Vijana wapewa mbinu kufanikiwa sekta binafsi

Dodoma. Ukosefu wa vyanzo endelevu vya fedha, upungufu wa rasilimali watu na uwezo mdogo wa kitaalamu ni changamoto zinazotajwa kuzuia sekta binafsi kushiriki kikamilifu kuimarisha sera, ukosefu wa fursa za kilimo na ujasiriamali na kuua ubunifu kwa vijana nchini.

Aidha changamoto hizo zinachangia kushindwa kutoa usimamizi wa huduma muhimu na fursa kwa vijana ambazo zingewawezesha kuingia katika ujasirilimali na kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Changamoto hizo zimetajwa na Mkuu wa mradi wa Feed the Future wa Uimarishaji wa Sekta Binafsi nchini, Elibariki Shammy wakati akizungumza kwenye mkutano na wadau wa sekta binafsi na vijana kuhusu kilimo, biashara na uchumi.
 
Elibariki amesema mradi huo unalenga kuwezesha na kukuza fursa za kiuchumi kwa wajasiriamali vijana, kuboresha sekta ya Kilimo.
“Mradi huu utafanya kazi kwa karibu na Taasisi za vijana, sekta binafsi Serikali mifumo ya masoko hizi Teknolojia fursa vyama vya sekta binafsi kuwawezesha kutekeleza na kutoa huduma za kibiashara vyama vikuu vya Sekta binafsi Taasisi binafsi katika ngazi Mikoa na Wilaya”amesema Shammy.

Aidha Shammy amesema mradi huo unalenga kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kujenga fursa kwaajili ya vijana na kukuza ajenda za uchumi nchini.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya kilimo Dk Hussein Omar amesema mradi huo una nafasi kubwa ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuingiza vijana katika sekta za kiuchumi hususani kilimo.

“Rais amedhamiria kuimarisha maendeleo ya sekta binafsi nchini, Serikali imejipanga kikamilifu kufanya kazi na mradi wa Feed the future Tanzania ili kusaidia vijana katika sekta binafsi na kukuza uwekezaji ndani na nje ya Nchi”amesema Kiongozi huyo.

Dk Hussein amesema moja ya kazi ya Wizara ya kilimo ni kukifanya kilimo biashara na kushawishi vijana kujiunga na sekta hiyo ili kuwasaidia kukuza uwekezaji na uchumi wao kwa ujumla.