Viongozi wa vyama vya ushirika waaswa kutafuta mafunzo
Muktasari:
- Viongozi wapya wa vyama vya msingi wanaochaguliwa wametakiwa kuhakikisha wanapata mafunzo ya namna ya kuviendesha vyama vyao ili waviongoze kwa ufanisi.
Tabora. Viongozi wapya wa vyama vya msingi wanaochaguliwa wametakiwa kuhakikisha wanapata mafunzo ya namna ya kuviendesha vyama vyao ili waviongoze kwa ufanisi.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama, (Kacu), Emmanuel Charahani amesema kama vyama viongozi wake hawapati mafunzo watajikuta wanashindwa kuviendesha inavyotakiwa na kujikuta wanakwama.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa tatu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Milambo ambacho kitachagua viongozi wake wapya wa bodi, amebainisha kwamba mafunzo ndio silaha yao kubwa kuviendesha kwa ufanisi.
"Kila bodi mpya inapochaguliwa ihakikishe wanapata mafunzo haraka iwezekanavyo vinginevyo watashindwa kuviendesha kwa ufanisi," amesema.
Chama kikuu cha Ushirika cha Milambo kitafanya uchaguzi wa viongozi wake wa bodi baada ya waliokuwepo kuondolewa madarakani na Msajili kutokana na kukumbwa na kashfa ya pembejeo na Mali za chama kuhujumiwa.
Mkuu wa wilaya ya Kaliua, Abel Busalama aliyefungua mkutano huo kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Philemon Sengati amewataka wajumbe kuchagua viongozi waadilifu na wachapakazi watakaokipeleka mbele chama chao.
Amesisitiza wasichaguliwe viongozi wenye tamaa kwani watakirudisha nyuma chao na hivyo wanachama kukosa imani nacho.