Viongozi wa vyama vya ushirika watakiwa kuacha ubadhirifu

Muktasari:

  • Viongozi wa vyama vya Ushirika Mkoa wa Arusha wametakiwa kuacha vitendo vya ubadhirifu wa fedha  na badala yake  kujiimarisha kimaadili hali itakayosaidia kuepusha migogoro inayosababisha vyama hivyo kuvunjika.

Viongozi wa vyama vya Ushirika Mkoa wa Arusha wametakiwa kuacha vitendo vya ubadhirifu wa fedha  na badala yake  kujiimarisha kimaadili hali itakayosaidia kuepusha migogoro inayosababisha vyama hivyo kuvunjika.

Hayo yalibainishwa katika jukwaa la vyama vya ushirika linalofanyika mkoani humo kwa kuvikutanisha  vyama mbalimbali vya mkoani hapa.

Akibainisha tabia za ufujaji zinazofanywa na baadhi ya viongozi Mrajisi Msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani humo, Grace Masambaji amesema miongoni mwa viongozi wa vyama hivyo wamekuwa si waaminifu kwa kutumia fedha kwa matumizi yasiyostahili .

"Kama serikali tumekuwa tukijitahidi kupambana na viongozi wa namna hiyo na mpaka sasa kuna viongozi ambao wameshawajibishwa na kesi zao zinaendelea mahakamani na tumejipanga kuimarisha usimamizi katika vyama vya ushirika "amesema

Ameeleza kuwa kodi kubwa ni jambo linalotajwa kudidimiza vyama na ucheleshwaji wa mikopo kwa wanachama.

"Vyama hivi bado vinahudumua wananchi wa hali za chini hakuna unafuu kwani kodi ni kubwa hivyo tunaomba kodi hii ishuke kutoka 30% ya sasa ya mapato hadi 10% Serikali iangalie hivi vyama kwa kusamehe adhabu na riba zifutwe kwakuwa ni kubwa sana "amesema  

Nao baadhi ya washiriki wa jukwa hilo, Gospel Massawe na Pascalina Shayo wameeleza namna ambavyo wanapata wakati mguu pindi waliochukua mkopo kushindwa kurudisha kwa wakati.

Naye Katibu Tawala Wilaya ya Arumeru, James Mchembe ametoa wito kwa viongozi hao kufanya kazi kwa nidhamu ili kutimiza lengo la muunganiko wa vyama hivyo ikiwemo kujikomboa katika umaskini.