Viera: Mkimbizi kutoka Kenya anayekaribia kuwa mwamuzi EPL

Thursday January 14 2021
verapic
By Mwandishi Wetu

Nairobi, Kenya. Kijana mkimbizi kutoka nchini Kenya, Jacob Viera anayetafuta riziki katikati ya miji ya London, Liverpool na Manchester huenda akaukwaa uamuzi wa soka huko Uingereza.

Katika umri wake mdogo akiwa ndio ameanza kutafuta maisha katikati mwa Jiji la Nairobi wakati akianza kucheza soka akiwa chini ya miaka 16, Viera alinusurika kifo. Umewahi kukutana na wahuni wa mjini? Unaijua shughuli yao?

Ilianza kama utani. Viera alikuwa mmoja wa vijana waliounda timu ya taifa ya Kenya ya vijana wa chini ya miaka 16 (U16) iliyokuja Arusha kushiriki mashindano ya Kanda ya U16 yaliyoshirikisha Kenya, Uganda, Rwanda, Zanzibar, Burundi, Msumbiji na Tanzania Bara. Alikuwa na furaha.

Kabla ya safari, timu ya Kenya iliweka kambi ya wiki mbili katika hoteli moja jijini Nairobi. Ni katika hoteli hiyo alikutana na wanaume watano waliotaka kujua siku ya timu kusafiri, na walikuwa na kazi maalumu ambayo walitaka awafanyie.

Kwa mujibu wa maelezo ya Viera alipoambiwa kuhusu kazi hiyo aliogopa. Kisa? Kwa udogo alionao alifikiria kwamba angehusishwa katika usafirishaji wa dawa za kulevya. Akilini alianza kuwaza mambo mengi. Hatari iliyokuwa mbele yake aliiona kwa ukaribu iwapo ni kuhusishwa katika shughuli hiyo haramu.

“Niliogopa sana. Kwa umri mdogo niliokuwa nao nilijua hatari ya kukubali kazi waliyotaka niifanye. Nikubali kusafirisha dawa, nikikamatwa na kufungwa au nikatae niadhuriwe na watu wale, sikujua cha kufanya,” anasema Viera katika moja ya mahojiano.

Advertisement

“Akili ilibidi ifanye kazi kwa haraka. Nilichowaza ni kuwadanganya kuhusu siku ya safari. Niliwaambia safari itachelewa tofauti na ilivyopangwa. Hii ilikuwa njia pekee ya kuepuka kutumika na watu hao. Niliwaambia marafiki zangu na kocha kuhusu watu hao.”

Mpango huo ulienda kama alivyopanga. Timu ilisafiri kwenye Arusha, ilishiriki michuano hiyo na kumaliza kwenye nusu fainali ilipoondolewa na Uganda. Mwezi mmoja baada ya timu kurudi kutoka Tanzania, vyombo vya habari vilikuwa na habari mbaya.

Habari za watu kukamatwa kwenye hoteli waliyoweka kambi wakiwa na dawa za kulevya, ilitawala kwenye vyombo vya habari. Kwa mujibu wa Viera, baada ya kusimulia kilichotokea kwa familia yake uamuzi wa kumpeleka mbali na Nairobi ulifikiwa.

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Viera aliendelea kucheza soka na aliichezea Muhoroni Youth kwa miezi sita kabla ya kurudi Nairobi. Alipata fursa ya kucheza kwenye ligi ya soka ya Kenya akiwa na Tena United na Ligi Ndogo FC. hapo alianza kupata umaarufu.

“Nikiwa Tana United nilibahatika kuwa nahodha wa kikosi kilichosheni vipaji, lakini mambo yalianza kubadilika. Nilianza kuona tofauti katika maisha yangu. Nililazimika kuzurura mitaani, nisiruhusu watu kujua ninapoishi kwa kuhofia usalama wangu,” anasema.


Shoti ya umeme

Juni 10, 2014, Viera aliporudi nyumbani akitokea mazoezini alikutana na tukio lililotishia kutoa uhai wake. Tukio hilo lililobadili maisha yake akiwa anataka kufungua mlango wa chumba uliotengenezwa kwa nondo kilichofuata kilikuwa ni kishindo kikubwa.

Baada ya hapo hakusikia chochote. Alikuwa amepigwa shoti ya umeme. Kijana huyo alirushwa sakafuni, akalala hapo kwa muda akiwa hajitambui mpaka pale jirani yake (Jimoh) alipomuona sakafuni, huku mlango ukiwa wazi.

Maelezo ya Viera mwenyewe ni kuwa kitasa cha mlango kilikuwa na nyaya za umeme. Alikimbizwa hospitali akiwa na majeraha kadhaa mwilini. Alikuwa ameunguzwa usoni, shingoni na sehemu mbalimbali za mwili kiasi kwamba madaktari walisema alihitaji miujiza kupona..

Wakati anakutwa mkasa huo uliomweka hospitali kwa zaidi ya miezi sita alikuwa anawaza safari ya kuelekea nchini Uingereza kufanya majaribio katika klabu ya Newcastle United. Baada ya kupona alifanikiwa kusafiri na kujiunga na kituo cha soka cha Newcastle United.


Newcastle, Spurs

Miaka sita baadaye kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 kwa sasa bado yupo kwenye soka na anawashukuru waliomsaidia kufika alipo japo anachofanya sasa sicho alichotaka kufanya wakati anaondoka kwenda Uingereza, kwani hakufanikiwa kupata nafasi Newcastle.

Hata hivyo, baada ya mlango huo kujifunga mwingine ulifunguka, baada ya kumvutia skauti wa Tottenham Hotspurs.

Wiki sita baadaye, Viera alipata tiketi ya basi kwenda London. Alikaa hotelini pamoja na wenzake 600 waliokuwa wanataka hifadhi kwa wiki mbili kabla hajawekwa kizuizini Hammersmith wiki tatu.

Siku ambayo alipaswa kufanya majaribio Spurs aliitwa kwa ajili ya maswali, kwa mara ya pili. Aliwekwa kizuizini na simu kuchukuliwa. Hivyo ndivyo fursa ya kujiunga na Tottenham ilivyoenda na maji. Alipoteza nafasi nyingine.

Kilichofuata alisafirishwa usiku hadi Liverpool kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi kuona kama vidonda alivyopata kutokana na mkasa wa umeme kama vinaweza kutibika. Huko alifanya mazoezi na vijana wa chini ya miaka 18 wa Everton. Bahati mbaya aliumia. Hilo likawa pigo la tatu.


Marafiki ‘wampa’ urefa

Baada ya kupoteza fursa zote za kucheza soka, Viera alianza kujifunza kazi ya uamuzi kupitia kwa marafiki zake aliokutana nao wakati anafanya mazoezi na Everton, mmoja akiwa ni Stuart Carrington ambaye ni kocha wa zamani wa kituo cha soka Everton.

Kupitia kwa Carrington ambaye kwa sasa anafanya kazi kwenye Shirikisho la Soka England (FA) jijini Liverpool (LCFA), Viera kwa sasa ni mwamuzi wa daraja la nne, anayefanya kazi kwenye programu za FA inayotoa mafunzo na fursa kwa jamii. Pia amepata uraia wa Uingereza. Kwenye makao makuu ya LCFA huko Walton Hall Park, kunakofanya kazi kwa ukaribu na Asylum Link Merseyside inayosaidia wakimbizi kupata hifadhi, ni kawaida kumkuta Viera akichezesha mechi ya wakimbizi wa zamani kutoka Syria, Somalia, Misri, Eritrea, Iran na Sudan.

Shirikisho la Soka England limefanya uamuzi wa kumpandisha daraja kutokana na umahiri anaouonyesha na hivi karibuni huenda akawa mwamuzi wa kwanza mwenye asili ya Afrika Mashariki kuchezesha mechi za Ligi Kuu England (EPL).


Kuendesha klabu

Viera pia alianzisha taasisi inayojulikana kama Klabu. Klabu ilifungua ofisi kwenye kambi ya wakimbizi ya Kalobeyei (Kalobeyei Refugee Settlement) 2019. Kuna wakimbizi 36,000 kutoka nchi 13 tofauti za Afrika kambini hapo.

Hivi karibuni, Klabu ambayo balozi wake ni nyota wa zamani wa Bolton Wanderers, Patrice Muamba ilipata msaada kutoka kwa Trent Alexander-Arnold, Alexandre Lacazette na César Azpilicueta ambao wameahidi kupitia akaunti zao jamii kuipatia fedha.

Advertisement