Vijiji vinne kunufaika mradi wa maji Musoma

Katikiro Jomba, mkazi wa kijiji cha Mmhare kata ya Etaro wilaya ya Musoma akichota maji kutoka kwenye moja ya vituo vya kusambaza maji baada ya kukamilila kwa mradi wa maji uliogharimu zaidi ya Sh1 bilioni. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Vijiji vinne katika kata ya Etaro wilayani Musoma Mkoa wa Mara vitanufaika na mradi wa maji wa zaidi ya Sh1 bilioni.

Musoma. Vijiji vinne katika kata ya Etaro wilayani Musoma Mkoa wa Mara vitanufaika na mradi wa maji wa zaidi ya Sh1 bilioni.

Mradi huo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakazi 10,000 wa vijiji vya Etaro, Busamba, Mmahare na Rukuba na utasaidia kuondoa adha ya kutembea zaidi ya kilomita 14 kufuata maji Ziwa Victoria.

Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) wa halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini, Edward Sironga amesema  baada ya kukamilika kwa mradi huo ofisi yake imeanza usanifu wa mradi mwingine katika kata ya Nyakatende.

"Tayari tumepokea Sh100 milioni kwa ajili ya mradi wa kata ya Nyakatende ambapo kijiji cha Kigeraetuma na Kakisheri vinakwenda kunufaika tukimaliza tutaomba tena fedha kwa ajili ya vijiji viwili vya kata hii ambavyo havipo kwenye awamu hii," amesema Sironga.

Wakizungumza mara baada ya kuzinduliwa kwa mardi huo baadhi ya wanufaika wameishukuru Serikali akisema mradi huo ni suluhisho la kudumu baada ya kuhangaika na shida ya maji kwa zaidi ya miaka 50

"Tulikuwa tunatembea zaidi ya kilomita 14 kufuata maji ziwani, maji ambayo pia sio salama lakini hatukuwa na namna, na hapa kijijini kwetu tunasumbuliwa na magonjwa hasa ya kuhara na kichocho kwa hiyo mradi huu mbali na kutuondolea shida ya maji lakini pia utaimarisha afya zetu," amesema Maria Domisiane mkazi wa Etaro

Naye Katikiro Jomba amesema kukamilika kwa mradi huo ni jitihada za mbunge wa jimbo hilo, Profesa Sospeter Muhongo ambaye baada ya kuchaguliwa alipokea ombi maalum kutoka kwa wazee wa kata hiyo kuelezea changamoto walizokuwa nazo likiwemo sula la ukosefu wa maji.