Viongozi wa dini waeleza waliyozungumza na Dk Mwinyi

Muktasari:

  • Viongozi wa dini Zanzibar wamekutana na kuzungumza na Rais Hussein Mwinyi wakimpongeza kwa hatua anazochukua na kumshauri mambo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa visiwa hivyo.

Unguja. Viongozi wa dini Zanzibar wamekutana na kuzungumza na Rais Hussein Mwinyi wakimpongeza kwa hatua anazochukua na kumshauri mambo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa visiwa hivyo.

Viongozi hao wamekutana naye leo Jumatano Juni 9, 2021 Ikulu Vuga mjini Unguja, Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao hicho katibu wa Baraza la Maaskofu Zanzibar, Askofu Dickson Kaganga amesema mbali na kumpongeza rais kwa hatua za kiuchumi anazochukua,  wamemshauri kutengeneza mkakati mzuri na viongozi wa dini ili kusaidia katika mapambano hayo.

“Katika uongozi wake ameleta matumaini makubwa kwa wananchi bila kujali dini zao na hatua zinaonekana, tumekuja kumwambia wakati mwingine matumaini yanakuwa mbele kwa hiyo wajitahidi ili matumaini ya wananchi waliyonayo yaweze kufikiwa zaidi.”

“Ushauri tuliompa ni kuhusu uchumi wa bluu elimu itolewe ili wengi waweze kuielewa, aweze kutengeneza mkakati na viongozi wa dini ili na sisi tuweze kwenda sambamba na hilo,” amesema.

Amesema wamemuomba atengeneze utamaduni wa uongozi kuanzia ngazi za juu hadi chini ili wote waimbe wimbo mmoja, “ sisi viongozi wa dini tunaunga mkono jitihada za kisiasa, kiuchumi na kuleta maendeleo.”

Amesema Zanzibar imepitia kwenye siasa za vurugu na mgawanyiko akidai huenda kuna watu zilikuwa zinawapa maslahi hivyo wasingetamani warudi katika hali hiyo.

“Wapo watu wangetamani turudi tulipotoka, sisi tunawataka waumini na wakazi wote wa Zanzibar tumuunge mkono rais katika hatua anazochukua za kuunganisha wananchi wote mahali ambapo hakuna amani maendeleo hayawezi kupatikana,” amesema.

Mjumbe wa Baraza la Maaskofu Zanzibar, Damas Foi amesema wamemweleza ukweli Rais Mwinyi na kumuomba awe anatembelea makanisa na kuzungumza na waumini kama anavyofanya kila Ijumaa kwenye misikiti jambo ambalo amedai amekubali.

Naye katibu wa Mufti Zanzibar, Mfaume Ali Mfaume amesema viongozi wa dini wana jukumu la kusimamia amani, utulivu, mshikamano, umoja na ushirikiano hivyo wameona wasibaki nyuma waende kumuona na kumueleza wanayoona yanafaa.

“Kwa sura ambayo naiona sasa kwa mazingira ya nchi yetu ilivyo tuna amani na utulivu wa kutosha na hatua anazochukua na tupo wamoja, kwa sasa kilichobaki ni maendeleo,” amesema.