Vijana 25,503 wahitimu mafunzo JKT, 501 wakishindwa

Vijana 25,503 wahitimu mafunzo JKT, 501 wakishindwa

Muktasari:

  • Jumla ya vijana 25,503 wamehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya mujibu wa sheria kwa wahitimu wa kidato cha sita mafunzo yaliyotolewa katika vikosi 19 nchini.

Butiama. Jumla ya vijana 25,503 wamehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya mujibu wa sheria kwa wahitimu wa kidato cha sita mafunzo yaliyotolewa katika vikosi 19 nchini.

Takwimu hizo zimetolewa leo ijumaa Septemba 24, 2021 na Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajab Mabele wakati akifunga mafunzo kwa wahitimu wa mafunzo hayo katika kikosi cha Jeshi cha 822 Rwamkoma wilayani Butiama.

Mabele amesema kuwa vijana 501 wameshindwa kuhitimu mafunzo hayo yaliyoanza rasmi Juni 21 mwaka huu kutokana na sababu mbambali ikiwemo kifo, masomo na utovu wa nidhamu.

"Kijana mmoja kwa bahati mbaya alifariki dunia kutokana na ugonjwa, mwingine aliomba mwenyewe ruhusa ya kwenda kusoma nje ya nchi na tulimruhusu lakini wengi wameshindwa kutokana na utovu wa nidhamu ikiwemo utoro" amesema Mabele

Amefafanua kuwa kati ya hao walioshindwa kuhitimu mafunzo vijana wa kiume ni 437 huku wa kike wakiwa ni 64 na kutumia muda huo kuwapongeza vijana wa kike kwa uvumulivu wao uliopelekea wachache kushindwa kuhitimu mafunzo.

Mabele amesema kuwa kumekuwepo na dhana kuwa JKT kuna mateso jambo amablo sio kweli kwani kila kinachofanyika jeshini na kwenye mafunzo kina maana yake hivyo kuoomba jamii kuondokana na dhana hiyo.

"JKT hakuna mateso na nyie ni mashahidi na ushahidi wenyewe ni namna ambavyo vijana wa kike wachache sana wameshindwa kuhitimu, ijulikane kuwa kila kinachofanyika jeshini kina maana yake mfano ukiambiwa kaa chini au jiviringishe kuna maana na ujue kuna kitu tunakitafuta na sio mateso" amesema Mabele

Amesema kuwa mafunzo hayo kwa vijana yanalega vitu vingi ikiwemo suala la malezi na nidhamu na kwamba hatarajii kusikia kuwa miongoni mwa vijana waliohitimu mafunzo hayo watakuwa ni waanzilishi wa migomo katika vyuo watakavyopangiwa kusoma hapo baadaye.

Hata hivyo amesema kuwa licha ya mafunzo hayo kuanza huku kukiwa na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 hakuna kijana aliyepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo na kuwataka wahitimu hao kuchukua tahadhari sambamba na kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo.


Amesema kuwa wapo watu katika jamii ambao bado wanapinga chanjo hiyo na kuwataka vijana hao kuamini kuwa chanjo ya uviko 19 ni sawa na chanjo nyinhine ambayo walichanjwa wakiwa wadogo na kusema kuwa chanjo hiyo haizuii kuugua bali uwezekano wa kufariki kutojana na ugonjwa unakuwaji mdogo sana.

Awali kaimu kamanda wa kikosi cha Jeshi 822 Rwamkoma, Memne Kinana alisema kuwa vijana 23 kati ya 1,070 waliojiunga na mafunzo hayo katika kikosi chake hawakuweza kuhitimu mafunzo.

Amesema kuwa kati ya hao kijana mmoja alifariki dunia kutokana na ugonjwa huku wengine wakishindwa kutokana na utoro pamoja na utovu wa nidhamu na kwamba wakati wa mafunzo hayo vijana hao wamejifunza mambo kadhaa ikiwemo kilimo, ujasiriamali na masuala ya ulinzi.