Vodacom ilivyojikita matumizi ya teknolojia sekta ya kilimo

Thursday August 04 2022
Vodacom PIC

Edgar Mboki - Project Manager of Agriculture kutoka Vodacom akichangia mada wakati wa kongamano la kilimo kwenye ukumbi wa Tari, Jijini Mbeya ambako yanafanyika maonyesho ya sherehe za wakulima ya Nanenane.

By Tumaini Msowoya

Mbeya. Meneja Miradi ya Kilimo wa Vodacom Tanzania, Edga Mboki amesema kwa sababu wanatambua mchango wa sekta ya kilimo kwenye ukuaji wa pato la Taifa, wameamua kujikita kwenye matumizi ya teknolojia.

Amesema ili kufikia ajenda ya 10/30, lazima wakulima walime kidigitali ikiwamo suala zima la utafutaji wa masoko.

Mboki amesema hayo leo Alhamisi Agosti 4, 2022 wakati akizungumza kwenye Kongamano la Shamba Darasa linanaloendeshwa na Mwananchi Communications Ltd (MCL) katika ukumbi wa Tari, Jijini Mbeya ambako yanafanyika maonyesho ya sherehe za wakulima ya Nanenane.

Amesema Vodacom inathamini sekta ya kilimo ikiamini teknolojia ni njia muhimu itakayoweza kuwasaidia wakulima kufikia malengo ya kuzalisha kibiashara.

“Tunajua sekta ya kilimo inagusa maisha ya kila Mtanzania na tunayo nia ya kumpeleka Mtanzania kwenye matumizi ya teknolojia, kilimo kidigitali kinaweza kurahisisha sekta ya kilimo mpaka kwenye masoko,” amesema.

Mboki amefafanua kilimo cha kidigitali pia kinaweza kuwa mwarobaini kwenye mabadiliko ya tabia nchi kwa wakulima kupata taarifa sahihi za hali ya hewa na mabadiliko hayo.

Advertisement

Alisema sio tu kwamba kilimo kinachangia pato la Taifa lakini pia ni fursa ya ajira kwa makundi yote wakiwemo vijana.

“Sisi kama Vodacom tuliona kuna haja ya kutumia utaalamu wetu wa teknolojia kwenye sekta hii ya kilimo na tumeweza kuwafikia wakulima wengi wanaotumia mtandao wetu,” amesisitiza kiongozi huyo wa Vodacom.


Advertisement