Viongozi wa dini, Serikali wawasili maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani
Mkuu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo pamoja na viongozi wengine wa dini wakiwa katika ukumbi wa Kuringe mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro wakimsubiri mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yanayofanyika Kitaifa Mkoani Kilimanjaro, Maadhimisho hayo yameandaliwa na Baraza la wanawake Chadema ( BAWACHA). Picha na Janeth Joseph
Moshi. Viongozi mbalimbali wa dini akiwemo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo pamoja na viongozi wengine wa dini tayari wamewasili katika viwanja Ukumbi wa Kuringe vilivyopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Kilimanjaro.
Katika maadhimisho hayo, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, akipokewa na wanawake Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha).
Viongozi wengine wa serikali waliwasili katika viwanja vya ukumbi huo, ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima pamoja na viongozi wengine wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Vifijo na nderemo vimetawala katika viwanja vya Ukumbi wa Kuringe vilivyopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro katika maadhimisho hayo ya Siku ya Wanawake Duniani.
Hata hivyo, mamia ya wanawake wa chama hicho kutoka bara na visiwani wamefurika ndani na nje ya ukumbi huo, wakimsubiri Rais, Samia.