Vodacom yatangaza mwaka wa faida na gawio

Muktasari:

  • Baada ya kupata hasara kwa mwaka uliopita, kampuni ya Vodacom imesema itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inapata faida na inatoa gawio kwa wanahisa katika mwaka huu wa fedha.


Dar es Salaam. Baada ya kupata hasara kwa mwaka uliopita, kampuni ya Vodacom imesema itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inapata faida na inatoa gawio kwa wanahisa katika mwaka huu wa fedha.

Katika mwaka wa fedha uliopita uliopita Vodacom ilipata hasara ya zaidi ya Sh30 bilioni hali ambayo imesababisha wanahisa wake wasipate gawio katika mwaka husika.

Akizungumza leo Oktoba 15, 2021 katika mkutano wa wanahisa jijini hapa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Vodacom Jaji mstaafu Thomas Mihayo, amesema watafanya kila wawezalo.

"Tutafanya kila linalowezekana chini ya Sheria ili mwaka huu watu gawio, hatuwezi kusema lazima kwa kuwa hatujui ya mbeleni lakini tumeanza kuona ishara ya matumaini. Mtu kama alikuwa anatumia mashine mbili za kupumulia moja ikiondolewa unashukuru," amesema Jaji Mihayo.



Amesema suala la kutoa gawio kwa kampuni ambayo imeorodheshwa katika soko la hisa ni kipaumbele, lakini katika mwaka husika Vodacom ilikwamishwa na utaratibu wa Serikali wa kusajili laini kwa alama za vidole ambao ulipunguza wateja milioni 2.9 na kwa upande mwingine mlipuko wa Uviko-19.

"Uamzi wa kutotoa gawio ni mzito ambao unamuuma kila mtu ukifikiwa watu hawalali kwakuwa ni kinyime na matarajio ya wanahisa lakini wameridhia katika mkutano mkuu kwakuwa imefanyika hivyo ili kampuni iendelee kustawi," amesema.

Aidha amesema wanahisa wameafiki agenda zote za mkutano mkuu ikiwepo ya kumwajiri Mkurugenzi Mtendaji Mpya, kuwaongezea muda baadhi ya watendaji na taarifa ya mwaka wa fedha uliopita na wamekubaliana kuwa ifikapo Novemba wataangalia mwenendo wa biashara ya kampuni hiyo na kuwataarifu wana hisa.

Kuhusu tozo mpya zilizoanzishwa na Serikali katika mwaka huu wa fedha amesema zimetikisa biashara, kwani watu wengi wamepunguza kutuma fedha kwa njia ya mtandao na badala yake wanatumia njia mbadala.

"Kusema kweli tozo zimeathiri biashara baadhi ya watu wameacha wameacha kutuma fedha kwa njia ya mtandao nikiwemo mimi mwenyewe lakini tunashukuru baada ya Serikali kuingilia kati na kupunguza viwango kama yanakwenda vizuri," amesema Jaji Mihayo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo ambaye atamaliza muda wake mwishoni mwa mwezi huu, Hisham Hendi amewashukuru watu wote aliofanya nao kazi katika kipindi chake na kuwatakia kila la kheri akisema leo ndiyo ulikuwa mkutano wake wa mwisho na wanahisa pamoja na waandishi wa habari.