Vijana ACT watoa mapendekezo sita minada ya korosho

Vijana ACT watoa mapendekezo sita minada ya korosho

Muktasari:

  • Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo imetoa mapendekezo sita kwa serikali ili kuwasaidia wakulima wa korosho kufaidika na zao hilo kwa msimu wa 2021/2022.

Dar es Salaam. Wakati wakulima wa zao la korosho wakiwa wanaendelea na minada ya uuzaji wa korosho, 2022 Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo imetoa mapendekezo sita kwa serikali ili kuwawezesha wakulima wafaidike na zao hilo kwa msimu wa 2021/2022.

Mapendekezo hayo ni pamoja na kutowalazimisha wanunuzi kutumia bandari ya Mtwara, Serikali kurejesha ruzuku ya kusafirisha korosho nje ya nchi, kupunguza tozo kwa wakulima na tozo za bandarini na kupitiwa upya kwa mfumo wa Stakabadhi ghalani. 

Katika msimu uliopita mwaka 2020/2021 bei ya juu ya korosho kwa wastani kilo iliuzwa ghalani kwa sh 2,700 hadi 3,500 tofauti na msimu huu, ambapo korosho zimeuzwa ghalani kwa bei ya Sh 2,445 hadi 2,400.

Akizungumza na wanahabari jana Oktoba 16 jijini hapa, Mwenyekiti wa Ngome hiyo Abdul Nondo amesema, bei ya zao hilo imeendelea kuporomoka kupitia minada ya mwanzo ambayo tayari imeshafanyika.

Amesema ili bei ya zao hilo iweze kupaa, Serikali inapaswa kutengua uamuzi wake ya kulazimisha, wanunuzi kusafirisha korosho kwa kutumia bandari ya Mtwara, kwani huongeza gharama kwa mnunuzi.

“Serikali irejeshe fedha za ushuru wa kusafirisha bidhaa nje (Export Levy) kwa wakulima ili zitumike kuendeleza zao hili, ambapo itaondoa utitiri wa tozo kwa mkulima na mnunuzi zinazojirudia,” amesema Nondo.

“Kama itakuwa ni vigumu kuzirejesha fedha hizo ili kusaidia kuendeleza zao hili, basi kodi ya ushuru wa kusafirisha bidhaa nje, iondolewe kwa miaka kadhaa ili kuondoa mzigo huo kwa mnunuzi ili bei kwa mkulima iwe nzuri,”alisema.

Aidha ushauri mwingine ni kuhusu tozo zinazotozwa kwa mkulima na mnunuzi, zirekebishwe kulingana na bei husika, kwani haiwezekani ikawa ileile kila msimu bila kuangalia bei iliyopo kwa mkulima.

“Kuhusu mfumo wa Stakabadhi Ghalani, tunashauri uangaliwe upya na kufanyiwa marekebisho ya msingi, hasa kupunguza mnyororo wa walaji kupitia zao la korosho na jasho la mkulima,” amesema.

Pia alibainisha kuwa lazima mfumo wa Stakabadhi Ghalani, lazima uende sambamba na bei elekezi ya serikali kuliko kumuacha mnunuzi kuja na bei yake katika sanduku linalobebwa na vyama vya ushirika.

“Ngome ya vijana tunashauri serikali iwe inadhibitisha tozo ambazo vyama vya ushirika vinatoza kwa wakulima ili kumlinda mkulima dhidi ya utitiri wa tozo,” amesema na kuongeza.