Video ya mateso dhidi ya mtoto yawaibua Polisi, Wizara
Dar es Salaam. Video vya mateso, ukatilli na unyama dhidi ya mtoto mdogo iliyosambaa mitandaoni, imeiibua Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kulaani vikali kitendo hicho.
Wakati wizara ikieleza hayo, Jeshi la Polisi limetaka mwenye taarifa za mtuhumiwa wa kitendo hicho kutoa taarifa ofisi yoyote ya serikali na au kituo cha polisi ili hatua sitahiki ziweze kuchukuliwa.
Hatua hiyo inatokana na kipande cha video kilichosambaa mtandaoni leo Jumanne, Septemba 19, 2023 kikionesha mwanamume mmoja akiwa amemfunga mtoto juu kwa kamba huku akining’inia mithili ya nyama buchani.
Kipande hicho cha video cha sekunde 14 kimesambaa mitandaoni na kuibua mijadala mikali.
Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime imesema,“tunatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za nani alifanya kitendo hicho au kilifanyikia wapi asisite kutoa taarifa polisi au kwa kiongozi yeyote kufanikisha kukamatwa kwa muhusika.”
“Pia, mtoto huyu lazima atakuwa na mama, baba, babu, bibi, shangazi, mjomba, majirani na viongozi wa serikali za mitaa.”
Wakati Polisi likimsaka mtuhumiwa huyo, Kamishana wa Ustawi wa Jamii, Dk Nandera Mhando ametoa taarifa juu ya tukio hilo akisema wizara inalaani ukatili huo uliofanyika kwa mtoto huyo na kusababishia mateso, udharirishaji na kumuondolea utu wake.
“Watoto wanahaki ya kulindwa, kupendwa, kuendelezwa, kushirikishwa na haki nyingine zote za binadamu,” amesema Dk Mhando
Pia, imesema hakuna sababu inayoweza kukubarika kufanyika kwa ukatili huo mbaya uliofanywa na mtu anayesadikika kuwa ni mzazi, mlezi au mtu wake wa karibu wa mtoto huyo.
“Mtu huyo kimsingi anategemewa awe mlinzi namba mmoja kwa mtoto wake dhidi ya vitendo vyote vya ukatili kwa mujibu wa kifungu cha 9(a,b) cha sheria ya mtoto. Kitendo kilichofanywa na mtu huyo ambaye hajafahamika jina lake anawakilisha kundi la wazazi au walezi wenye tabia ya kuadhibu watoto kwa vitendo visivyo vya kibinadamu,” amesema
Dk Mhando amesema,“wizara inatoa wito kwa wazazi au walezi pale wanapoona watoto wao wanaonyesha tabia kinzani au zisizofaa wawashirikishe wataalamu wa huduma za ustawi wa jamii, wanasaikolojia na viongozi wa Dini zao ili kupata msaada wa marekebisho ya tabia zao na kuepusha ukatili,” amesema