VIDEO: Wanandoa wawekwa ndani kwa amri ya DC Sabaya

Thursday January 21 2021
By Daniel Mjema

Moshi. Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya ametoa agizo la kukamatwa kwa mfanyabiashara,  Alex Elibariki Swai na mkewe kwa tuhuma za ukwepaji kodi na uuzaji pombe bandia.

Sabaya ametoa amri hiyo usiku wa kuamkia leo Januari 21,2021 alipofanya msako wa kushtukiza katika duka la mfanyabiashara huyo lililopo nje kidogo ya mji wa Bomang’ombe na kushuhudia kile alichodai ni madudu ukwepaji kodi na uhujumu uchumi.

Akiwa amefuatana na maofisa wa Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  aliamuru kukamatwa papo hapo kwa mfanyabiashara huyo na mkewe, Neema.

Kwanza alipofika katika duka hilo alianza  kumhoji mfanyabiashara huyo aina ya biashara anayofanya kwa mujibu wa leseni yake, naye akadai ni duka la rejareja, lakini timu ilipoingia ndani inadaiwa kukuta hali tofauti.

Upande wa nyuma wa duka hilo, kulikutwa masanduku yanayodaiwa kufikia 800 ya bia za aina mbalimbali, sanduku za soda, pombe kali zinazodaiwa ni bandia na mapipa ya Diesel na bidhaa nyingine.

“TRA na Takukuru, nataka mumchunguze mfanyabiashara huyu kwa miaka mitatu tupate kodi ya serikali. Ukitizama hapa makadirio ya kodi ni ya duka la rejareja kumbe kinachofanyika ni biashara ya jumla,” amesema Sabaya.

Advertisement

Sabaya alienda mbali na kuwaagiza maafisa wa TRA kuchunguza stika zilizokutwa katika chupa za pombe kali zinazodaiwa kuwa ni za bandia, zilitolewa kwa mfanyabiashara gani hadi ziingie mikono isiyo salama.

Katika purukushani hiyo, walikutwa na watu wengine wawili ambao walikuwa tayari wamenunua bidhaa dukani hapo, lakini wakapewa risiti ya elektroniki (EFD) kutoka kwa mfanyabiashara mwingine wa jumla.

Mmiliki huyo wa duka alipoulizwa ilipo mashine yake ya EFD, alidai kuwa iko kwa wakala kwa ajili ya kuingizwa alama za utambuzi (QR Codes), lakini maofisa wa TRA waliokuwepo walipoulizwa wakadai hawana taarifa hiyo.

Advertisement