku 25,742 duniani kwa mwili wake kuhifadhiwa katika makazi yake ya milele yaliyopo nyumbani kwake, Kijiji cha Ngarash, Wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha.

Maelfu ya waombolezaji wamejitokeza kijijini hapo kutoka maeneo tofauti ya ndani na nje kushiriki safari hiyo ya mwisho ya 'Mtu wa maamuzi magumu' kama anavyoelezwa na watu mbalimbali kwenye salamu zao za rambirambi.

Pumzi ya mwisho ya Lowassa ilikata saa 8 mchana wa Jumamosi ya Februari 10, 2024 akiwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya utumbo kujikunja, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.

Rais Samia kushiriki ibada ya mazishi ya Lowassa

Pumzi ya kwanza aliivuta Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, siku aliyozaliwa akiwa mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa.

Hadi anafikwa na mauti, Lowassa alikuwa ameishi siku 25,735 sawa na miaka 70 na miezi mitano. Sawa na miezi 845 na siku 15.

Hadi anazikwa leo Jumamosi ambapo si jeneza lenye mwili wake au mwili wake utaonekana ni sawa na siku 25,742.

 Ibada ya mazishi, inaongozwa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa akiwa na maaskofu wenzake 11, wachungaji na wainjiristi.

Msafara wa viongozi hao wa dini umeingia viwanja maalumu vya mazishi saa 3:10 asubuhi hii.

Hadi saa 1:45 asubuhi ya leo , ndani kulikuwa kumejaa kwani waombolezaji wameanza kuingia saa 9 alfajiri. Magari binafsi, mabasi na makubwa  yaliyotoka mikoani ni mengi sana.

Viongozi mbalimbali wamekwisha kufika wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu, marafiki wa Lowassa 'Friends of Lowassa.'

Safari hii ya mwisho ya "Mwana Matumaini" itaongozwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Televisheni mkubwa zimefungwa maneno mbalimbali ili kuruhusu waombolezaji waliokaa kwenye mahema ndani na nje ya nyumba kufuatilia tukio hilo, wakiwa hapohapo kijijini kwa Lowassa.

Katika siku hizo alizoishi hapa duniani, Lowassa alimuoa Regina na kubarikiwa kupata watoto watano, wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert na Richard wa mwisho.

Jana Ijumaa, Februari 16, 2024, Fredrick ambaye ni mtoto mkubwa alisema huo ndio msiba mkubwa wa kwanza kutokea, “kwenye familia yetu. Hatujawahi kupata msiba mkubwa kama huu."

Fredrick ambaye pia ni Mbunge wa Monduli amesema licha ya yeye kuwa mtoto mkubwa, "lakini mrithi wa ardhi hii (nyumbani hapo) na nyumba ni mtoto wa mwisho ambaye ni Richard wala si mimi."

Kuhusu waliotofautiana na baba yake, Fredrick amesema hajawahi kumsikia baba yake akisema fulani ni adui yake kwa kinywa na hata alipoelezwa na watu fulani na fulani ni maadui aliwajibu, "yawezekana hamjamuelewa au alighafirika kwa jambo hili na lile. Kwa hiyo baba hajawahi kumtaja adui yake kwa kinywa chake."

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ndiye alitangaza kifo hicho kwa niaba ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Dk Mpango amesema, Lowassa alifariki baada ya kuugua magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.

“Hayati Edward Lowassa ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu tangu Januari 14, 2022 JKCI na baadaye akapelekwa kwa matibabu zaidi nchini Afrika Kusini na kurejea tena JKCI,” amesema. 


Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa na Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume nyumba kwa hayati Edward Lowassa . Picha na Said Khamisi

Lowassa ni nani?

Edward Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa.

Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967. Kisha akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 - 1971, kabla ya kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora mwaka 1972–1973.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu na baadaye Chuo Kikuu cha Bath, Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).

Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.

Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990.

Lowassa alichaguliwa kuwa Mbunge wa Monduli mwaka 1990 na 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge), kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi na Makazi akiwa Waziri mwaka 1993–1995.

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi (mwaka 1995), Lowassa alishinda ubunge kwa asilimia 87.3. Alikaa bila uteuzi wowote kwa miaka miwili.

Mwaka 1997–2000, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Kuondoa Umasikini).

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 aligombea tena ubunge wa Monduli na kushinda kwa mara ya tatu. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Maji na Mifugo hadi mwaka 2005.

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005, aligombea ubunge na kushinda kwa asilimia 95.6. Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Bunge likamthibitisha kwa kura 312.

Uwaziri mkuu wa Lowassa ulikoma Februari 7, 2008, alipojiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond.

Kamati Maalumu ya Bunge ya watu watano iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ilisisitiza kuwa wizara ya Nishati na Madini na Ofisi ya Waziri Mkuu ndizo zinazopaswa kubeba lawama ya uingiaji wa mkataba mbovu na Richmond, kampuni ambayo uchunguzi ulionyesha ni ya mfukoni mwa watu huku Serikali ikilazimika kulipa mabilioni ya fedha katika mkataba ambao una upungufu makubwa.

Wakati Lowassa analitaarifu Bunge kuwa amemuandikia Rais barua ya kujiuzulu, alisisitiza kuwa “…anafanya hivyo ili kulinda taswira ya chama chake na Serikali na kuwa shida ya wabaya wake ni u-waziri mkuu na siyo kingine…”

Baada ya kujiuzulu, Lowassa aligombea ubunge kwa mara nyingine Monduli (mwaka 2010) na kupata asilimia 90.93 ya kura zote.

Lowassa ni miongoni mwa wana-CCM 17 waliochukua fomu kuwania urais mwaka 1995 lakini aliyepitishwa ni Mkapa. Mwaka 2015, alijitosa kuwania uteuzi ndani ya CCM kuwania urais. Hata hivyo, jina lake lilikatwa.

Baada ya kukatwa, Julai 28, 2015, Lowassa aliandika historia mpya katika maisha yake ya kisiasa na nchi kwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza kuhamia chama pinzani cha Chadema.

Chadema kilimteua kuwania urais. Alindika historia nyingine kwa kupata kura nyingi ambazo hajawahi kupata mgombea wa upinzani wa urais tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995.

Lowassa alipata kura milioni sita sawa na asilimia 40 nyuma ya mgombea wa CCM, John Magufuli aliyepata kura milioni nane sawa na asilimia 58.


Endelea kufuatilia Mwananchi kupata habari za kila kinachoendelea Monduli yanakofanyika mazishi ya kiongozi huyo...