Vipaumbele Wizara ya Mifugo na Uvuvi 2023/2024
Muktasari:
- Wizara ya Mifugo na Uvivu imeliomba Bunge la Tanzania kuidhinisha kiasi cha Sh296 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele takribani 18 vya sekta ya mifugo na uvuvi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameliomba Bunge kuidhinishia Sh296 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele takribani 18 vya sekta ya uvuvi na mifugo kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Sh296 bilioni ni ongezeko ambalo katika bajeti ya mwaka 2022/23 wizara hiyo iliidhinishiwa Sh268.85 bilioni, ikilinganishwa na Sh168.2 bilioni kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Ulega ameeleza hayo leo Jumanne Mei 2, 2023 wakati akiwasilisha hotuba ya makaridio ya bajeti ya wizara yenye vipaumbele takribani 18 ikiwemo kuongeza malisho (majani) ya mifugo yatakayohudumia soko la ndani na nje ya nchi.
Kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora za mifugo ili kuboresha mbari za mifugo, kuimarisha afya ya mifugo, kuboresha huduma za ugani, kuanzisha na kuendeleza vituo matumizi vya uwekezaji vya vijana, kuimarisha huduma za utafiti na mafunzo ya taaluma za mifugo.
Vipaumbele vingine katika sekta ya mifugo ni pamoja kuwezesha uongezaji thamani na biashara ya mifugo na mazao yake, kuimarisha Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco) kuanzisha mamlaka ya kusimamia miundombinu ya mifugo kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli katika sekta ya hiyo.
“Katika kutekeleza vipaumbele hivi baadhi ya kazi zitakazofanyika ni pamoja na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake ili kuimarisha upatikanaji wa malighafi za viwanda vya mazao ya mifugo. Tutajenga skimu za unenepeshaji katika mashamba ya Narco ili kutoa fursa kwa vijana na kina mama kushiriki.
“Tutaanzisha vituo vipya vya uwekezaji vya vijana na kuendeleza vituo vingine vilivyoanzishwa, pia tutahimilisha ng’ombe 100,000, sambamba na kununua madume bora na kuyagawa kwenye vikundi vya wafugaji,” amesema Ulega.
Mbali na hilo, Ulega ambaye ni mbunge wa Mkuranga mkoani Pwani, amewaomba wabunge kuunga mkono hatua ya wizara hiyo ya kutaka kuendesha mchakato wa kupeleka mizani katika minada ya awali na kuacha biashara ya kuuza ng’ombe kwa makisio.
“Tunataka biashara ya kuuza ng’ombe kwa makisio iwe mwisho. Ng’ombe wote wauzwe kwa kilo kama ambavyo nyama inavyouzwa katika mabucha na sio makisio, jambo hili litawaheshimisha wafugaji wetu nchini,” amesemaa Ulega.
Vipaumbele vya sekta ya uvuvi
Akitaja vipaumbele vya sekta ya uvuvi, Ulega amesema Wizara inatarajia kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi ambayo kazi yake mahususi itakuwa ni kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza rasilimali za uvuvi.
Amesema mamlaka hiyo ni sehemu ya utekelezaji vipaumbele vinavyoendana na kufungamanisha Uchumi wa Buluu hususan matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi ikiwemo uvuvi wa asili na ukuzaji viumbe maji.
“Ushauri wa kuanzishwa kwa chombo hiki ulianzia hapa bungeni na Serikali imeona kuna mantiki na faida kubwa kwenye kuanzisha chombo hiki. Chombo hiki kinakwenda kusimamia maelekezo hayo,” amesema.
Amesema Wizara itajielekeza kuimarisha uwezo wa uvuvi katika bahari kuu, kuimarisha taasisi za Uvuvi ili kuongeza ushiriki katika uchumi wa buluu.
Ametaja mengine kuwa ni kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji, kuimarisha uthibiti wa ubora wa mazao ya uvuvi na masoko na kuimarisha huduma za ugani wa uvuvi na ukuzaji viumbe maji.
Ulega amesema ili kuimarisha uwezo wa uvuvi katika bahari kuu na taasisi za uvuvi Wizara imekusudia kununua meli za kuvua kwenye kina kirefu.
“Wizara kupitia programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi kwa ufadhili wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), inaendelea na taratibu za ununuzi wa meli tatu za uvuvi wa bahari kuu zenye vifaa vya kisasa kwa ajili ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).
“Hadi sasa, msawazo (Specifications) kwa ajili ya ununuzi wa meli hizo, upembuzi yakinifu wa awali (Pre-feasibility Study) na andiko dhana umekamilika na kuwasilishwa kwenye mamlaka husika,” amesema Ulega.
Pamoja na hayo Ulega pia amesema mojawapo ya kipaumbele ni kuimarisha taasisi za uvuvi kwa kujenga miundombinu muhimu ikiwemo kununua boti mbili zenye vioo chini (glass bottom boat) ili kuongeza utalii kwenye hifadhi za bahari na maeneoTengefu.
Ulega amesema boti hizo pia zitatumika kufanya tafiti za kujua wingi, aina na mtawanyiko wa samaki katika maziwa ‘Victoria, Tanganyika, Natron na Eyasi). bahari ya hindi na bwawa la nyumba ya mungu; kujenga vyumba vitano vya mihadhara na vifaa vyakufundishia katika kampasi tano za FETA.
Katika uendelezaji wa bandari, Ulega amesema mwaka wa fedha 2023/2024, sekta ya uvuvi itaendelea na ujenzi wa bandari ya uvuvi katika eneo la Kilwa Masoko, mkoani Lindi.
Pamoja na hayo Ulega amesema watakamilisha ujenzi wa mialo minne ya Igabiro (Bukoba), Chifunfu (Sengerema), Igombe (Ilemela) na Kayenze (Ilemela) pamoja na vituo vitatu vya usimamizi wa rasilimali za uvuvi vya Sota (Rorya), Simiyu (Busega) na Nyakaliro (Sengerema).
Aidha, amesema Serikali itafanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa soko la samaki Kigamboni na maeneo nane ya ujenzi wa miundombinu ya Ofisi za Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (Kigoma, Tanga, Mtwara, Muleba, Kagera, Mtera, Ikola, na Singida).