Vijana 14 watua kuchangamkia fursa ya kilimo biashara Morogoro
Muktasari:
- Vijana hao 14 ambao wameagwa leo Januari 30 kwenda mkoani Morogoro kwa ajili ya kujihusisha na kilimo biashara watanufaika na mkopo wa zaidi ya Sh400 milioni na kwamba utasaidia kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana hapa nchini.
Rombo. Katika kukabiliana na changamoto ya ajira nchini, vijana 14 waliopewa mafunzo ya kilimo biashara katika Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wamepewa mikopo ya zaidi Sh400 milioni kwa ajili ya kwenda kuzalisha mazao ya bustani ikiwemo nyanya, hoho, matango na pilipili.
Vijana hao watazalisha mazao hayo kwa mkataba, ambapo kila kijana atakopeshwa jumla ya Sh28.6 milioni fedha ambazo zimetolewa na benki ya Equity, kwa udhamini wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO) kwa kushirikiana na ofisi ya Mbunge wa Rombo.
Akiwaaga vijana hao leo, Kaimu Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Rombo, Abdallah Chumu aliwataka vijana hao kwenda kufanya kazi kwa uaminifu na kuchapa kazi na kuzitumia fedha hizo kwa matumizi yaliyokusudiwa.
"Nimpongeze sana Mbunge wetu wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda, kwa juhudi anazozifanya za kuhakikisha vijana wake wa Rombo wanapata ajira kwa kujiari na hii sio kazi rahisi kama mnavyofikiri, nendeni mkawajibike ili dhamira ya mbunge ikapate kwenda kutimia kwenu,"
"CCM tunamshukuru sana mbunge wetu kwa uwajibikaji wake kwa kuhakikisha vijana wetu wanajiajiri wenyewe kwa kutumia fursa hii ya kilimo kule Morogoro. Ametusaidia kupunguza mzigo wa lawama kwa vijana, ni heshima kubwa sana kwa hiki alichokifanya kwa vijana wetu," amesema.
Aidha aliwataka vijana hao kuhakikisha dhamira waliyopambaniwa inatimia na kwamba kupitia nafasi hiyo wazalishe ajira nyingine na fedha zilizotolewa zitumike kwa matumizi yaliyokusudiwa.
"Mhakikishe mnafikisha dhamira ya waliowapambania, tunatarajia kupitia ninyi pia muweze kuzalisha ajira nyingine, nendeni mkatumie hizi fedha kwenye matumizi yaliyokususdiwa ili kusudi msiwaangushe waliobeba dhamana yenu na kusema hawa vijana ni waaminifu, wachapakazi," amesema.
"Nendeni mkafungue fursa za wenzenu wengine, mkawajibike na kutekeleza yale ambayo mmekusudia, ili mkafungue milango kwa wengine na mjue mnaenda kuibeba taswira ya Rombo lakini kumsaidia mbunge kwamba amewamini vijana sahihi," amesema.
John Mrina, ambaye ni Katibu wa Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda aliwataka vijana hao kutumia fursa waliyoipata kwa uaminifu mkubwa na kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
"Profesa Mkenda amepambana na kuhakikisha anatekeleza ahadi zake za kuwawezesha vijana kiuchmini kama alivyoahidi lakini kaonyesheni mfano kwamba vijana hasa wanaotoka katika wilaya hii wanaweza kufanya mapinduzi makubwa katika kilimo na kuinua uchumi wa nchi," amesema.
"Leo hii vijana mmekopeshwa Sh28,633,000 kila mmoja, fedha ambazo zimetolewa na benki ya Equity kwa udhamini wa chuo cha SUGECO na ofisi ya mbunge, katumieni nafasi hii kuleta mafanikio makubwa katika kilimo," amesema.
Blandina Shirima, ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mradi huo, amemshukuru mbunge huyo na kusema kuwa fursa hiyo wataitumia kama chachu ya fursa ya maendeleo kwa vijana na kwamba wanategemea kufanya makubwa katika kilimo.
"Tumepata mafunzo ya kilimo biashara kupitia kwa mbunge wetu, ni mafunzo mazuri na yametujengea uwezo mkubwa na tunatetegemea makubwa katika kilimo, naamini fedha hizi tulizopatiwa tutaenda kuzifanyia mambo makubwa katika sekta ya kilimo hapa nchini na kuwa wakulima wa mfano," amesema.
"Tunaamini kilimo kinalipa kuliko hata ajira za kukaa Maofisini, kuna watu wanathamni sana ajira za ofisini lakini naamini katika kilimo hiki ambacho tunaenda kukifanya kitaleta manufaa makubwa sana kwetu sisi vijana," amesema Shirima