Vyuma vya anuani za makazi vyaadimika

Meneja wa wakala wa barabara za mijini na vijijini (Tarura) Mkoa wa Kilimanjaro Nicholaus Francis.

Muktasari:

  • Meneja wa Tarura Mkoa wa Kilimanjaro, Nicholaus Francis amesema wanakabiliwa na upungufu wa vyuma vya kuweka anwani za makazi hali inayochelewesha kazi.

Moshi. Ukosefu wa vyuma kwa ajili ya Postikodi, imetajwa kuwa moja ya changamoto inayowakabili wakala wa barabara za mijini na vijijini (Tarura) Mkoa wa Kilimanjaro, katika uwekaji wa anuani za makazi.

Meneja wa Tarura Mkoa wa Kilimanjaro, Nicholaus Francis amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, kuhusu na uwekaji wa anuani za makazi katika barabara zilizoko chini yao.

Amesema hadi kufikia sasa uwekaji wa anuani za makazi umefikia asilimia zaidi ya 40, kwa Mkoa huo na hadi kufikia Mei 31, mwaka huu, watakuwa wamefikia zaidi ya asilimia 60.

Amesema changamoto iliyojitokeza ni kuadimika kwa vyuma kwa ajili ya postikodi na kwamba tayari wameagiza na kuzungumza na Sido, ili vitakapopatikana kazi ifanyike jwa haraka na kukamilisha shughuli hiyo.

"Tayari tumekwenda Sido kuwapa kazi ya kutengeneza vibao vya anuani za makazi katika barabara zote lakini tatizo lililojitokeza ni kwamba hivi vyuma kwa ajili ya posticodi vimeadimika kwa sababu ni nchi nzima vinahitajika."

Ameongeza kuwa, "tumeuliza Dar es salaam tumeambiwa hakuna mzigo wa kutosha, Arusha tumeambiwa lamda baada ta wiki mbili hadi tatu ndiyo wanaweza kuwa na hivyo vyuma lakini kazi inaendelea kama maelekezo ya serikali yalivyoelekeza na hadi Mei 31 zoezi hili, tunaweza kufikia asilimia zaidi ya 60."

Aidha amesema Mkoa wa Kilimanjaro una barabara 2,655 zenye kilometa 4,625 ambazo zimesajiliwa na wanapaswa kuweka anuani za makazi 5,310.

"Tarura tulipokea maagizo kwa ajili ya uwekaji anuani za makazi (Postcode) kwenye barabara zetu zote tunazozihudumia na katika Mkoa mzima tuna barabara karibu 2,655 ambazo zimesajiliwa zenye kilometa 4,625," alisema.

"Awali tulipokea maelekezo kila barabara tutakayo itengeneza, tuweke anuani za makazi na katika bajeti ya mwaka huu inayoendelea, tulikuwa tumejiandaa kuweka anuani za makazi 601 kwa barabara zinazoendelea kufanyiwa matengenezo"

"Baadae tukapewa maagizo ya kuweka anuani za makazi katika barabara zote, tukajikuta tunatakiwa kuweka posticodi badala ya 601, sasa tunatakiwa kuweka posticodi 5,310, ambazo gharama zake ni zaidi ya Sh910 milioni," alisema.

Akizungumzia suala la malipo, Meneja alisema kwa Tarura hakuna utaratibu wa wananchi kuchangia lakini kama kuna mtu anataka kujitolea kufadhili kibao cha mtaa wake hazuiliwi.