Vurugu CUF zachukua sura mpya

Muktasari:

  •  Wakati Mwenyekiti wa Kamati tendaji ya Wilaya ya Kinondoni wa CUF, Rajabu Salim akisema kada mmoja wa chama hicho amejeruhiwa katika vurugu zilizotokea jana wilayani hapo, chama hicho sasa kimekusudia kulifikisha suala hilo kwenye ngazi za kisheria.

  

Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Kamati tendaji ya Wilaya ya Kinondoni wa CUF, Rajabu Salim akisema kada mmoja wa chama hicho amejeruhiwa katika vurugu zilizotokea jana wilayani hapo, chama hicho sasa kimekusudia kulifikisha suala hilo kwenye ngazi za kisheria.

Vurugu hizo zilijitokeza kwenye ofisi hiyo jana baada ya wajumbe waliosimamishwa kwa madai ya utovu wa nidhamu, kugombea ofisi na wajumbe wapya kugombea kutumia Ofisi hiyo kati ya wajumbe wapya walioteuliwa na uongozi wa chama.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Desemba 17, Salim amemtaka kada aliyejeruhiwa kuwa ni Mwinyi Bakari kwa kuchanwa nyembe kiasi cha kumsababishia maumivu makali kufuatia vurugu zilizojitokeza kwenye Ofisi hizo.

Salim amesema kutokana na tukio hilo wamechukua hatua ya kwenda kuripoti kama ilivyo desturi na kwamba hatua kama hizo walianza kuzichukua kabla, baada ya kuona dalili za kundi hilo kuonesha viashiria vya vurugu.

Hata hivyo Kamanda wa jeshi la Polisi Kinondoni, Ramadhan Kingai alisema Bado hajapata taarifa ya tukio hilo na kwamba anafuatilia kujua kilichotokea na kuwakamata walishiriki kuleta vurugu hizo.

“Bado sijapata taarifa ngoja nifuatilie kujua kilichotokea ili tuweze kuwachukulia hatua wale wote walioleta vurugu," amesema Kamanda Kingai.

Kwa upande wake Bakari anayedaiwa kujeruhiwa amesema wanachama hao walikusudia kufanya mkutano kwenye Ofisi hiyo lakini hawakufuata utaratibu na alipowakataza walimjia juu kwa kudai wao bado ni wajumbe hali.

"Kwakuwa mimi ni mkuu wa itifaki na udhibiti wa chama niliwaambia waondoe hilo jambo ndipo walipoanza kunivamia kwa kunivaa maungoni kwakuwa wao walikuwa wengine walinivuta vuta hadi uchochoroni hadi nje wakiwa wananipiga," amesema.

"Baada ya kuona ugomvi unaendelea na hadi nje nikaanza kukimbia baada ya kuangalia mwili wangu damu zinatoka baadae nikaenda kuripoti Polisi kituo kidogo kilichopo jirani hapa nikapewa PF3 nikaenda hospitali," amesema Bakari wakati anaongeza na gazeti hili.

Akizungumzia vurugu hizo, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano kwa Umma wa chama hicho, Mohamed Ngulangwa amesema vikao vya chama vitakaa kuwajadili wanachama wote walioleta vurugu hizo na kuwapa adhabu inayostahili.

“Chama chetu ni taasisi na tumejiwekea utaratibu kwa kile kilichotokea Jana hatuwezi kuitisha kikao kuongelea isipokuwa tutafanya vikao kwa mujibu wa Katibu na kuwapa adhabu kukomesha tabia hizi,” amesema Ngulangwa.