Vyama vya Wakulima Tanga kuwasilisha mkakati kuzalisha mkonge tani 70,000

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima ametoa wiki mbili kwa Vyama vya Msingi vya Wakulima wa Mkonge (Amcos) kuja na mpango mkakati unaonyesha namna ya kufikia lengo la kimkoa la uzalishaji wa zao hilo la tani 70,000 Kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.


Tanga. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima ametoa wiki mbili kwa Vyama vya Msingi vya Wakulima wa Mkonge (Amcos) kuja na mpango mkakati unaonyesha namna ya kufikia lengo la kimkoa la uzalishaji wa zao hilo la tani 70,000 Kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

Ameyasema hayo  wakati wa ufunguzi wa jukwaa la nne la wadau wa maendeleo ya ushirika Mkoa wa Tanga ambapo amesema kuwa lengo la mkoa ni kilimo cha mkonge kiweze kunufaisha wakulima wadogo.

Amsema kuwa ni muhimu vyama hivyo kuja na mpango wao Ili wakati mkoa ukijipanga uone ni hatua zipi za kuchukua Ili kutimiza azma hiyo Kwa pamoja kwani mkakati uliopo ni kuhakikisha zao hilo linazalishwa kwa wingi na wakulima wadogo.

"Badala ya kukaa na kusubiri mipango ya serikali nendeni mkajadiliane kisha mje na mkakati wenu kwanza wa kuongeza uzalishaji lakini na ushauri wa nini cha kufanya Ili kufikiwa Kwa lengo la uzalishaji wa tani 50,000 ifikapo mwaka 2025," amesema Rc Malima.


Ameongeza kuwa mpaka sasa uzalishaji wa zao hilo kitaifa umefikia tani 39,000 huku  Mkoa wa Tanga pekee unazalisha tani 28,000 kati ya hizo tani 6,000 zinatokana na wakulima wadogo walioko kwenye vyama vya msingi.


"Sasa mimi nataka mjitahidi uzalishaji wenu uweze kufikia angalao tani 20,000 Kwa mwaka nyie vyama vya msingi kwani najua uwezo huo ,na hizi tani 50,000 najua Kwa kupitia wakulima wakubwa tutaweza kufikia lengo hilo,” amesema Malima.


Aidha RC Malima amewataka viongozi wa Vyama vya Ushirika kuendelea kutoa elimu Kwa wanachama wao Ili waweze kuona umuhimu wa kujiunga na vyama vya Ushirika Kwa ajili ya maendeleo Yao nataifa Kwa ujumla


Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Tanga, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tanga, John Henjewele amesema  kuwa muda mrefu vyama hivyo vinakabiliwa na changamoto ya idadi ndogo ya wanachama hali ambayo inasababisha kutofikiwa kwa malengo ya kunufaika na uwepo wa vyama hivyo.


"Licha ya ushirika kuwa kimbilio la wananchi wengi lakini kwa Tanga ushiriki ni mdogo hususani kwenye vyama vya akiba na mikopo jambo ambalo linasababisha kutofikiwa lengo la ushirika," amebainisha  Henjewele.


Pia, ameipongeza Serikali Kwa kuja na mpango wa kuuza korosho Kwa njia ya stakabadhi ghalani kwani Kwa muda mrefu zao la korosho limekuwa likiuzwa kwa bei ya chini hivyo Kwa kuanza kutekeleza mfumo huo umewasaidia wakulima kunufaika zao hilo.