Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vijana 800 kusomeshwa Veta, wenye ulemavu wahimizwa kujitokeza

Mratibu wa mradi wa VEMA kutoka Plan International, Gadiely Kayanda (Aliyesimama) akiwasilisha namna mradi huo kwenye kipengele cha uwezeshaji kiuchumi kwa vijana utakavyotekelezwa wakati alipokutana na Maofisa Elimu wilaya ya Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza, Maofisa Maendeleo wa Kata, vijana waliounda vikundi, wadau wa maendeleo na wanafunzi. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

Hadi kufikia Novemba 9 mwaka huu, ni vikundi 42 vyenye vijana 700 pekee vilikuwa vimeanzishwa na kujisajili kwa ajili ya kunufaika na ufadhiri wa mradi huo wa VEMA ulioko chini ya Plan International.

Mwanza. Vijana 800 kutoka kata 13 za Wilaya ya Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza wanatarajia kunufaika na mradi wa Vijana Elimu Malezi na Ajira (VEMA) kwa kupatiwa mafunzo maalum katika Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (Veta) mkoani hapa ili kuwajengea uwezo wa kuzalisha na kujiajiri.

Taarifa hiyo imetolewa na Mratibu wa mradi wa VEMA kutoka Plan International, Gadiely Kayanda alipozungumza na Mwananchi ambapo amesema hadi kufikia Novemba 9 mwaka huu, vikundi 42 vyenye vijana 700 vilikuwa vimeanzishwa na kujisajili ili kunufaika na ufadhiri huo kati ya vikundi 50 vyenye vijana 800 vinavyolengwa.

Kayanda amesema pamoja na kuwa lengo la mafunzo hayo yatakayokuwa yakifanyika kwa miezi sita kuanzia Januari 2024, ni kuona angalau asilimia tano ya wanufaika ni watu wenye ulemavu lakini takwimu zinaonyesha kuna vijana nane pekee wenye ulemavu sawa na asilimia moja huku akihimiza wazazi na walezi kuwahimiza vijana wao wenye ulemavu kushiriki.

“Wilayani Ilemela kata zinazolengwa ni Kayenze, Sangabuye, Shibula, Bugogwa, Kahama, Buswelu na Nyamhongolo na wilaya ya Nyamagana kata zitakazonufaika Kishiri, Mahina, Mhandu, Buhongwa, Rwanima na Luchelele,”

“Tunatarajia vijana 800 kunufaika na mradi huo, tutawalipia ada ya Sh400,000 kila mmoja, kwa wanaoishi kata zilizoko mbali na ilipo Veta tutawatafutia mafundi wenye ujuzi husika ama kuanzisha vituo vya ufundi na tutawalipia ili wajengewe uwezo huo,” amesema

Akitoa vigezo vya kunufaika, Kayanda amesema mradi unafanya kazi na Maofisa Maendeleo wa Kata ambazo mradi unatekelezwa, vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wasiyo katika mfumo rasmi wa elimu na wanaoishi katika mazingira magumu wanatengeneza kikudi chenye watu kuanzia watano kisha kuingizwa kwenye mradi.

“Tutawawezesha kuunda vikundi vya hisa, mafunzo ya ujasiriamali, mafunzo ya usimamizi wa fedha, uendeshaji wa hisa na kukopa, stadi za maisha na usawa wa kijinsia. Vijana wengi wamemaliza shule na vyuo lakini kwa sababu hawana Hand on skills (Ujuzi) wa kuwawezesha kufanya shughuli za uzalishaji mali na kujiajiri ndiyo maana wanalalamika maisha magumu,”amesema Kayanda

Pia, amewahimiza vijana wa kike kuomba kunufaika na mafunzo hayo ambapo amedokeza kuwa katika vikundi ambavyo vimeshasajiliwa wanawake ni asilimia 51 pekee huku lengo likiwa ni angalau kuwa na wanufaika wa kike angalau asilimia 60 ili kuleta usawa wa kijinsia katika jamii.

Akizungumzia mradi huo, Ofisa Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Mkurugenzi Manispaa ya Ilemela, Sara Nthangu amesema iwapo walengwa watanufaika na mafunzo hayo, tatizo la ukosefu wa ajira katika wilaya hizo litapunguzwa.

“Kupitia vikundi watakavyounda utakuwa mwanzo mzuri wa kuweza kudhaminika kwa urahisi kwenye taasisi za kifedha na kukopesheka kwa sababu vikundi vyao vitakuwa vinatambulika na kuwa na usimamizi wa watalaam kama hawa wadau wa Plan International,”amesema

Mkazi wa Kishili wilayani Nyamagana, Veronica Msenyele (19) amesema baada ya kusitisha masomo ya Sekondari kutokana na ugumu wa maisha katika familia yake hatimaye anaamini mradi huo utatoa fursa kwake kutimiza ndoto yake ya kuwa msanifu majengo.

“Tupo vijana wengi ambao tulitamani kusoma na kutimiza ndoto zetu lakini kutokana na changamoto mbalimbali katika familia zetu ikiwemo ukata tumeshindwa kuzifikia. Naamini fursa hii itakuwa njia ya kufikia ndoto yangu tumeshasajili kikundi chetu ili kupata ufadhiri huu,” amesema Veronica.

Naye, Mkazi wa Bugogwa wilayani Ilemela mkoani hapa, Zacharia Paschal amewataka vijana hasa wa kike na wenye ulemavu kuchangamkia fursa hiyo aliyoitaja kuwa mwarobaini wa changamoto ya ajira kwa vijana waliokosa fursa ya kupata elimu katika mfumo rasmi.