Waagizwa wasilete ubabe wakitakiwa kuvunja ukuta, vibanda vyao

Mwenyekiti wa Halmshauri ya Mji wa Kibaha, Mussa Ndomba akizungumza na wakazi wa Sofu Mjini Kibaha Wakati wa hafla ya kumtambulisha Mkandarasi atakayejenga barabara kwa kiwango cha lami ambayo inatakiwa kukamilika kwa kipindi cha miezi saba. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

  • Wakazi Kata ya Sofu waombwa kutoa ushirikiano kwa mkandarasi wa ujenzi wa barabara ili ukamilike kwa wakati.

Kibaha. Wakazi wa Kata ya Sofu Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mkoa wa Pwani wametahadharishwa kutoweka vikwazo vitakavyosababisha kuchelewa kukamilika ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kwani kufanya hivyo watakuwa wanarudisha nyuma maendeleo kwenye eneo lao.

Tahadhari hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani, Mussa Ndomba kwenye hafla ya utambulisho wa mkandarasi aliyepewa zabuni ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami  yenye urefu wa mita 700 ambao unatakiwa kukamilika kwa kipindi cha miezi saba.

"Mkandarasi yukó tayari hivyo ni vyema mkatoa ushirikiano ukiambiwa sogeza kibanda chako barabara ipite au vunja ukuta ni vyema ukatii ili kuharakisha maendeleo,"amesema.

Amesema kuwa kupelekwa mradi huo kwenye eneo lao ni bahati kwani maeneo mengi yana uhitaji hivyo kama wataanza kuweka vikwazo watakuwa hawajitendei haki.

"Tunamshukuru Rais wetu mama Samia Suluhu kwa kutupatia Sh1 bilioni ambazo zinatokana na tozo ya miamala ya simu na ndizo tumeziingiza kwenye mradi huu,"amesema.

Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa mitaa 700 utagharimu zaidi ya Sh943 milioni   pesa kutoka Serikali Kuu  zilizopatikana kutokana na tozo za miamala ya simu.

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa kata hiyo wamemuomba mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga barabara hiyo kutoa kipaumbele cha nafasi za kazi kwa wakazi wa eneo hilo ili wafaidi na kodi zao.

"Tunaomba Mkandarasi alieleewe hilo tuna vijana wengi wenye nguvu na afya njema wanaoweza kufanya kazi, hivyo wafikiriwe kupatiwa nafasi za kufanya kazi kwenye mradi huu," amesema Iddi Alfani.

Naye Jesca Saimoni amesema kuwa endapo mkandarasi huyo atawafikiria na kuwapa kipaumbele cha nafasi za kazi, vijana wazawa wa eneo hilo kutaimalisha mahusiano bora kwa pande zote mbili jambo ambalo ni jema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sofu,  Ester Mainoya amesema kuwa ni jambo la faraja kupata mradi huo wa barabara ya kiwango cha lami ngumu kwenye maeneo yao kwakuwa walisubiri kwa hamu kwa miongo mingi.

"Wananchi wamekuwa wakipata tabu ya usafiri, lakini barabara hii ikikamilika naamini tutapata usafiri wa daladala,"amesema.

Kwa upande wake Yohana John amesema kuwa barabara hiyo itakapokamilika italeta ahueni kwa jamii nzima ikiwemo wanafunzi na wagonjwa.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), Mhandisi  Bupe Anjetile amesema baadhi ya kazi anazotakiwa kufanya mkandarasi huyo ni kusafisha eneo la barabara, kuondoa udongo  laini wa juu, kuandaa matabaka mbalimbali pamoja na kujenga makaravati na mitaro na kukamilisha katika hatua zote.

Kwa upande wake, mkandarasi huyo Mhandisi Baltazar Malamsha  wa Kampuni ya M/S Globalink General Contractors Ltd amesema kuwa ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati anaomba ushirikiano kutoka kwa wananchi katika nyanja mbalimbali ikiwemo usalama wa vifaa vya kazi.