Viongozi wa Chadema waachiwa Mwanza

Saturday July 24 2021
Chadema pc

Mjumbe wa kamati kuu ya Chadema na mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, John Heche.

By Peter Saramba
By Mgongo Kaitira

Mwanza. Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanachama wote 15 waliokuwa wanashikiliwa na polisi wameachiwa kwa dhamana.

Ingawa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhanj Ng'anzi hajapatikana kuzungumzia dhamana za viongozi hao, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi ambaye ni miongoni mwa waliokuwa wanashikiliwa ameithibitishia Mwananchi kuachiwa kwao.

"Ni kweli tumeachiwa kwa dhamana yenye masharti tofauti; tumetawanyika kila mtu ameenda kwake. Mimi hivi sasa niko kwenye gari naenda nyumbani japo nioge kwanza ndipo mambo  mengine yafuate," alisema Obadi

Katika hatua nyingine, mjumbe wa kamati kuu ya Chadema na mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, John Heche ambaye pia alikuwa mikononi mwa polisi amelazwa hospitali baada ya kuugua ghafla akiwa kituo cha polisi usiku wa kuamkia jana.

"Kweli mdogo wangu John (John Heche) amelazwa hospitali baada ya kujisikia vibaya kiasi cha kushindwa kupumua vizuri akiwa mahabusu ya polisi usiku wa kuamkia leo," alisema Chacha Heche ambaye ni kaka yake John.

Alisema hali ya mdogo wake huyo ilikuwa haijatengamaa hadi kufikia jana jioni na madaktari walikuwa wakiendelea kumhudumia huku wakiendelea na uchunguzi wa kina kubaini kiini cha tatizo lake.

Advertisement
chadema 2

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Boniface Heche aliyejitambulisha kuwa ni mdogo wake John alisema kiongozi huyo wa Chadema hakuwa katika nafasi ya kuzungumza kwa sababu alikuwa kwenye chumba cha daktari katika moja ya hospitali binafsi jijini Mwanza (jina linahifadhiwa) akiendelea kuhudumiwa.

"Labda upige baada ya dakika 20 au nusu saa hivi; yuko kwenye chumba cha daktari hawezi kuzungumza," alisema Boniface ambaye ndiye anamuuguza kaka yake hospitalini

Advertisement