Vigogo wabwagwa kura za maoni ubunge CCM Ngorongoro

Vigogo wabwagwa kura za maoni ubunge CCM Ngorongoro,

Muktasari:

  • Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Ngorongoro ,wamewadondosha wagombea wasomi na vigogo waliokuwa wanapewa nafasi  kumrithi aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, William Tate Ole Nasha aliyefariki Septemba 27 mwaka huu.


Arusha. Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Ngorongoro ,wamewadondosha wagombea wasomi na vigogo waliokuwa wanapewa nafasi  kumrithi aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, William Tate Ole Nasha aliyefariki Septemba 27, 2021.

Katika matokeo ya kura za maoni yaliyoshirikisha wagombea 17, yaliyotangazwa jana usiku na Msimamizi wa uchaguzi Gerald Munisi, Mwenyekiti wa halmashauri ya Ngorongoro Emmanuel Oleshangai ndiye aliyeongoza kwa kupata kura 420   akifuatiwa na  Mkurugenzi wa Shirika la Wafugaji (TPCF)Joseph Parsambei aliyepata kura 187.

Wagombea waliokuwa wakipewa nafasi kubwa lakini hawakupata kura nyingine ni wahadhiri, Dk Elifuraha Lalkaita anayefundisha Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira na Dk Kokei Malubo anayefundisha Chuo cha Wanyamapori cha Mwika.

Wakili maarufu Daudi Haraka naye amepata kura chache sawa na Mkurugenzi wa Taasisi ya udhibiti  wa ubora wa mbegu (TOSCI )Patrick Nambolo Ngwediagi.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti  wa halmashauri ya Ngorongoro Elias Ngorisa alipata kura136, Patrick Nambolo ambaye ni Mkurugenzi wa TOSC amepata kura 61,  Dk. Kokel Melubo kura 56, Moloimet Olorwas kura  21,Mesha Pius kura 19, Patrick Girigo kura 10, Elizabeth Sinodya kura 7 na mtoto wa aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo hilo,William Telele kura 7.

 Wakili Daudi Haraka kapata kura 5, Dk Elifuraha Laltaika kura 4,Rose Njilo kura 03,Elionora Sangei kura 02, Leyan Sabore kura 1,Elias Nagore -01 na James Taki hakupata kura

Hata hivyo Katibu CCM Wilaya ya Ngorongoro Amos Shimba amesema kura hizo sio ushindi kwakuwa majina yote yatatumwa uongozi wa ngazi za juu za Chama hicho kwa mujibu wa taratibu.

"Mchakato bado vikao vya juu ndio vitapitisha  jina moja la Mgombea atakayewakilisha Chama hicho kwenye Uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Desemba 11, 2021" amesema.