Viongozi wa dini watakiwa kuelimisha jamii chanjo ya Uviko-19

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai

Muktasari:

Viongozi wa dini mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuisaidia Serikali kuhamasisha wananchi kujitokeza kupata chanjo ya Uviko-19.

Moshi. Viongozi wa dini mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuisaidia Serikali kuhamasisha wananchi kujitokeza kupata chanjo ya Uviko-19.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai leo Jumanne Januari 18, 2022 wakati akifungua semina ya kushirikisha viongozi dini kuhamasisha mbinu za kujikinga na Uviko-19, iliyofanyika katika ukumbi wa Uhuru Hotel mjini Moshi.

Kagaigai amesema viongozi wa dini wana kundi kubwa la watu nyuma yao, hivyo wakishirikiana kwa karibu na Serikali kuhamasisha wananchi kupata chanjo ya Uviko-19 watawezesha Watanzania wengi kujitokeza.

"Tunatambua ninyi viongozi wa dini mna kundi kubwa la watu, sasa tunaomba mtusaidie kutoa elimu na kuhimiza wananchi kujitokeza kupata chanjo ya Uviko-19 " ameesema Kagaigai.

Baadhi ya viongozi wa dini walioshiriki semina hiyo wamesema uelewa duni na kauli za upotoshaji zilizotolewa na baadhi ya watu wanaoaminika nchini kumechangia kwa kiasi kikubwa watu kuwa na hofu ya kuchanja chganjo hiyo.

Sheikhe wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaaban Mlewa amesema watu wengi ambao hawajanja ni kwa sababu ya hofu waliojengewa awali na watu wanaowaamini juu ya chanjo hizo na kueleza kuwa bado inahitajika nguvu kubwa katika kuhamasisha na kuwapa elimu wananchi.

"Watu wengi ambao hawajachanja wamejawa na hofu, wanaamini kauli za upotoshaji zilizotolewa awali kuwa chanjo ina madhara, sasa viongozi wa dini kwa kushirikiana na serikali tuna kazi kubwa ya kuhamasisha wananchi ili kuwaondolea ile hofu"

Naye Naibu waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amewataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha kila wanapokwenda mitaani kutoa elimu ya chanjo hiyo, kuhakikisha wanaambatana na wakuu wa mikoa, wilaya, wabunge na madiwani ambao ndio wenye watu katika jamii.