Vigogo wa siasa wazichambua R nne za Rais Samia
Muktasari:
- Viongozi wa kisiasa wameeleza jinsi wanavyozifahamu R nne za Rais Samia Suluhu Hassan. Wakieleza kuwa falsafa hiyo inapaswa kuungwa mkono kwa sababu italeta manufaa kwa Watanzania.
Dar es Salaam. Wadau wa siasa nchini wamezichambua R nne za Rais Samia Suluhu Hassan na kueleza namna wanavyozielewa na kuamini kuwa mwarobaini wa changamoto zinazolikabili Taifa kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Wadau wamejadili jambo hilo leo Januari 3, 2024 wakati wa mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa uliowashirikisha wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, kujadili R nne zilizoasisiwa na Rais Samia Julai 30, 2022.
Rais Samia alianzisha R nne zinazohusisha maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya, mambo ambayo wameeleza kuyaunga mkono, huku wakitaka watendaji wa Serikali nao wayatafsiri kwa vitendo.
Akizungumza kwenye majadiliano yaliyoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bakari Machumu, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira amesema tangu kuanzishwa vya mfumo wa vyama vingi, tofauti baina ya vyama vya siasa zilikuwepo licha ya kwamba zimekuwa zikibadilika.
Ametolea mfano huko Zanzibar ambako ilifikia watu kutozikana kwa sababu ya tofauti za kisiasa na mtu akifa ‘anakufa kama chama, siyo kama mtu’.
Wasira amesema maridhiano ndiyo yanakuwa msingi wa kwanza kwa sababu bila maridhiano huwezi kuzitekeleza nyingine kama mabadiliko au kujenga nchi.
"Ninaamini maridhiano ndiyo kitu cha kwanza na haliwezi kuwa jambo la siku moja, ni endelevu. Tuendelee kumuunga mkono Rais Samia kwa kuwa linakwenda kutuleta pamoja kama Watanzania," amesema Wasira.
Akiwa na mtazamo kama huo, Rais wa zamani wa Bunge la Afrika, Getrude Mongella amesisitiza kwamba R nne za Rais Samia ndiyo zinaweza kulifikisha Taifa kwenye maendeleo ambayo Watanzania wanakusudia kuyafikia.
"Maridhiano ni kuheshimu mawazo ya watu wengine, tusipofanya hivyo hatuwezi kwenda mbele," amesema Mongella wakati akishiriki majadiliano hayo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama cha ADC, Doyo Hassan Doyo amesema nia ya Rais Samia kwenye hizi R nne isisitizwe kwa wananchi pamoja na watendaji serikalini ili zitafsiriwe kwa vitendo.
"Tutengeneze mazingira ili 4R ziweze kutekelezwa kwa vitendo. Hilo likifanyika, basi Dira ya Taifa itafikiwa na kuvuka hata mipaka ya nchi," amesema Doyo.
Ameongeza kuwa kwake R nne ni uhuru wa vyombo vya habari na wa kujieleza. Amesisitiza kwamba Rais Samia anatakiwa kuungwa mkono kwa sababu amerirudisha Taifa kwenye mazingira waliyokuwa wakiyatamani.
Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema - Zanzibar, Salum Mwalimu amesema R nne za Rais zinaweza kuunganisha malengo ya maendeleo endelevu (SDG), ya mwaka 2030 na Ajenda 63.
Amesisitiza kuwa lazima Taifa liangalie nguzo zinazoangaliwa na wengine katika kujipima, iwapo na kama joto la kisiasa limepanda ni muhimu kuja na vitu kama R nne ili kulishusha.
"Ni muhimu kuja na vitu vitakavyoiwezesha Tanzania kupimwa na kuliwezesha kupiga hatua. Mabadiliko yanayozungumzwa sio kwenye siasa tu, bali kiuchumi na kijamii," amesema Mwalimu.
Naye, Katibu Mkuu wa Chadema, Ado Shaibu amesema falsafa ya R nne inaweza kulijenga Taifa kiuchumi, kisiasa na kijamii kama itatekelezwa kwa ukamilifu.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wake utakwenda sambamba na ufikiaji wa malengo endelevu ya maendeleo pamoja na Ajenda 63.
Shaibu ameungana na Wasira kwamba ni muhimu kuanza na maridhiano, hata hivyo ametofautiana naye kwa kuweka msisitizo kwenye mabadiliko kwamba ndiyo nguzo muhimu kwa Taifa.
"Nguzo imara ya reforms (mabadiliko) iende na mabadiliko ya Katiba na sheria. Mchakato wa Katiba lazima uanze sasa, nguzo ya reforms ni Katiba mpya.
"Tunataka tupate kalenda ya utekelezaji wa hatua mbalimbali katika mchakato wa kuandika Katiba, tujue hatua fulani itafanyika wakati fulani. Tunahitaji mwafaka wa kitaifa, mengi tumeyajadili huko nyuma," amesema.