Vishoka wakithiri ofisi za umma

Muktasari:

  • Ni katika ofisi zinazotoa huduma kwa kwa wananchi, urasimu, rushwa na uzembe vyatajwa kustawisha hali hiyo.

Dar es Salaam. Saa 6:15 asubuhi naingia ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuomba leseni ya udereva.

Lengo la safari yangu si tu kufika TRA, bali pia ofisi za Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi pamoja na Uhamiaji kufuatilia taarifa za uwepo wa vishoka ambao wapo kwa kivuli cha kutoa msaada kwa wanaohitaji huduma, huku wakisababisha usumbufu na wakati mwingne kuhusishwa na utapeli.

Katika ofisi hiyo ya TRA eneo la Posta, Dar es Salaam nilipokewa na watumishi wakionyesha shauku ya kunisikiliza.

Baada ya salamu waliniuliza nahitaji nini, nikawaambia shida yangu ni kupata leseni kuendesha ya gari.

Waliniuliza kama nafahamu utaratibu, nilijibu hapana, nikawaomba wanielekeze kwa kuwa mara yangu ya kwanza kufika kwenye hapo.

Mmoja wa watumishi hao, aliniambia zipo njia mbili naweza kupata huduma, ya kwanza ni njia ndefu na ya pili fupi.

Niliwaomba ufafanuzi wa njia hizo, nao wakaniitia mtumishi mwingine kutoka ndani ya ofisi hizo, ambaye waliniambia ndiye mhusika, nimweleze atanisikiliza na kunisaidia.

“Karibu kaka”, nilimjibu asante. “Unahitaji leseni daraja gani?” Nahitaji daraja D.

Aliniuliza kama ningehitaji daraja la juu zaidi, nami niliitikia ‘ndiyo’, huku nikiuliza endapo hilo linawezekana ikiwa kiwango nilichosomea ni daraja D.

Alinihakikishia kwamba ninaweza kupata daraja la juu zaidi kama nitakuwa na kiwango cha fedha watakachokitihaji.

Baada ya maongezi aliniuliza kama nahitaji njia ndefu yenye mlolongo mrefu, akisema itanitaka nipeleke vyeti, kwenda polisi na kusubiri siku saba ndipo nipate leseni.

Aliniambia nitapaswa kulipia Sh70,000 (kihalali) kwa leseni itakayodumu miaka mitano, lakini kama nitahitaji kwa muda mfupi niongeze fedha.

“Kwa njia hii kinachohitajika ni TIN namba na daraja unalotaka, ukiniachia Sh120,000 kwangu utakuja kuchukua leseni tu ndani ya siku moja wala husumbuki,” anaeleza.

Utaratibu huu si wa kwangu tu, hata Beatrice Joseph, mkazi w Tabata Segerea anasimulia kwamba, leseni aliyonayo aliipata bila kufika TRA bali aliletewa ofisini.

“Nilimpatia mtu Sh150,000 akaniletea leseni nikiwa ofisini, watu wameshafanya hii ndio ajira na wanasomesha na kulisha familia kupitia kazi hii,” anaeleza.

Wakati hayo yakifanyika, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo anasema hilo ni kosa.

Alisema, endapo mtumishi huyo akithibitika, hasa kushirikiana na vishoka, hatua kali huchukuliwa na mamlaka hiyo.

Kayombo alisema njia wanazotumia kuhakikisha wananchi hawaingii kwenye mikono ya vishoka, ni kuwaelimisha kuhusu utaratibu ambao TRA inautumia kuwafikia wateja.

Njia hizo ni kupitia barua au maofisa kuwatembelea wafanyabiashara wakiwa wamevalia vitambulisho vya mamlaka hiyo.

“Tunawapa uwezo wa kudhibitisha kama wana wasiwasi kuhusu mtu ambaye anaweza kuwa kishoka, lakini tunapowakamata (vishoka) tunawatangaza ili wafahamike na hatua za kisheria huchukuliwa,” anasema.

Vilevile, alisema kwa sasa huduma nyingi za TRA zinapatikana kwa njia ya mtandao, kama TIN, ritani na uwasilishaji wa nyaraka za forodha na hivyo mfumo wa watu kuonana umepungua.

Anaonya kwamba TRA haina utaratibu wa kuwatumia wito wateja wake kupitia ujumbe wa simu na kuwa wanaofanya hivyo ni vishoka.


Wizara ya Ardhi

Baada ya TRA nilifunga safari kwenda ofisi za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi eneo la Kivukoni, kwa malengo yaleyale, hapa nikihataji kufanya uchunguzi wa uhalali wa eneo ninalotaka kununua ‘official search’ na niliambiwa niwasilishe nyaraka zinazohusu eneo hilo na nikapewa utaratibu wa kulipia.

Niliambiwa baada ya kulipia Sh40,000 ningepaswa kusubiri kwa siku saba ndipo nikachukue majibu.

Wakati ninaondoka alinifuata mwanamume mmoja ndani ya ofisi hizo na kuniuliza kama nataka jambo langu likamilike ndani ya muda mfupi, nilipomwambia hata ingewezekana niondoke na majibu yangu, alinipa njia mbadala.

Aliniuliza kama nina Sh30,000, nikamuomba apunguze lakini akasema hatumii fedha hizo peke yake, akasisitiza kama nataka uharaka nihakikishe nampatia kiasi hicho kwa kuwa sikuwa na kiwango hicho tulishindwana.

Hata hivyo, ofisi hiyo zimeweka utaratibu wa kudhibiti hali hiyo ingawa bado vitendo hivyo havijakomeshwa.

Ofisa Mawasiliano Serikialini Wizara ya Ardhi, Anthony Ishengoma alisema si lazima wananchi kufika kwenye ofisi za wizara hiyo, badala yake watumie mifumo ya Tehama kupata huduma.

Anasema mwananchi anapofika kwenye ofisi na kuanzisha mazungumzo na watu wasio watumishi wa wizara, ndipo huangukia mikononi mwa wezi na kutapeliwa.


Uhamiaji

Uhamiaji nako si salama kwa vitendo hivyo, Japhet Jamal, mkazi wa Mwenge, Dar es Salaam anasimulia mkasa uliomkuta wakati anataka kuhuisha pasipoti yak.

Alisema baada ya kukamilisha taratibu zote akisubiri kulipia hati yake, siku iliyofuata alitumiwa namba ya malipo akielekezwa afanye malipo kwa ajili aliyoelekezwa au ikishindikana atumie namba ya simu.

Anasema baada ya kuchunguza namba hizo (control number)ndipo akagundua ulikuwa mtego wa kitapeli.

“Kilichonishangaza ni kuwa hao watu wamejuaje kwamba nimeomba pasipoti na nimefikia hatua ya kupia na namba yangu wamepata wapi,” alihoji.

Ombeni Jackson, mkazi wa Mbagala alisema “kikubwa ufanisi katika utendaji ni mdogo, ndiyo maana kishoka anachukua hela anakwenda kugawana nao, kazi inafanyika kwa haraka,” alisema

Alishauri watendaji ndani ya ofisi za umma waongeze ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

Licha ya madai hayo, Msemaji wa Jeshi la Uhamiaji, Mrakibu wa Uhamiaji Paul Mselle alisema kwa sasa si rahisi vishoka kufika katika ofisi hizo.

Kama ilivyo kwa TRA na Aridhi, msemaji huyo wa Uhamiaji naye alisema wanatumia mifumo ya tehama kutoa huduma na mwombaji pekee ndiye anayewasilisha maombi yake kwenye mamlaka hiyo.

“Kishoka hawezi kuingia na kuwasilisha maombi ya mtu hapa, unakuta wakati mwingine ufahamu wa kutumia mifumo yetu kupata huduma bado, huyo anaenda stationery (duka la vifaa na huduma za kiofisi) ili mtu amjazie, hao wanaweza kumdanganya…lakini kishoka hawezi kufika mbele yetu,” anaeleza.

Mselle alisema mara nyingi vishoka wanaowatapeli wananchi huwa wapo nje na huwalaghai watu kuwa wana uwezo wa kuwsaidia kupata huduma kwa haraka.


Rushwa, urasimu vyatajwa

Kuibuka kwa vishoka katika ofisi za umma kunaelezwa na Profesa Aldin Mutembei, wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuwa msingi wake mkubwa ni rushwa.

“Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema Tanzania rushwa inanuka. Ofisa ndani ya mamlaka anakula rushwa lakini ili asishikwe anamtumia mtu mwingine (kishoka), wanapata fedha wanagawana,” anasema.

Anasema kutokana na rushwa mtu wa kati anaweza kutoa huduma haraka kuliko mtu wa mwazo ambaye ndiye mwenye wajibu huo.

Jambo la pili analotaja Profesa Mutembei ni urasimu, akifafanua kuwa mtu anapokwenda kwa afisa anayehusika hucheleweshwa kutokana na ofisa huyo kuwa na kazi anayoifanya, lakini anapotokea mtu wa kati na kumpatia chochote, huifanya kazi hiyo kwa haraka.

“Watu hawafanyi kazi kwa sababu kuna mambo mengine wanayafanya,” alisema.

Anapokuja mtu anakupa hela kidogo hiyo ndio unaipa kipaumbele unaifanya kazi haraka unamaliza, kwa njia hiyo huwezi kuondoa vishoka,’’anasema.

Kauli ya Profesa Mutembei kuhusu urasimu, inaungwa mkono na Greyson Mgonja, wakili katika kampuni ya Trasis Attorney, analiyesema tatizo hilo ndilo linasababisha wananchi kuwakimbilia vishoka kwenye ofisi za umma.

“Huduma ya siku moja unachukua siku tatu, mfano kuna huduma tunaenda kuwasaidia wateja kusajili inachukua siku tatu hadi nne, lakini ukimtumia kishoka unampa hela kidogo anakwenda anakamilisha jambo lako ndani ya muda mfupi,” alisema.

Watanzania wengi hatupendi usumbufu tunaofanyiwa kwenye ofisi za serikali, kwa hiyo utendaji mdogo ndani ya ofisi hizo zinachangia watu kuwakimbilia vishoka, ”anasema.

Mgonja anashauri huduma zinazotolewa na serikali ziboreshwe zaidi ili kila mtu ahudumiwe ndani ya muda mfupi.

Kauli ya uwepo wa urasimu kwenye taasisi za uma inaungwa mkono na Mkurugenzi Mstaafu wa Misitu na Nyuki Dk Felician Kilahama.

“Unaingia kwenye ofisi unapokelewa na kuhudumiwa ni tofauti na matarajio yako, lakini unaambiwa ukitaka mambo yaende mtumie fulani, huyo unayemtumia atahitaji malipo kama ilivyo kwa dalali,” alisema.