VIDEO: Ukweli sakata la diwani kukutwa kwa Ashura

Ukweli sakata la diwani kukutwa nyumbani kwa Ashura

Muktasari:

  • Diwani wa Kawe (CCM), Mutta Rwakatare aliyekuwa amepotea na kisha kupatikana nyumbani kwa mwanamke anayeitwa  Ashura, ameahidi kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya Kinondoni kuwa hatopotea tena huku mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akianika ukweli kwa Sakata hilo.

Dar es Salaam. Diwani wa Kawe (CCM), Mutta Rwakatare aliyekuwa amepotea na kisha kupatikana nyumbani kwa mwanamke anayeitwa  Ashura, ameahidi kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya Kinondoni kuwa hatopotea tena huku mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akianika ukweli kwa Sakata hilo.

Mutta ameyasema hayo leo Ijumaa Juni 24,2022 katika kikao hicho kilichoketi kujadili ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Baada ya Meya wa Manispaa hiyo,  Songoro Mnyonge kumaliza kuzungumza na kumkaribisha mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Amos Makalla naye alimpa nafasi Rwakatare  azungumze.

Rwakatare  aliyekuwa amekaa kwenye kona ya ukumbi amesema, "kwanza nikushukuru mkuu wa mkoa. Pia nitumie kikao hiki kuahidi kwamba sitapotea tena kwani nilikuwa kwenye 'Royal Tour' ya Lost and Found."

Naye Makalla amesema Ashura anayedaiwa kumteka Rwakatare  aliwasiliana naye wiki moja kabla ya tukio hilo kutokea.

"Ashura mimi namfahamu kwa kuwa alikuwa mke wa rafiki yetu Macheni lakini baada ya mumewe kufariki aliolewa huko Ujerumani."

"Alinipigia simu wiki moja kabla ya tukio kunieleza masuala yake binafsi ya kurudi nchini akitokea Ujerumani na kuna msaada alikuwa anahitaji kutoka kwangu. Hata hivyo,  mara baada ya tukio la Mutta kutokea na kupiga simu kuona namba inayotokea ni yake (ya Ashura) ilibidi  nimuhoji (Ashura)  kulikoni kufanya hivyo na alinielezea yote na kubaini hakuwa mtekaji kama watu wanavyosema."

"Yule ni rafiki wa familia ya kina Mutta  na hata walipomnasa Mutta walimkuta ndio amempa supu ya kuku," amesema Makalla.